Jumamosi, 17 Oktoba 2026

JAJI MAFAWIDHI TANGA ATAKA MATOKEO CHANYA KATIKA KAZI

Na MUSSA MWINJUMA-Mahakama Kuu, Tanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Tanga, Mhe. Abdallah Gonzi, amewahimiza Viongozi wa Mahakama mkoani Tanga kuangalia vipaumbele na kuweka mipango madhubuti ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi.

Mhe. Gozi alitoa wito huo jana tarehe 16 Oktoba, 2026 wakati anaongoza kikao cha Menejimenti kilichofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Tanga.  

“Nawapa rai viongozi wenzangu, tangalie vipaumbele na kuweka mipango madhubuti katika utendaji kazi kwa kutumia akili na utashi. Usipobadilika katika utendaji kazi huwezi kupata mafanikio, angalia vipaumbele ili kukamilisha shughuli muhimu ndani ya ofisi,” alisema.

Akitumia msemo wa Kiswahili, Jaji Gonzi alisema, “Kata Pua, unda wajihi,” akimaanisha elekeza rasilimali katika mambo ya msingi ya utendaji kazi, huku ukipata athari chache katika maeneo mengine ili kufanikisha shughuli za ofisi.

Akizugumza wakati anafungua kikao hicho, Mhe Gonzi alieleza lengo la vikao kama hivyo ni kutafuta tija katika utendaji kazi.

Taasisi ni nafsi ya kisheria, kuna mambo madogo ambayo yanazorotesha utendaji kazi, lakini kutokana na ukubwa wa Taasisi yanaweza yasionekane, kujulikana ama kusahaulika. Ndio sababu kubwa ya kuwa na vikao kama hivi,” alisema.

Jaji Gonzi alieleza pia kuwa ni lazima kuwe na michakato ya ndani ya namna ya kutatua matatizo yaliyopo ndani ya Masjala kwani wamekabidhiwa nyenzo na rasilimali mbalimbali ili kutimiza malengo ya Taasisi.

Alisisitiza kuwa pamoja na uwepo wa upungufu wa rasilimali hizo, bado wana wajibu wa kutimiza majukumu na kuhakikisha malengo ya Taasisi yanafikiwa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Messe Chaba na Mhe. Happiness Ndesamburo, Naibu Msajili, Mhe. Hudi Majid Hudi na Mtendaji wa Mahakama, ambaye ni Katibu wa kikao hicho, Bw. Jumanne Msuta.

Taarifa mbalimbali za mashauri na kiutendaji ziliwasilishwa wakati wa kikao hicho. Akichangia kwenye kikao hicho, Mhe. Ndesamburo alieleza Mahakama inawatumishi wengi, hivyo kila mmoja anatakiwa kujitofautisha katika utendaji kwa kutumia kidogo alichonacho kutatua changamoto kwenye eneo lake la kazi.

Mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mhakama Kuu Masjala Ndogo Tanga, Mhe. Abdallah Gonzi, akiongoza kikao cha Menejimenti. Kulia kwake ni Jaji Messe Chaba na Kushoto kwake ni Jaji Happiness Ndesamburo.

Katibu wa kikao ambaYe pia ni Mtendaji wa Mahakama Tanga, Bw. Jumanne Msuta akiwa katika majukumu ya kikao hicho. Kushoto kwake ni Naibu Msajili, Mhe. Hudi Majid Hudi na mwisho ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Simon Kobero.

Jaji Mfawidhi wa Mhakama Kuu Masjala Ndogo Tanga, Mhe. Abdallah Gonzi, akiwa na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Tanga.

Jaji Mfawidhi wa Mhakama Kuu Masjala Ndogo Tanga, Mhe. Abdallah Gonzi, (katikati) akiwa na Mhe. Messe Chaba (kulia kwake) na Mhe Happiness Nesamburo (kushoto kwake). Waliosimama kutoka kushoto ni Mtendaji wa Mahakama, Bw. Jumanne Msuta, anayefuata ni Naibu Msajili, Mhe. Hudi Majid Hudi na mwisho ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Simon Kobero.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni