·
Wajenga
mitaro kupitisha maji ya mvua Barabara ya Mahakama Hiltop Kigoma
Na
AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma imechukua hatua madhubuti za
kukabiliana na mvua kubwa za El Niño zinazotajwa kunyesha mapema mwezi huu kwa
kushirikiana bega kwa bega na Wadau mbalimbali katika ujenzi na uimarishaji wa
mitaro ya barabara kuanzia eneo la Mahakama Kuu hadi Hiltop mkoani humo.
Mtendaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka, hivi
karibuni alifanya ukaguzi wa uchimbaji, ujenzi na uzibuaji wa mitaro ya maji
iliyopo katika barabara ya Mahakama kwenda hoteli ya kitalii ya Hilltop.
Hatua
hiyo haioneshi tu umuhimu wa usalama wa miundombinu ya majengo ya Mahakama na
barabara zinazowahudumia wananchi, bali pia inaakisi nguvu ya ushirikiano wa
dhati baina ya Mahakama na jamii inayoizunguka.
“Leo,
kazi ya ukarabati na usafishaji wa mitaro ya kupitisha maji ya mvua katika
barabara inayotoka eneo la Mahakama hadi Hilltop Kigoma inaendelea kwa kasi.
Hatua hii inalenga kuhakikisha maji ya mvua yanapita kwa urahisi bila
kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu ya barabara, au hatari kwa
watumiaji wa njia hiyo na wananchi wa maeneo ya jirani,” alisema Bw. Kasuka.
Aliongeza kwa kusema kuwa, "ushirikiano
wetu na Wadau mbalimbali hapa Kigoma unadhihirisha kuwa usalama wa miundombinu
na mazingira yetu ni jukumu la pamoja, hasa kipindi hiki cha kujiandaa na msimu
wa mvua kubwa."
Aliendelea
kusema kuwa, Mahakama inatambua na kupongeza mchango mkubwa wa wadau wote
waliojitokeza kushirikiana katika zoezi hili muhimu na kwamba jitihada hizo inalenga
kulinda mali, kupunguza athari za vyanzo vya maji vilivyoziba na kuweka
mazingira safi na salama yatakayowezesha huduma za kimahakama na shughuli za
wananchi kuendelea bila kikwazo.
Kwa
upande wake, Mhandisi Dan suka kutoka Kampuni ya Hilltop, alisema kwa niaba ya Kampuni
hiyo kuwa, “tunawashukuru kila mdau aliyeshiriki kwa namna moja au nyingine
kufanikisha kazi hii ya haraka na yenye tija kubwa kabla ya mvua hizo kuanza
kunyesha.”
Vile
vile alimuhakikishia Mtendaji wa Mahakama Kuu Kigoma, kuwa ujenzi huo
utakamilika mapema kabla ya muda waliojiwekea ili kuzikabili mvua
zinazotarajiwa kunyesha mapema hivi karibuni.
Wadau waliojitokeza kujenga mitaro hiyo kwa kushirikiana na Mahakama Kuu Kigoma ni pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)-Kigoma, Magereza pamoja na Hoteli ya Hilltop ambapo kwa pamoja walihakikisha mitaro hiyo inayopitisha maji mengi kuelekea ziwani inakarabatiwa na kuwa imara katika kukabiliana maji mengi.
Mhandisi Ujenzi wa Kampuni wa Hilltop Kigoma, Dan Suka (kushoto) akitoa maelezo ya maendeleo ya
ujenzi wa mitaro ya barabara ya Mahakama kwenda Hilltop, kwa Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya
Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka. Ujenzi wa mitaro hiyo ni jitihada za kubabiliana Mvua
za El Nino.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akiwaelekeza jambo Mafundi wa Ujenzi mitaro ya barabara ya Mahakama kwenda Hilltop unaoendelea.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akitembea katika mtaro mpya unaoendelea kujengwa kwa ushirikiano na wadau wanaotumia barabara hiyo ya Mahakama kwenda Hilltop Kigoma.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akitazama mtambo unaofanya kazi ya kutengeneza mitaro ya barabara ya Mahakama kwenda Hilltop Kigoma.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akiendelea kukagua na kuona ubora wa ujenzi wa mitaro hiyo inayojengwa ili kukabiliana na Mvua za El Nino.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akitazama uchanganyaji wa saruji na mchanga kwa ajili ya ubora wa ukuta wa kingo za mtaro unajengwa kwa ajili ya kukabiliana na mvua za El Nino.
Mhandisi Ujenzi wa Kampuni wa Hilltop Kigoma, Mhandisi Dan suka akiendesha Mtambo alipokuwa akichonga barabara na mitaro kwa ajili ya kukabiliana na Mvua za El Nino.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni