Alhamisi, 8 Oktoba 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA WAHIMIZWA KUZINGATIA MAADILI, HUDUMA BORA KWA WATEJA

Na. PAUL MAKANINE na HABIBA MBARUKU- Mahakama, Dodoma

Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, amewataka Waandishi Waendesha Ofisi na Watunza Kumbukumbu wa Mahakama kuzingatia maadili ya utumishi, usiri wa taarifa na matumizi sahihi ya taarifa za Serikali ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora na zenye ufanisi.

Bi. Patricia ametoa wito huo leo tarehe 8 Oktoba, 2026 katika ukumbi wa Mkutano uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya huduma kwa mteja kwa watumishi hao yanayolenga kuwajengea uwezo katika kuboresha utoaji wa huduma kwenye maeneo yao ya kazi.

Aidha, amewakaribisha watumishi hao kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kuboresha namna wanavyowahudumia wananchi na wadau wengine wanaofika katika Mahakama kupata huduma.

Bi. Patricia, ameeleza kuwa huduma kwa mteja ni “Chen”; ambayo inahitaji mtumishi kuwa na uelewa mzuri wa majukumu yake, kuwa na mawasiliano mazuri na wateja pamoja na kuzingatia misingi ya maadili ya utumishi wa umma.

“Ni muhimu kila mtumishi kuelewa nafasi yake katika utoaji wa huduma na kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia weledi, heshima na maadili,” amesema Bi. Patricia.

Vilevile, Bi. Patricia amewakumbusha watumishi hao kuongeza uwezo na uelewa kuhusu maadili ya watumishi wa Mahakama na utumishi wa umma kwa ujumla, kwa kuzingatia maadili katika kila hatua ya utoaji wa huduma, ikiwemo namna ya kuwapokea, kuwahudumia wateja, kutunza kumbukumbu na kushughulikia taarifa zinazowahusu wananchi na Serikali. Amesisitiza kuwa maadili ni msingi muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa Taasisi za umma.

Aidha, Bi. Patricia amesisitiza kuhusu umuhimu wa kutunza siri za ofisi  ndani na nje ya kazi , huku akiwataka watumishi hao kutambua kuwa taarifa wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao zinapaswa kulindwa na kutotolewa kwa watu wasiohusika.

“Utunzaji wa siri ni jambo la msingi katika utendaji kazi wetu. Kila mtumishi anatakiwa kuwa makini na taarifa anazopokea au kuzitunza katika utekelezaji wa majukumu yake,” amesisitiza.

Kadhalika, amewakumbusha watumishi hao kutumia taarifa za Serikali kwa usahihi na kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa, akieleza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya taarifa yanaweza kuathiri uaminifu, usalama na ufanisi wa utoaji wa huduma.

Amesema kuwa kila mtumishi ana wajibu wa kuhakikisha taarifa za Serikali anazoshughulikia zinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na zinatunzwa kwa namna inayolinda maslahi ya Taasisi na wananchi.

Akitoa wasilisho lake katika mafunzo hayo, Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Dkt. Evetha Mboya, amewajengea washiriki uelewa kuhusu dhana ya huduma kwa mteja, kumtambua mteja wa Mahakama, matarajio ya wateja wa Mahakama pamoja na namna bora ya kuwahudumia wateja wa ndani na nje ya Mahakama.

Dkt. Evetha amefafanua kuwa utoaji wa huduma bora, ikiwemo mawasiliano na wateja, mwenendo na mtazamo wa mtumishi katika kumhudumia mteja, pamoja na umuhimu wa kuzingatia weledi na maadili katika kuhakikisha wateja wanapata huduma inayokidhi matarajio yao ni jambo muhimu linalokuza taswira ya Taasisi, kwani wateja hueneza taarifa kulingana na walivyohududmiwa.

Aidha, ameeleza vipengele muhimu vinavyopima ubora wa huduma kwa mteja, ambavyo ni Tangibles (mwonekano na mazingira ya huduma), Reliability (uwezo wa kutoa huduma kwa usahihi na kwa kuaminika), Responsiveness (utayari na kasi ya kumhudumia mteja), Assurance (uwezo wa kumjengea mteja imani na kujiamini katika huduma anayopewa) na Empathy (uwezo wa kumwelewa na kumjali mteja).

Pia, ameeleza kuhusu namna bora ya kuwahudumia wateja wa ndani na nje ya Mahakama, ikiwemo namna ya kukabiliana na wateja wenye changamoto (difficult customers) kwa weledi, utulivu na heshima, bila kuathiri ubora wa huduma inayotolewa.

Mafunzo hayo yaliyoanza leo kwa awamu kwa kada za Waandishi Waendesha Ofisi na Watunza Kumbukumbu yanatarajiwa kuendelea hadi tarehe 8 Novemba, 2026, yakihusisha kada zilizobaki ambazo ni Wasaidizi wa Ofisi, Walinzi Maafisa TEHAMA na Wahandisi, huku yakitarajiwa kuwawezesha watumishi hao kuongeza uelewa kuhusu huduma kwa mteja, maadili ya utumishi.


Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, akitoa mafunzo kwa Waandishi Waendesha Ofisi na Watunza Kumbukumbu leo tarehe 08 Oktoba 2026, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.



Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Dkt. Evetha Mbuya akitoa mafunzo kwa Waandishi Waendesha Ofisi na Watunza Kumbukumbu leo tarehe 08 Oktoba 2026, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Sehemu ya Waandishi Waendesha Ofisi na Watunza Kumbukumbu waliohudhuria Mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Maadili, yaliofanyika leo tarehe 08 Ocktoba 2026, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.



Sekretarieti ya Mafunzo kwa Waandishi Waendesha Ofisi na Watunza Kumbukumbu waliodhuruia Mafunzo hayo leo tarehe 08 Oktoba 2026, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Picha na Halima Mnete-Mahakama, Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni