Na NOEL SYLIVESTER Mahakama Kuu Masjala Ndogo Songea,
Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji mkoani Songea jana tarehe 16 Oktoba, 2026 lilitoa mafunzo
kwa watumishi wa Mahakama ili kuwaongezea uelewa na
uwezo wa kukabiliana na majanga, kuokoa maisha na kulinda mali.
Mafunzo hayo ya usalama dhidi ya majanga ya moto na mbinu za uokoaji yalifanyika
katika maeneo ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Songea, yakihusisha nadharia
pamoja na vitendo.
Mkufunzi kutoka Jeshi hilo, Afande
Roden Mlimbila, aliwapatia washiriki elimu kuhusu masuala ya usalama dhidi ya
moto, hatua za kuchukua wakati wa kutokea janga la moto, pamoja na mbinu za
kutumia vifaa vya kuzimia moto na taratibu za uokoaji.
Kupitia mafunzo ya vitendo, washiriki walipata
fursa ya kujifunza kwa vitendo namna ya kutumia vifaa vya kuzimia moto na
kuzingatia hatua muhimu za kiusalama wakati wa kukabiliana na majanga, ili
kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza katika mazingira ya kazi na maeneo
mengine.
Akizungumza kwa niaba ya Mahakama Kuu Songea,
Afisa Tawala, Bi. Khadija Ngayonga, alilishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa
kutoa mafunzo hayo, akieleza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kuimarisha
usalama wa watumishi, wananchi wanaofika mahakamani pamoja na mali za Taasisi
hiyo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utayari wa watumishi wa Mahakama katika kukabiliana na dharura, kwa kuzingatia umuhimu wa kuchukua tahadhari, kufuata maelekezo ya wataalamu na kuhakikisha mazingira ya utoaji wa huduma za kimahakama yanakuwa salama.
Picha ya pamoja ya watumishi
wa Mahakama Kuu Songea wakiongozwa na Afisa Tawala, Bi Khadija Ngayonga (wa pili
kutoka kushoto aliyevaa ushungi) na Wakufunzi
wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (waliovaa sare).
Mkufunzi kutoka Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji, Afande Roden Mlimbila wakati wa kutoa mafunzo.
Wakufunzi kutoka Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji wakifundisha kwa vitendo.
Mtumishi wa Mahakama
akielekezwa na Mkufunzi namna ya kushika na
kutumia mtungi wa gesi ya kuzimia moto.
Mtumishi wa Mahakama
akizima moto kwa kutumia mtungi maalumu wa kuzimia moto kwenye mafunzo ya
vitendo.
Habari hii imhaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni