Alhamisi, 1 Oktoba 2026

JAJI FREDERICK MANYANDA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MAGEREZA

Na SHARIFU MOKIWA – Mahakama, Sumbawanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Sumbawanga, Mhe. Frederick Kapela Manyanda amefanya ziara ya ukaguzi katika Gereza la Kilimo Mollo na Gereza la Mahabusu Manispaa ya Sumbawanga kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wafungwa na mahabusu, kutathimini utendaji kazi na kukagua mazingira wanayoishi.

Ziara hiyo ni sehemu ya ukaguzi wa robo ya tatu unaofanywa na Mahakama, Jaji Mfawidhi alipata wasaa wa kupokea taarifa ya hali za magereza hayo na kupata fursa ya kuzungumza na wafungwa na mahabusu, kusikiliza changamoto mbalimbali kuzitolea majibu kwa kushirikiana na wadau wa haki jinai.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Manyanda alisema kuwa, ukaguzi huo umelenga kusikiliza hoja na changamoto mbalimbali kutoka kwa wafungwa na mahabusu ili kuona namna zinavyoweza kushughulikiwa na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Mahakama na Magereza.

“Tunakuja kuwatembelea ili kusikiliza hoja, shida mbalimbali, kwa sababu sisi na ninyi ni kitu kimoja. Kuna maisha baada ya hapa, yeyote anaweza akaja hapa na akatoka,” alisema Jaji Manyanda.

Katika Gereza la Kilimo Mollo, Mkuu wa Gereza hilo, SSP Sebastian J. Mganga, aliwasilisha changamoto mbalimbali zinazohusiana na utendaji wa mfumo wa Haki Jinai, ikiwemo kucheleweshwa kwa wito wa Mahakama ya Rufani, kucheleweshwa kwa nakala za hukumu, changamoto ya upatikanaji wa vitabu, pamoja na mambo yanayohusu Mahakama Mtandao.

Gereza la Kilimo Mollo lina jumla ya wafungwa 216. Aidha, wafungwa katika gereza hilo wanashiriki katika shughuli za urekebu zinazofanyika ndani ya gereza.

Baada ya kutembelea Gereza la Kilimo Mollo, ziara ilifanyika pia katika Gereza la Mahabusu Sumbawanga, ambapo Mhe. Manyanda alipata pia fursa ya kusikiliza na kuzungumza na uongozi wa gereza hilo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na mfumo wa Haki Jinai.

Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Ally Abdalah Mgaya, alimshukuru Jaji Mfawidhi pamoja na wadau alioambatana nao kwa ziara hiyo na kuwakaribisha kwa kaguzi nyingine kwa lengo la kusikiliza changamoto na kufahamu maendeleo ya mahabusu na wafungwa.

Ziara hiyo ni muhimu kwa Mahakama na wadau wa haki jinai katika kutathmini utendaji kazi wao na namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku ikiwemo kusimamia masuala yote ya kijinai.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Sumbawanga, Mhe. Frederick Kapela Manyanda (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa haki jinai wakiwa katika gereza la mahabusu Sumbawanga.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo Sumbawanga, Mhe. Pamela Mazengo (wa kwanza kulia), Naibu Msajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga Mhe. Kisasila Saguda (wa kwanza kushoto) waliokaa meza moja na Maafisa wa Magereza wakati wa ziara hiyo katika gereza la kilimo la mollo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda (katikati) wakati akisikiliza taarifa fupi kutoka kwa Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Ally Abdalah Mgaya (kushoto aliyesimama) akiwasilisha ripoti fupi baada yakufika Gerezani hapo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Sumbawanga, Mhe. Frederick Kapela Manyanda (kushoto) akiwasili Gereza la Mahabusu Sumbawanga kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wafungwa na mahabusu, kutathimini utendaji kazi na kukagua mazingira wanayoishi, (kulia) ni Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Ally Abdalah Mgaya akimkaribisha gerezani hapo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Sumbawanga, Mhe. Frederick Kapela Manyanda (aliyeketi kiti cha mbele) wakati akisikiliza taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Mollo Sumbawanga SSP Sebastiani J. Mganga (kulia aliyesimama)

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Sumbawanga, Mhe. Frederick Kapela Manyanda (kushoto) akipokelewa na Mkuu wa Gereza la Mollo Sumbawanga SSP Sebastiani J. Mganga pamoja na Maafisa wengine wa Jeshi hilo mara baada ya kuwasili katika ziara ya ukaguzi wa Gereza la Kilimo Mollo Sumbawanga kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wafungwa na mahabusu.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni