Jumamosi, 24 Oktoba 2026

MAHAKAMA KUU GEITA YAZINDUA MAZOEZI YA PAMOJA

Na INNOCENT MWANDOJE, Mahakama Geita

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, imezindua rasmi programu ya mazoezi ya pamoja kwa watumishi wake, hatua inayolenga kuimarisha afya, ustawi wa mwili na akili pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Mahakama kwa wananchi.

Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu, ukihusisha Majaji, Mahakimu, watumishi kutoka idara mbalimbali pamoja na wadau wa Mahakama.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza, alisema kuwa afya bora ni msingi muhimu wa kuongeza tija kazini na kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwa weledi na ufanisi.

Alieleza kuwa mazoezi ya pamoja yatafanyika kila siku ili kuwapa watumishi fursa ya kushiriki shughuli za kuimarisha afya zao, huku wakijenga mshikamano na ushirikiano mahali pa kazi.

“Tunatambua umuhimu wa afya kwa watumishi katika kufanikisha shughuli za utoaji haki kwa wakati, hivyo kupitia mazoezi haya ya pamoja tunalenga kujenga nguvu kazi yenye afya njema, ari ya kazi na umoja,” alisema Jaji Kahyoza.

Kwa upande wa watumishi walioshiriki uzzinduzi huo walieleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema utasaidia kupunguza changamoto za kiafya zitokanazo na kukaa muda mrefu ofisini pamoja na kuongeza mshikamano na ushirikiano baina ya watumishi.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita imeendelea kuonyesha dhamira ya kuwajali watumishi wake kwa kuweka mazingira bora ya kazi yanayochangia afya njema, ustawi wa watumishi na kuimarisha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza akiteta na watumishi pamoja na wadau wa Mahakama waliohudhuria uzinduzi wa mazoezi ya pamoja.

Watumishi pamoja na wadau wa Mahakama wakimsikiliza kwa umakini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza katika uzinduzi wa mazoezi ya pamoja.

Watumishi pamoja na wadau wa Mahakama wakipasha misuli joto kwa pamoja kabla ya kuanza kwa mazoezi ya viungo vya mwili.

Mwalimu wa mazoezi akitimiza wajibu wake kwa kuwahamasisha watumishi na wadau wa Mahakama kuongeza bidii na kuwa makini wakati wa mazoezi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita Mhe. Projestus Kahyoza (wa pili kulia) kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa mazoezi baada ya kumalizika.

Habari hii imeharirwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni