Na EVA LESHANGE & AMIRI BAKARI, Mahakama – Singida
Katika kuunga mkono juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani
na kuongeza ufanisi wa kazi, Chama cha Mahakimu na Majaji (TMJA) Tawi la
Singida kimefanya ziara ya kipekee ya kiutalii katika Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro na Makumbusho ya Kimataifa, mara baada ya kukamilisha Mkutano wao wa
Robo Mwaka.
Ziara hiyo ya
siku nne, iliyoanza ilifanyika hivi karibuni wilayani
Karatu Mkoani wa Arusha. Ziara hiyo iliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akiwa pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Singida, Mhe. Nenelwa Joyce Mwihambi, wakiongozana na Mahakimu mbalimbali
kutoka kanda hiyo.
Jumla ya washiriki 35, wakiwemo Majaji wawili, Naibu
wasajili (DRs) wawili pamoja na Mahakimu 31 walishiriki katika safari hiyo
yenye lengo la kujenga undugu, kuhamasisha utalii wa ndani na kujifunza
masuala mbalimbali ya kihistoria na kiuhifadhi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa TMJA
Singida ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Singida, Mhe. Fadhili Luvinga alieleza kuwa, ziara hiyo katika Makumbusho na katika Bonde la
Ngorongoro (Ngorongoro Crater) imewapa fursa ya kujifunza mambo mengi ya
msingi. Washiriki walipata fursa ya kuelewa kwa kina maisha ya wanyamapori,
historia ya uundaji wa Bonde la Ngorongoro kupitia milipuko ya volkano, pamoja
na mabadiliko ya maisha ya binadamu wa kale hadi leo, ikiwa ni pamoja na
kujionea nyayo za binadamu hao wa kale.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, kama wadau ambao pia
wanashiriki katika utunzaji wa mazingira na utawala bora, ziara hiyo
imewafundisha mbinu bora zinazotumiwa na hifadhi hiyo katika kulinda mazingira
na kuhifadhi wanyamapori kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ziara ya TMJA Singida imeweka kiwango kipya kwa taasisi
za kisheria nchini katika kuchanganya majukumu ya kiutendaji na ustawi wa
watumishi kupitia utalii wa ndani, huku ikitoa hamasa kwa makundi mengine
nchini kutembelea vivutio vya utalii vya Taifa.
Aidha kabla ya kuanza kwa ziara hiyo ya kitalii, Wana TMJA Singida walifanya Kikao cha Robo Mwaka ambapo ilibainishwa kuwa, kikao hicho ni chombo muhimu cha kujitathmini na kuweka mikakati ya kiutendaji kwa Mahakimu wa Tawi la Singida.
Mlezi wa TMJA Singida, Jaji Mfawidhi, Mhe. Mwenda aliwashukuru kwa
ushirikiano uliopo miongoni mwa wanachama, huku akiwataka kuendelea kupambana
na kutokata tamaa katika majukumu yao ya siku hadi siku.
Mlezi huyo, amehimiza viongozi na watendaji wa Mahakama kusimamia uwajibikaji, kufuata maadili bila kuongozwa na huba wala
chuki, na kuongeza kasi ya utoaji haki kwa wananchi.
Pia, aliwakumbusha Mahakimu kama viongozi kuongea na watumishi walio chini yao kwa lugha ya matumaini badala ya kuwa sehemu ya malalamiko, huku akionya dhidi ya kutoa ahadi zisizotekelezeka na kuhimiza kuwasaidia watumishi wenye changamoto mbalimbali ili wawe na amani na utulivu maeneo ya kazi.

Timu ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ziara yao katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro iliyofanyika hivi karibuni. Ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na kuhamasisha utalii wa ndani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (kulia) pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Jaji Nenelwa Joyce Mwihambi (kushoto) wakiwa katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro wakiwaongoza Wanachama wa TMJA Tawi la Singida.

Timu ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida wakiwa wakimsikiliza kwa makini Ofisa Hifadhi
(wa pili kulia) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu uhifadhi na vivutio
vilivyopo Ngorongoro.

Muonekano wa jumla wa Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida wakifuatilia kwa umakini maelezo kutoka kwa Ofisa Hifadhi ya Ngorongoro wakati wa ziara yao.

Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida, wakifuatilia kwa umakini maelezo kuhusu miundombinu na
historia ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida, wakiwa katika picha ya kumbukumbu mbele ya bango la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wakati wa ziara yao.

Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida, wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya bango la Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro wakati wa ziara yao ya kitalii na mafunzo.

Timu ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida, wakiwa katika picha ya pamoja wakiwa na furaha
tele kwenye eneo ambalo lina muonekano mzuri wa Bonde la Ngorongoro (Crater View Point) wakati
wa ziara yao.

Pundamilia mama akimlinda mwanaye akiwa
amepumzika, wanyama hawa ni miongoni mwa matukio ya kuvutia ya wanyamapori
yaliyoshuhudiwa na Wanachama wa TMJA Singida wakati wa ziara yao
Ngorongoro.

Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji (TMJA) Tawi la Singida, wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Lango Kuu la Loduare (Loduare Gate) mara baada ya kuwasili katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida, wakiwa ndani ya gari la kitalii wakishuhudia na kufurahia urembo wa asili wakati wa ziara yao katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Tembo alipoonekana akitembea kwa amani katika
mazingira yake ya asili ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, ikiwa ni
miongoni mwa vivutio vilivyoshuhudiwa na Wanachama wa TMJA Tawi la Singida
wakati wa ziara yao.

Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida, wakiwa ndani ya gari la kitalii huku wakishuhudia
na kufurahia urembo wa asili wakati wa ziara yao katika Hifadhi ya Taifa ya
Ngorongoro iliyofanyika hivi karibuni.

Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida wakiwa katika picha ya kumbukumbu huku wakiwa wameshika bango la ziara yao ndani ya Makumbusho ya Ngorongoro Lengai Geopark
Museum iliyofanyika hivi karibuni.

Muonekano wa nje wa jengo la Makumbusho ya
Geopark (Ngorongoro-Lengai Geopark Museum), Kituo muhimu cha urithi wa
kijiolojia, historia na utalii kilichotembelewa na Wanachama wa TMJA Tawi la
Singida wakati wa ziara yao iliyofanyika hivi karibuni.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni