- Yalenga kuwajengea uwezo Mahakimu, Wadau wa Haki Jinai kuhusu Utoaji na Utekelezaji wa Amri za Uangalizi na Huduma kwa Jamii
Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe imeendesha mafunzo kuhusu utoaji na utekelezaji
wa adhabu mbadala, zikiwemo amri za uangalizi na huduma kwa jamii lengo likiwa
ni kuwajengea uwezo Mahakimu na Wadau wa mfumo wa Haki Jinai kuhusu matumizi
sahihi ya adhabu hizo kwa mujibu wa sheria.
Mafunzo
hayo yalifanyika tarehe hivi karibuni na kuhudhuriwa na Mahakimu wa ngazi
zote wakiwemo wa Wilaya za mbali walioshiriki kwa njia ya mtandao. Washiriki
wengine walikuwa Mawakili wa Serikali, Maofisa wa Jeshi la Magereza na wadau
wengine wa mfumo wa Haki Jinai.
Mafunzo
hayo yaliratibiwa na Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola na kutolewa na Wataalam
kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Kitengo cha Huduma za Uangalizi
na Huduma kwa Jamii jijini Dodoma.
Akizungumza
wakati wa akitoa neno la utangulizi katika mafunzo hayo, Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano alisema
kuwa, matumizi sahihi ya Adhabu Mbadala yanaweza kusaidia kupunguza msongamano
wa wafungwa na mahabusu magerezani, pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji
kwa Serikali.
Alieleza
pia kuwa, adhabu hizo zina nafasi muhimu katika kumrekebisha mkosaji bila kumuweka
gerezani, pale ambapo sheria inaruhusu, huku akizingatia masharti yaliyowekwa
na Mahakama.
Mhe.
Luambano alisema kuwa, mafunzo hayo yameandaliwa kufuatia ukaguzi uliofanywa
hivi karibuni na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya
Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, ambao ulibaini maeneo yaliyohitaji kupewa
kipaumbele katika kuboresha utoaji na utekelezaji wa Adhabu Mbadala.
Akifungua
mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Victoria Nongwa alisema
kuwa, kufuatia ukaguzi alioufanya katika Mahakama za Mmwanzo hivi karibuni,
eneo la utoaji na utekelezaji wa amri za uangalizi na huduma kwa jamii ni
miongoni mwa maeneo yenye changamoto za utekelezaji miongoni mwa Mahakimu.
Kwa
sababu hiyo, aliona ipo haja ya kuandaa mafunzo hayo kwa haraka ili kuongeza
uelewa kwa Mahakimu na wadau wa mfumo wa haki jinai kuhusu sheria na taratibu
zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa amri hizo.
Mhe.
Nongwa alieleza pia, umuhimu wa adhabu mbadala kuwa ni kusaidia kupunguza
gharama kwa Serikali katika kuwatunza wafungwa Magerezani, kurudisha mamlaka ya
urekebu kwa jamii, kulinda utu wa mkosaji na kuwezesha mkosaji kurekebisha
mwenendo wake huku akihudumia familia yake.
Aidha,
ameeleza kuwa, aliona umuhimu wa kuwashirikisha wataalamu kutoka Kitengo cha
Uangalizi na Huduma kwa Jamii ambao, kwa kiasi kikubwa, wanahusika moja kwa
moja katika eneo hili la usimamizi wa amri hizo.
Kwa
sababu hiyo, Mhe. Nongwa aliwasisitiza washiriki kushiriki kikamilifu katika
mafunzo hayo kwa kutoa mawazo yao, kuuliza maswali na kuelezea uzoefu wao
katika eneo hilo.
“Ni
imani yangu kuwa, baada ya mafunzo haya, sio tu kwamba matumizi ya adhabu
mbadala yataongezeka, bali pia taratibu na michakato yote ya utoaji na
utekelezaji wa adhabu hizo mbadala itazingatiwa kikamilifu. Ili kufanikisha
hilo, nawaomba mshiriki kikamilifu mafunzo haya kwa kutoa mawazo na maoni yenu,
kuuliza maswali na kuchangia kwa namna inayofaa, hususan wakati wa majadiliano,”
alisema Mhe. Nongwa.
Katika
mafunzo hayo, Afisa Uangalizi Mkuu na mmoja wa Wawezeshaji, Bw. Samweli Kabunga
alitoa mada kuhusu utaratibu wa kisheria unaoongoza utoaji na utekelezaji wa amri
ya huduma kwa jamii katika mfumo wa utoaji haki, hususan kwa makosa ambayo
sheria inaruhusu mhusika kupewa adhabu mbadala badala ya kifungo gerezani.
Alifafanua
kuwa, amri ya huduma kwa jamii inayotolewa kama adhabu mbadala kwa kuongozwa na
Sheria ya Huduma kwa Jamii, sura ya 291, pamoja na Kanuni zake, humwezesha
mkosaji kubaki katika jamii na kutekeleza kazi zenye manufaa kwa jamii kama
njia ya kutumikia adhabu aliyopewa na Mahakama kwa kipindi kilichoamriwa na Mahakama.
Akifafanua
zaidi juu ya mambo muhimu kuhusiana na amri ya huduma kwa jamii, Bw. Kabunga
alieleza kuwa, amri hiyo inaweza kutolewa moja kwa moja mahakamani kwa
kuzingatia masharti ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Huduma kwa Jamii au kutolewa
na Mahakama kwa mchakato kuanzia gerezani baada ya mkosaji kuhukumiwa kifungo
gerezani kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 52 cha Sheria ya Magereza, sura
ya 58.
Sambamba
na hayo, Bw. Kabunga alisema kuwa kabla ya kutolewa kwa amri ya huduma kwa
jamii yapo mambo kadhaa ambayo Mahakama inapaswa kujiridhisha nayo ikiwa ni
pamoja na: ukomo wa adhabu iliyowekwa kisheria (kifungo kisichozidi miaka
minne); uwepo wa mkosaji mahakamani; ridhaa ya mkosaji; uwepo wa mikakati ya
kutosha ya utekelezaji wa amri; uwepo wa ripoti ya Ofisa Huduma kwa Jamii
inayoonesha kuwa mkosaji anaweza kutoa huduma kwa jamii; na kadhalika.
Matumizi
sahihi ya amri ya huduma kwa jamii, kwa maneno ya Bw. Kabunga, yanaweza
kusaidia kupunguza msongamano magerezani, kumuwezesha mkosaji kurekebisha tabia
na kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii huku akiwajibika kwa kosa
alilolitenda.
Naye
Afisa Uangalizi Mwandamizi, Bw. Deogratius Shirima aliwasilisha mada kuhusu
masharti ya kisheria yanayohusu utoaji na utekelezaji wa amri za uangalizi na
makundi ya wahalifu wanaoweza kuwekwa chini ya uangalizi huo. Alieleza kuwa,
tathmini ya mkosaji haipaswi kuzingatia kosa alilolitenda pekee, bali pia
mazingira yake binafsi na kijamii, huku mambo yanayoweza kuzingatiwa yakiwa ni
pamoja na umri, tabia, hali ya afya ya akili na mazingira mengine yanayoweza
kuwa na umuhimu katika kutoa uamuzi unaofaa kwa mujibu wa sheria.
Bw.
Shirima alielezea amri ya uangalizi kwa kufafanua kuwa, mhalifu anayepewa
adhabu hiyo anaachwa kwenye jamii na kuwekwa chini ya uangalizi na usimamizi wa
Ofisa Uangalizi kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka
mitatu kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uangalizi wa
wakosaji (sura ya 247) pamoja na kanuni zake.
Kwa
sababu hiyo, Bw. Shirima alifafanua kuwa, ni muhimu kwa Ofisa Uangalizi kuchunguza
mazingira ya mkosaji kabla ya kutoa mapendekezo kwa Mahakama kuhusu adhabu
inayofaa na kwa upande wa Mahakama ni muhimu kuchunguza mapendekezo ya Ofisa Uchunguzi
kabla ya kuamua kutoa amri ya uangalizi kwa mkosaji.
Kwa
upande wake, Afisa Uangalizi Mkuu, Bi. Sheroline Mzava aliwasilisha mada kuhusu
Taarifa ya Uchunguzi wa Kijamii (TUK) na kuelezea umuhimu wake katika kuisaidia
Mahakama kufanya uamuzi sahihi unaozingatia mazingira ya mkosaji na shauri
linalosikilizwa wakati wa kutoa adhabu kwa mkosaji.
Alisema kuwa, taarifa hiyo hujumuisha
uchunguzi wa historia ya mkosaji, mwenendo wake wa maisha, mazingira ya
kifamilia na kijamii, pamoja na mambo mengine yanayoweza kusaidia Mahakama
kutathmini adhabu inayofaa.
Bi.
Sheroline aliongeza kuwa, taarifa ya uchunguzi wa kijamii humuwezesha Ofisa Uangalizi
kutoa tathmini na mapendekezo yanayoweza kuisaidia Mahakama kufanya uamuzi
unaozingatia sheria, mazingira ya shauri husika na uwezekano wa mkosaji
kurekebisha mwenendo wake ili asirudie tena kosa.
Kwa
upande mwingine, Washiriki wa mafunzo hayo walipata fursa ya kujadili
changamoto zinazoweza kujitokeza katika utoaji na utekelezaji wa amri za uangalizi
na huduma kwa jamii, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuimarisha
ushirikiano kati ya Mahakama na wadau wengine wa mfumo wa haki jinai.
Mafunzo
hayo yanatarajiwa kuimarisha uelewa wa pamoja miongoni mwa washiriki kuhusu
matumizi sahihi ya adhabu mbadala, kwa kuzingatia sheria, mazingira ya kila
shauri na maslahi mapana ya jamii, ili kuchangia utoaji haki wenye ufanisi.
Ofisa Uangalizi Mwandamizi, Bw. Deogratius Shirima akiwasilisha mada kuhusu masharti ya kisheria yanayohusu Utoaji na Utekelezaji wa Amri za Uangalizi wakati wa Mafunzo kuhusu utoaji na utekelezaji wa adhabu mbadala yaliyofanyika hivi karibuni Mahakama Kuu Njombe. Wengine walioketi ni Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Maofisa wa Jeshi la Magereza na Wadau wengine wa mfumo wa Haki Jinai.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (aliyeketi katikati) pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (kushoto) na Ofisa Uangalizi Mkuu, Bi. Sheroline Mzava wakimsikiliza kwa makini Mratibu wa Mafunzo kuhusu Utoaji na Utekelezaji wa Adhabu Mbadala ambaye ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola (hayupo katika picha).
Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola akiendelea na uratibu wa mafunzo hayo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo
ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Utoaji na Utekelezaji wa Adhabu Mbadala. Wanaoonekana pembeni ni sehemu ya Wataalam kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Kitengo
cha Huduma za Uangalizi na Huduma kwa Jamii kutoka jijini Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.
Victoria Nongwa akifungua mafunzo ya Utoaji na Utekelezaji wa Adhabu Mbadala.
Ofisa Uangalizi Mkuu, Bw. Samwel Kabunga akitoa mada kuhusu
Utaratibu wa kisheria wa Adhabu mbadala (Huduma kwa Jamii) wakati wa mafunzo hayo.
Ofisa Uangalizi Mkuu, Bi. Sheroline Mzava (aliyesimama) akiwasilisha
mada kuhusu Taarifa ya Uchunguzi wa Kijamii (TUK) wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.
Mkuu wa Mashitaka Mkoa (RPO) wa Njombe, Wakili Shaban Mwegole (aliyesimama) akichangia mada.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni