Jumatatu, 28 Septemba 2026

MAHAKIMU 23 TMJA SHINYANGA WAZULU HIFADHI YA TAIFA GOMBE KIGOMA

  • Wafurahia na kustaajabu baada ya kujionea Sokwe wenye asili ya kipekee

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Timu ya Mahakimu 23 Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Shinyanga imefanya ziara ya kihistoria katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe mkoani Kigoma tukio lililoacha alama ya aina yake huku likiacha simulizi nyingi za kuvutia.

Ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki ilianza tarehe 25 Septemba, 2026 na kuhitimishwa tarehe 26 Septemba mwaka huu, ililenga sio tu kupumzisha akili kutokana na majukumu mazito ya kutoa haki, bali pia kujionea urithi wa asili na utalii wa kipekee wa Sokwe Mtu ambao ulimfanya Mtafiti maarufu duniani, Dkt. Jane Goodall kuweka kambi yake hapo miongo kadhaa iliyopita.

Mapema Asubuhi ya tarehe 26 Septemba, 2026, kikosi hicho kilichojumuisha Mahakimu 23 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga, kilianza safari kwa boti kupitia maji safi na ya bluu ya Ziwa Tanganyika kuelekea ufukweni mwa Hifadhi ya Gombe huku mandhari ya milima ya kijani kibichi inayoteremka moja kwa moja hadi ziwani ikianza kuwakaribisha wageni hao kwa shangwe za kimya kimya za upepo mwanana.

Akizungumza kwa niaba ya Wanachama hao, Mhe. Mariki alieleza kuwa, ziara hiyo ilikuwa ni fursa adhimu ya kujionea kwa macho urithi wa Taifa ambao umekuwa kivutio kikubwa cha kimataifa.

"Kazi ya utoaji haki inahitaji utulivu mkubwa wa akili na mtazamo mpana. Kuja hapa Gombe hakutupi tu nafasi ya kupumzika, bali kunatufanya tuzidi kuuthamini utajiri wa nchi yetu na kuona umuhimu wa kulinda mazingira na sheria zinazolinda maliasili zetu," alisema Naibu Msajili huyo.

Aidha, sehemu kubwa ya ziara hiyo ilikuwa ni kupanda milima ya hifadhi hiyo kuwatafuta sokwe maarufu chini ya uongozi wa Waongoza Watalii wenye uzoefu kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mahakimu hao walipitia njia za msitu mnene hadi walipofanikiwa kukutana na familia ya Sokwe waliokuwa wakila matunda na kucheza kwa uhuru.

Tukio hilo liliibua mshangao na furaha tele, Mahakimu hao walipata fursa ya kujifunza tabia za Sokwe hao ambao wanafanana kwa asilimia kubwa na binadamu, kuanzia mfumo wao wa maisha, mihemuko, hadi namna wanavyojali familia zao.

Ziara hiyo haikuishia tu kwenye kutazama Sokwe, bali pia ilijumuisha mafunzo ya uhifadhi wa mazingira, umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji vya Ziwa Tanganyika, na jinsi sheria za nchi zinavyoweza kuendelea kulinda Wanyamapori dhidi ya ujangili yaliyotolewa na Muongoza Watalii, Bw. Ahadi Boazi.

Alieleza kuwa, Hifadhi ya Taifa Gombe ipo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika kwa upande wa Magharibi iliyotangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa katika gazeti la Serikali la mwaka 1968, lenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 56, na jumla ya Sokwe 98, hivyo katika kulinda Makazi na ongezeko la Sokwe katika eneo hilo la Gombe Mkoani Kigoma Serikali imeendelea kulitunza kwa weledi mkubwa ili familia za Sokwe ziweze kuishi kwa miaka mingi bila muingiliano na shughuli za binadamu.

Hatimaye, kikosi hicho kiliondoka Gombe kikiwa kimebeba kumbukumbu zisizofutika na ari mpya ya kutekeleza majukumu yao ya kisheria huku wakiwa mabalozi wazuri wa utalii wa ndani na uhifadhi wa mazingira nchini Tanzania,

Vilevile, Mahakimu hao walipata wasaa wa kupita na kujionea Mji mkongwe wa Kigoma Ujiji, pamoja na uhifadhi wa kumbukumbu za Dkt. Livingstone Ujiji, ambapo walijionea, zana mbalimbali za Dkt. Livingstone pamoja Stanley walipokutana katika mji huo, sambamba na kuona Msikiti uliojengwa Mwaka 1840, pamoja na Nyumba pekee aliyolala Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, alipozulu Mji wa Kigoma Ujiji katika shughuli za harakati za uhuru wa Tanganyika.


Picha ya pamoja ya  Mahakimu 23 Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA)  Tawi la Shinyanga wakiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki (aliyeketi katikati). Kushoto ni Mwenyekiti wa TMJA-Shinyanga, Mhe. Yusuph Zahoro na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Tawi hilo, Mhe. Johannes Mbatina na wengine ni Mahakimu na Wanachama wa TMJA-Shinyanga waliofika Mkoani Kigoma kufanya utalii katika Hifadhi ya Taifa Gombe.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki akiwa katika Hifadhi ya Taifa Gombe akiwaongoza Wanachama wa TMJA-Shinyanga.

Ofisa Mwongoza Watalii katika Hifadhi ya Taifa Gombe, Bw. Ahadi Boazi akitoa maelezo kwa Mahakimu juu ya historia ya maisha ya Sokwe katika Hifadhi ya Taifa Gombe na uhifadhi wake.

Sehemu ya Timu ya Mahakimu 23 Wanachama wa TMJA-Shinyanga, waliofika katika kilele cha mlima uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Gombe wakiwa na nyuso za furaha ambapo ndio walikutana na familia ya Sokwe waliokuwa katika harakati za kujitafutia chakula cha matunda katika hifadhi hiyo.

Moja ya  Sokwe waliokuwa katika harakati za kujitafutia chakula cha matunda katika hifadhi hiyo akiwa ametulia akitazama wanadamu ambao nao walikuwa wakimtazama kwa mshangao kufuatia uumbaji wake unaofanana na wanadamu.

Picha ya sehemu ya Timu ya  Mahakimu 23 Wanachama wa TMJA-Shinyanga,wakisikiliza kwa makini maelekezo kutoka kwa Mwongoza Watalii katika eneo maaalum lililopo katika Hifadhi ya Taifa Gombe.

Sokwe dume na jike waliokuwa katika harakati za kujitafutia chakula katika hifadhi hiyo wakiwa wametulia wakitazama wanadamu ambao nao walikuwa wakiwatazama kwa mshangao.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni