Jumatano, 21 Oktoba 2026

KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA CHAFANYA ZIARA NJOMBE NA KATAVI

Na MWANDISHI WETU – Mahakama

Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania kinaendelea kuimarisha mawasiliano na wadau wa Mahakama kupitia ziara na mafunzo yanayolenga kuongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Kituo hicho, kukusanya mrejesho wa wananchi na kubaini changamoto zinazohitaji maboresho katika utoaji wa haki.

Katika robo ya tatu ya mwaka 2026, Kituo hicho kilifanya ziara mkoani Njombe na Katavi kwa lengo la kutathmini kiwango cha uelewa na kuridhika kwa wananchi na huduma za kimahakama, kusikiliza maoni, maswali, malalamiko na pongezi, pamoja na kubaini changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.

Ziara hiyo ilihusisha mahakama katika ngazi mbalimbali mikoani Njombe na Katavi kwa lengo la kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania, hususan Nguzo ya Tatu inayohusu ushirikishwaji wa wadau na kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama, sambamba na kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

Katika ziara hiyo, watumishi wa Kituo walikutana na watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo za Njombe na Katavi, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Mwanzo, Wateja waliofika siku husika kupata huduma katika Mahakama hizo, Wafungwa na Mahabusu ili kusikiliza maoni yao na kutoa elimu kuhusu majukumu ya Kituo na taratibu za kuwasilisha mrejesho. Ambapo katika ziara hiyo hoja mbalimbali ziliibuliwa na kutolewa ufumbuzi.

Miongoni mwa hoja zilizojitokeza kwa Kanda ya Njombe ni pongezi kwa kuanzishwa kwa Masjala Ndogo ya Mahakama Kuu Njombe. Wadau pia walipendekeza kuongeza elimu kwa wafungwa na mahabusu kuhusu haki zao na namna ya kuwasilisha maoni, kupanua ziara hadi magereza ya Wilaya.

Kwa upande wa Mkoa wa Katavi, hoja mbali mbali ziliibuliwa ikiwemo pia Pongezi kwa Mahakama kuanzisha Masjala ndogo ya Katavi, Aidha, watumishi wa Kituo walitembelea Gereza la Mahabusu Mpanda na Gereza la Wafungwa la Kalilankulukulu.

Shughuli hizo zinaakisi umuhimu wa kuwafikia wadau wa Mahakama katika maeneo mbalimbali ili kuongeza uelewa kuhusu huduma za kimahakama na kuimarisha njia za wananchi kutoa mirejesho (Malalamiko, Maoni Maulizo na Pongezi).

Hakimu Mkazi Kituo cha huduma kwa mteja Mhe. Adrian Msisiri, akitoa elimu kwa watumishi.

Moja ya mtumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe akiuliza kupata  ufafanuzi juu ya maswala yaliyowasilishwa kuhusu kituo cha huduma kwa mteja.

Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala  Ndogo ya Njombe wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupata elimu ya huduma kwa Mteja.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Godfrey Isaya (wa tatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu  Msajili  wa Mahakama Kuu Mhe. Gwai Sumaye (wa tatu kulia) na Mtendaji wa Mahakama Epaphras Tenganamba (wa kwanza kulia) wakiwa pamoja na watumishi wa Kituo cha Huduma kwa mteja cha Mahakama ya Tanzania.

Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Katavi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Watumishi kutoka kituo cha huduma kwa mteja baada ya kupata elimu.

Sehemu ya Wanachi wa Mkoa wa Katavi wakipata Elimu juu ya Huduma za Mahakama na namna wanavyoweza kufaidika na kituo cha huduma kwa mteja. 

Watumishi kutoka Kituo cha huduma kwa Mteja wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mkuu wa Gereza Afande John Jeremia (wa pili kushoto) na Maafisa mwengine wa Gereza baada ya kutoa elimu katika gereza hilo.

Sehemu Watumishi kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Gereza la Kalilankulukulu  pamoja na Maafisa wengine wa Gereza.

(Habari Hii Imehaririwa na Dkt. Evetha E. Mboya)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni