Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali amewaelekeza Viongozi katika ngazi mbalimbali za Mahakama katika Kanda hiyo kupanga mipango mizuri ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama yenye kuleta matokeo chanya kwa maslahi mapana ya Mahakama na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Mahimbali aliyasema hayo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti ya Mahakama hiyo tarehe 02 Oktoba, 2026 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara iliyopo Mto wa Mbu wilayani Monduli.
Jaji Mahimbali amesisitiza kuwa; ni muhimu kwa Viongozi wa kila ngazi ya Mahakama kushirikiana kwa karibu na watumishi walio chini yao katika kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakuwa bora, zitolewe mapema ipasavyo na kwa kiwango kinachotakiwa. Viongozi hao wamekumbushwa pia kuzingatia uwazi na uadilifu katika utendaji kazi wao wa kila siku.
“Ni muhimu sana kwa viongozi wa kila Mahakama kuwa na mawasiliano ya karibu kwa lengo la kuboresha huduma za Mahakama na hatimaye kuleta matokeo chanya katika utoaji haki,” alisisitiza Jaji Mfawidhi huyo.
Akiwasilisha
taarifa wakati wa Kikao hicho, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Arusha,
Mhe. Dkt. Clemence Mshomba alisema kuwa, hadi kufikia tarehe 01 Julai, 2026,
Mahakama Kuu Arusha ilikuwa na mashauri 503 yaliyokuwa yakiendelea Mahakamani.
Kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, Mahakama Kuu Arusha ilisajili
mashauri 336, mashauri 341 yalisikilizwa na mashauri 498 yalikuwa yanaendelea
kusikilizwa.
Kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, hadi kufikia tarehe 01 Julai, 2026, mashauri 42 yalikuwa yakiendelea Mahakamani hapo. Kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2026, jumla ya mashauri 62 yalisajiliwa na mashauri 52 yalisikilizwa. Mashauri yaliyosalia kufikia tarehe 28 Septemba, 2026 yalikuwa 52.
Mahakama za Wilaya kwa pamoja zilikuwa na mashauri 349 yaliyokuwa yakiendelea Mahakamani hadi kufikia tarehe 01 Julai, 2026. Kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, 2026, Mahakama za Wilaya zilisajili mashauri 457 na kumaliza mashauri 495. Mashauri yaliyobaki kufikia Septemba mwaka huu yalikuwa 311.
Kwa upande wa Mahakama za Mwanzo Mkoa wa Arusha, hadi kufikia tarehe 01 Julai, 2026, kulikuwa na jumla ya mashauri 209 yaliyokuwa yakiendelea Mahakamani. Kuanzia Julai hadi Septemba, 2026 mashauri yaliyosajiliwa ni 2,411 na mashauri 2,408 yaliamuliwa, idadi ya mashauri yaliyobaki ni 212.
Aidha, Mhe. Mshomba amewapongeza watumishi wa Mahakama Arusha kwa kufanya kazi kwa bidii, huku akiwasisitiza waongeze juhudi na maarifa ili kuongeza idadi ya mashauri yanayoamuliwa ikilinganishwa na idadi ya mashauri yanayosajiliwa kwa lengo la kutoa huduma kwa wakati na kuepukana na mlundikano wa mashauri usio wa lazima.
Naye Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Arusha, Bi. Grace Kapama aliwasilisha taarifa yake ambayo ilionesha kazi mbalimbali zilizofanywa ambazo kwa kiasi kikubwa zimeweka mazingira wezeshi ya usikilizaji mashauri. Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na ukarabati wa Mahakama mbili za Mwanzo ambazo ni Endabash na jengo la zamani la Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuwawezesha watumishi 14 kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi katika vyuo mbalimbali ili kuwajengea uwezo na watumishi wengine kushiriki mafunzo ya MDEA. Pia, malipo ya stahili mbalimbali za watumishi yamefanyika kwa wakati, hususan malipo ya fedha za chakula na maziwa pamoja na kuwapatia watumishi sukari na majani ya chai.
Vikao vya Menejimenti ni fursa muhimu ambayo Mahakama- Arusha imeitumia kujadili kwa pamoja mambo mbalimbali ya kikazi ikiwa ni pamoja kubuni njia bora za kufanikisha malengo ya Mahakama ambapo mafanikio na changamoto za kazi zimekuwa zikijadiliwa na kupata ufumbuzi wa pamoja.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe mbalimbali waliowakilisha ngazi mbalimbali za Mahakama katika Mkoa wa Arusha ikiwemo Mahakama Kuu Arusha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mahakama za Wilaya Arusha, Arumeru, Longido, Monduli, Karatu na Ngorongoro.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akiongoza Kikao
cha Menejimenti ya Mahakama Arusha kilichofanyika tarehe 02 Oktoba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara uliopo Mto wa Mbu
wilayani Monduli.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Dkt. Kassian Mshomba akiwasilisha Taarifa ya Mashauri wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Kanda ya Arusha kilichofanyika tarehe 02 Oktoba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara uliopo Mto wa Mbu wilayani Monduli.
Kaimu
Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Bi. Grace Kapama akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu katika Kikao cha Menejimenti ya Kanda kilichofanyika tarehe 02 Oktoba 2026
kwenye ukumbi wa mikutano wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara uliopo Mto wa Mbu
wilayani Monduli.
Wajumbe mbalimbali waliohudhuria Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Arusha kilichofanyika tarehe 02 Oktoba, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara uliopo Mto wa Mbu wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.
Jengo la zamani la Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai lililopo Wilayani Arumeru linavyoonekana kabla na baada ya ukarabati.
Jengo
la Mahakama ya Mwanzo Endabash wilayani Karatu linavyoonekana kabla na baada
ya ukarabati.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar)







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni