Na EVA LESHANGE & AMIRI BAKARI, Mahakama – Singida
Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, imeendelea na utekelezaji wa zoezi la
usafi wa mazingira katika maeneo yake kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ikiwa
ni sehemu ya juhudi za Mahakama katika kuimarisha usafi, afya, usalama na
ustawi wa mazingira ya kazi.
Zoezi
hilo linawashirikisha Majaji, Mahakimu pamoja na Watumishi wa kada mbalimbali
ambao kwa pamoja hushiriki katika kufanya usafi wa maeneo ya ofisi, na maeneo
mengine yanayozunguka majengo ya Mahakama.
Lengo
kuu la zoezi hilo ni kuhakikisha kuwa, mazingira ya Mahakama yanakuwa safi,
salama, yenye kuvutia na rafiki kwa watumishi, wadau wa Mahakama pamoja na
wananchi wanaofika katika maeneo hayo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za
kimahakama.
Mbali
na kuimarisha usafi wa mazingira, zoezi hilo pia ni sehemu ya kujenga na
kudumisha utamaduni wa uwajibikaji, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa
watumishi. Ushiriki wa pamoja katika shughuli za usafi unaonesha dhamira ya
Mahakama ya kuhakikisha kuwa kila mtumishi anatambua wajibu wake katika kutunza
na kuboresha mazingira ya kazi.
Katika
kuendeleza juhudi za kuboresha mazingira ya kazi, Mahakama Kuu Singida,
ilitumia siku hiyo pia kuendelea na shughuli za uboreshaji wa mazingira katika
eneo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida, ambapo maua yalipandwa
katika maeneo yanayozunguka jengo la Kituo hicho.
Hatua
hiyo inalenga kuimarisha utunzaji wa mazingira, pamoja na kuboresha mandhari na
muonekano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki. Upandaji wa maua
unatarajiwa kuongeza uzuri wa mazingira ya Kituo hicho na kuyafanya kuwa safi,
ya kuvutia na rafiki kwa watumishi, wadau wa Mahakama na wananchi wanaofika
kupata huduma.
Aidha,
Mahakama hiyo inaamini kuwa mazingira bora ya kazi yana mchango mkubwa katika
kuongeza ufanisi, ari na morali ya watumishi. Mazingira safi na salama huweka
mazingira bora ya utendaji kazi na hivyo kuchangia katika utoaji wa huduma bora
kwa wananchi kwa wakati na kwa weledi.
Kwa msingi huo, watumishi wameendelea kuhamasishwa kutunza usafi wa mazingira si wakati wa zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi pekee, bali kufanya usafi kuwa sehemu ya utamaduni na wajibu wa kila siku katika maeneo yao ya kazi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (mstari wa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi pamoja na watumishi wa Mahakama hiyo mara baada ya kukamilisha zoezi la usafi wa mazingira. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Singida, Mhe. Nenelwa Joyce Mwihambi na kulia kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Singida, Mhe. Jasmin Abdul.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akishiriki zoezi la upandaji maua katika eneo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Mahakama hiyo katika utunzaji wa mazingira na uboreshaji wa mandhari ya eneo la Kituo hicho.

Jaji Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Nenelwa Joyce Mwihambi akishiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji maua kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida.

Watumishi
wa Mahakama Kuu Singida wakishiriki zoezi la usafi na
upandaji maua katika eneo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida,
ikiwa ni sehemu ya juhudi za Kanda katika utunzaji wa mazingira, kuimarisha
afya na kuboresha mandhari ya eneo la Kituo.

Mtunza Kumbukumbu kutoka Mahakama ya Wilaya Manyoni, Bw. Salum Ramadhani Mussa akishiriki kikamilifu katika zoezi la kusafisha na kuweka mazingira safi katika Mahakama ya wilaya Manyoni.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Mhe. Fadhili Luvinga (kushoto), akishirikiana na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe. Said Siri (kulia) wakati wa zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Utemini.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ipembe, Mhe. Deodatus Patrick, akishiriki kikamilifu katika zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la Mahakama ya mwanzo Ipembe.

Mtunza
Kumbukumbu wa Mahakama ya Mwanzo Ikungi, Bi. Magreth Mtilimbania (mbele) akiwa
pamoja na Mlinzi wa Kituo hicho, Bw. Emmanuel Vicent (nyuma) kwa pamoja wakishiriki zoezi la
usafi wa mazingira katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Ikungi.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni