Jumatano, 28 Oktoba 2026

JOPO LA MAJAJI WA RUFANI LAFANYA KIKAO NA MAOFISA MAHAKAMA MBEYA

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya 

Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania limekutana na Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Wilaya na Mahakama za Mwanzo zilizopo jijini Mbeya kwa ajili kuwajengea na kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma na kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia weledi na kulinda maadili wanapotekeleza majukumu yao.

Aidha, Jopo hilo limewasisitiza Mahakimu hao kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kujifunza kwa kuzingatia uzoefu wa wengine katika  usikilizaji wa mashauri, uandaaji wa mienendo ya mashauri na uandishi wa hukumu ili kuboresha ufanisi katika utoaji haki.

Akizungumza katika kikao hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Amour Said Khamis, alisisitiza umuhimu wa Mahakimu kulinda heshima na hadhi ya taaluma ya sheria kwa kuzingatia maadili mema katika maisha yao ya kikazi na kijamii inayowazunguka. Ameongeza kuwa, Mahakimu wana nafasi muhimu katika jamii na hivyo wanapaswa kuwa mfano bora wa uadilifu na mwenendo unaostahili.

“Hakimu anatazamwa na watu wengi wanaomzunguka. Hakimu ni mtu mwenye heshima kubwa katika jamii yetu. Tujitahidi sana kulinda heshima zetu na tujikite sana katika kulinda maadili mema, iwe ndiyo utamaduni wetu,” alisema Mhe. Khamis.

Aidha, Mhe. Khamis aliwataka Mahakimu kujenga utamaduni wa kupendana, kushirikiana na kusaidiana katika utekelezaji wa majukumu yao, akibainisha kuwa ushirikiano ni nyenzo muhimu ya kuongeza maarifa, kutatua changamoto na kuboresha utendaji kazi ndani ya Mahakama.

“Huhitaji kumzungumzia mwenzako vibaya mbele yake au mbele ya jamii. Tupendane na tusaidiane, Mahakama ni familia moja. Pale unapoona kwako kuna mapungufu na mwenzako anajua, jifunze kutoka kwake,” alisisitiza Mhe. Khamis.

Katika hatua nyingine, Jopo hilo liliwahimiza Mahakimu kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na matumizi ya TEHAMA, hususani mfumo wa TanzLII, kwa ajili ya kupata na kujifunza kupitia hukumu mbalimbali zilizotolewa na Mahakama za juu na hasa Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Ilielezwa kuwa kujisomea hukumu hizo kutawasaidia kupanua uelewa wa kisheria, kuboresha uchambuzi wa masuala ya Sheria na kuimarisha ubora wa hukumu wanazoziandika.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Abeesiza Laurean Kalegeya, aliwataka Mahakimu kuwa na ari ya maendeleo ya kitaaluma kwa kujifunza kutoka kwa wenzao wenye uzoefu na maarifa zaidi.

Mhe. Kalegeya alisisitiza pia umuhimu wa kupendana, kuheshimiana na kukosoana kwa ukweli na kwa nia ya kujenga, akieleza kuwa utamaduni huo utasaidia kuongeza ufanisi na kuimarisha mahusiano ya kikazi. 

Mwenyekiti wa Jopo la Majaji hao wa Mahakama ya Rufani Mhe. Zephrine Nyalugenda Galeba aliwashukuru Mahakimu kwa ushiriki wao na kuwataka kuendelea kulinda na kuinua thamani ya taaluma ya sheria kwa kuzingatia uadilifu, nidhamu na mwenendo mwema.

Mhe. Galeba alisisitiza kuwa, Mahakimu wanapaswa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kutambua wajibu wao mkubwa katika kulinda haki na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama. 

“Taaluma ya Sheria ni taaluma ya umashuhuri na umaarufu. Tunatakiwa kuchunga kila hatua ya maisha yetu, tusimamie haki, tuwe waadilifu na tuwe na tabia njema katika jamii zetu,” alisisitiza Mhe. Galeba.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na viongozi wa Mahakama Masjala ya Mbeya wakiwemo Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Angaza Ernest Mwipopo, Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Said Mashaka Kalunde pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Bernard Abel Mpepo.

Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jopo hilo, Jaji wa Rufaa ya Tanzania Mhe. Zephrine Nyalugenda Galeba (katikati) akiendesha kikao na Maofisa Mahakama wa jijini Mbeya, kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Amour Said Khamis na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Rabia Hussein Mohamed.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Abeesiza Lurean Kalegeya (aliyesimama) akizungumza katika kikao hicho, Kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Abel Mpepo.

Sehemu ya Maofisa Mahakama walioshiriki katika kikao hicho wakifuatilia kwa makini nasaa mbalimbali zilizokuwa zikitolewa wakati wa kikao hicho.

Sehemu ya Maofisa Mahakama walioshiriki katika kikao hicho wakifuatilia kwa makini nasaa mbalimbali zilizokuwa zikitolewa wakati wa kikao hicho.

Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania Mhe. Zephrine Nyalugenda Galeba, (katikati waliosimama mbele), wakiwa kwenye picha ya pamoja na Maofisa Mahakama jiji la Mbeya. Wengine ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Amour Said Khamis (wa pili kushoto), wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Rabia Hussein Mohamed, (wa kwanza kushoto) ni Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Ernest Mwipopo na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Said Kalunde.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Mbeya Mhe. Paul Rupia (aliyesimama) akichangia jambo katika kikao hicho, kulia ni Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Scout Petter Andrew. 

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Ernest Mwipopo, (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao hicho cha Maofisa Mahakama na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

 







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni