Jumanne, 22 Septemba 2026

TMJA RUKWA YAFANYA MAFUNZO, UTALII MKOANI MBEYA

Na SHARIFU MNKANGARA –Mahakama, Sumbawanga

Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Tawi la Rukwa, kimefanya ziara ya siku nne katika fukwe za Matema zilizopo Ziwa Nyasa wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya, ziara hiyo ilihusisha pia mafunzo ya kubadilishana uzoefu, utalii katika fukwe hizo na kufanya michezo mbalimbali ya kuimarisha afya ya mwili na akili kwa wanachama hao.

Ziara hiyo ya kuelekea Matema Beach ilianza tarehe 17 Septemba, 2026 kutoka Sumbawanga, huku mafunzo ya kubadilishana uzoefu yaliyofuatiwa na kikao kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu na mikakati ya kusimamia shughuli za Chama.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Sumbawanga, ambaye pia ni mlezi wa Tawi hilo, Mhe. Frederick Kapela Manyanda, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Thadeo Mwenempazi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Sumbawanga, Mhe. Pamela Mazengo na Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga, Mhe. Kisasila Saguda, pamoja na wanachama wengine wa TMJA Tawi la Rukwa.

Akifungua Mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda alisema kuwa, mafunzo hayo kuhusu utekelezaji wa hukumu na amri za mahakama katika mashauri ya madai (Execution of Civil Decree and Order) ni muhimu kwani yatawasaidia kuongeza ujuzi katika kutekeleza majuku yao ya kila siku.

Mafunzo hayo, yalitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba, Mhe. Raymond Kaswaga ambayo yalijikita katika taratibu za utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama, changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji pamoja na makosa mbalimbali yanayofanywa katika hatua za utekelezaji.

Aidha, Mafunzo hayo yaliambatana na majadiliano ya vikundi vilivyolenga kuwawezesha washiriki kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama.

Katika kikao hicho, kilichofanyika baada ya mafunzo, iliazimiwa kwamba, wanachama wapate nafasi ya kukutana kila mwezi kwa mzunguko ya ki-wilaya ili kutathimini muenendo mzima wa Chama katika Tawi na kufuatilia utekelezaji wa maazimio yanayowekwa na kupata nafasi ya kutembelea wahitaji.

Sambamba na hilo, kikao kilifanya uchaguzi wa Mtunza Fedha wa TMJA Tawi la Rukwa kufuatia kuhamishwa kituo kwa Mhe. Wilington Rwabinyasi aliyekuwa Mweka Hazina wa Tawi, na uchaguzi Hakimu Mkazi, Mhe. Hilda Mavoa kutoka Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Sumbawanga.

Katika kuendelea na ziara hiyo, kulifanyika michezo mbalimbali kama chemsha bongo iliyohusisha kesi maarufu na muhimu za kisheria (famous and land mark cases) ambapo wanachama walipaswa kueleza kanuni na uamuzi uliotolewa katika kesi husika.

Michezo mingine ilikuwa, kuvuta kamba, kukimbia na magunia, kucheza drafti, karata, mbio za aina mbalimbali burudani iliyolenga kuimarisha afya na kukuza ushirikiano. 

Baada ya michezo hiyo, washindi walikabidhiwa medali na zawadi mbalimbali na Mlezi wa Tawi, Mhe. Manyanda. Makabidhiano hayo ya medali na zawadi yalishuhudiwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya ambaye alishiriki michezo hiyo kama mwenyeji wa Mkoa huo.

Katika tukio hilo, Mhe. Manyanda pia alikabidhiwa zawadi ya kikombe na Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Rukwa, Mhe. Nickson Temu, kwa kutambua mchango wake katika ulezi wa Chama hicho. 

Akizungumza mara baada ya michezo hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Thadeo Mwenempazi alisema kuwa, michezo ina nafasi muhimu katika afya na utendaji wa kitaaluma wa watumishi.

“Msione kwamba zawadi ni kidogo, zina maana kubwa sana katika mambo yote ya utendaji kazi wetu. Lakini pia kuna haja ya kuhakikisha afya zetu zinakuwa sawa ili kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu ya kila siku,” alisema Mhe. Mwenempazi.

Mhe. Mwenempazi aliongeza kuwa, mashindano ya chemsha bongo yalitoa fursa kwa wanachama kuendelea kujifunza kuhusu kanuni mbalimbali zinazohusiana na maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani na kushauri kiwe kitu endelevu kwa kuendelea kuchambua maamuzi na kuwashirikisha wengine katika kundi sogozi na kuwepo kwa tuzo kwa mwanachama atakayeonesha umahiri katika eneo hili.

Ziara hiyo ilihitimishwa tarehe 20 Septemba, 2026 kwa safari ya kurejea Sumbawanga, ikiwa imewakutanisha wanachama katika shughuli za kitaaluma, kiutawala, kiutalii na michezo kwa lengo la kuimarisha umoja, mshikamano na kushirikiana baina ya wanachama.

Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Rukwa wakiwa katika picha ya pamoja katika fukwe za Matema zilizopo Ziwa Nyasa maarufu kama Matema Beach, Wilaya ya Kyela Mkoa wa  Mbeya katikati walioketi ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala, Ndogo Mhe. Frederick Kapela Manyanda na Viongozi wengine waandamizi.

Sehemu ya washiriki wa michezo mbalimbali iliyokuwa ikichezwa katika ziara hiyo iliyoambatana na Mafunzo na utalii katika Fukwe za Matema Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya.


Sehemu ya washiriki wa michezo mbalimbali iliyokuwa ikichezwa katika ziara hiyo iliyoambatana na Mafunzo na utalii katika Fukwe za Matema Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala, Ndogo Mhe. Frederick Kapela Manyanda (katikati) akikabidhiwa zawadi ya kikombe na Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Rukwa, Mhe. Nickson Temu (kushoto) kwa kutambua mchango wake katika ulezi wa Chama hicho na (kulia) ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya ambaye alishiriki michezo hiyo Mhe. Fahamu Mtulya, kama mwenyeji wa Mkoa pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Thadeo Mwenempazi  (kulia).

Sehemu ya wanachama  TMJA walioshindi michezo mbalimbali na kutunikwa medali na zawadi mbalimbali katika mabonaza wakati wa ziara hiyo. 

Mwenyekiti wa TMJA tawi la Rukwa Mhe. Nickson Temu (aliyesimama) wakati wa majadiliano ya maazimio ya Chama hicho.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba Mhe. Raymond Kaswaga (aliyesimama mbele) akitoa mada wakati mafunzo ya taratibu za utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama.

Sehemu ya Washiriki wa mafunzo hayo ya (Execution of Civil Decree and Order) wakifatilia kwa umakini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala, Ndogo Mhe. Frederick Kapela Manyanda (katikati aliyesimama) akifungua kikao kilichoanza kwa mafunzo, (kushoto) ni Thadeo Mwenempazi Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga, (kulia) Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Mhe. Pamela Mazengo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha -Mahakama) 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni