Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amepongeza juhudi
zinazoendelea kuchukuliwa na Wataalam wa Mahakama ya Tanzania katika kuboresha
mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye usikilizaji wa
mashauri nchini.
Mhe. Dkt. Siyani ametoa
pongezi hizo leo tarehe 8 Oktoba, 2026, kwa Kurugenzi ya TEHAMA na ile ya
Usimamizi wa Mashauri, baada ya kupokea wasilisho la maboresho yaliyofanyika
kwenye mifumo miwili ambayo inaenda kuboresha usajili na usikilizaji wa
mashauri katika Mahakama za Mwanzo.
“Nawapongeza sana kwa
kuendelea kuifanya Mahakama yaTanzania kuwa kinara kwenye matumizi ya TEHAMA
katika shughuli za utoaji huduma za kimahakama. Taasisi nyingi za Serikali
zinaiga kutoka mahakamani,” amesema.
Jaji Kiongozi ameeleza
kuwa kuna mambo makubwa ambayo hayazungumzwi yaliyofanywa na Mahakama ya
Tanzania kwenye eneo hilo, ambayo yanaonekana siyo ya kawaida kwenye mamlaka
nyingine nje ya nchi.
Amesisisitiza kuwa
maboresho hayo yanayofanyika ni safari inayoendelea na wapo kwenye mwelekeo
mzuri. Amesema kuwa hayo ni mapinduzi makubwa, ukilinganisha na nchi nyingine.
“Tunayo mambo
tunayoyafanya makubwa sana ambayo sisi tukiyatazama tunayaona ya kawaida. Mtu
atajua tofauti kama akitoka nje ya nchi na kutazama wengine wanavyofanya. Sisi
tumepiga hatua kubwa sana. Huwezi kuona thamani ya hiki tunachofanya mpaka
uwaone wengine wanavyo hangaika,” Mhe. Dkt. Siyani amesema.
Jaji Kiongozi amewahimiza
Watalaam hao kubaini changamoto ambazo zinaweza kujitokeza na kuzifanyia kazi
haraka na pia kuwaandaa watumiaji kabla ya mifumo hiyo kuanza kutumika.
Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, naye amewapongeza wataalam hao, kwani mifumo hiyo inaendelea kuimarika zaidi ukilinganisha na jinsi alivyouona hapo mwanzo.
Akasisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya maboresho zaidi kwenye maeneo yatakayobainika kuwa na changamoto kwa watumiaji ili uweze kuleta manufaa yanayokusudiwa.
Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw.
Kalege Enock, pamoja na timu yake wamewasilisha maboresho ambayo yamefanyika
kwenye Mfumo wa kusajili mashauri katika Mahakama za Mwanzo, ambao uaitwa
Primary Court App.
Ameeleza kuwa Mfumo huo
ni “mobile application” ambayo mashauri yanaingizwa kwenye mfumo kwa kutumia
simu au kompyuta.
Maboresho mengine
yaliyowasilishwa yanahusu Mfumo unaoratibu majalada ya mashauri yaliyomalizika,
ambao unaitwa “Primary Court File Management System.” Kazi ya Mfumo huu ni
kuchukua kumbukumbu zilizoingizwa kwenye Primary App.
Mifumo hii
itawarahisishia wadau watakaokuwa wanataka kukata rufaa kutoka Mahakama ya
Mwanzo, kwani hawatahitajika kuchukua nakala ngumu ya jalada. Pia uwekaji namba
wa shauri pamoja na makusanyo ya maduhuli yatafanywa na mfumo wenyewe.
Viongozi wengine waliohudhuria uwasilishaji wa mifumo hiyo ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu (Masjala), Bw. Leonard Magacha, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, Mhe. Sundi Fimbo na Naibu Wasajili wengine.










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni