Na SETH KAZIMOTO - Mahakama Arusha
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha wamefanya ziara ya kitalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara iliyopo Mto wa Mbu wilayani Monduli tarehe 03 Oktoba, 2026.
Ziara hiyo iliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Frank
Mahimbali ambaye aliambatana
na watumishi mbalimbali wa Mahakama kutoka Kanda hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mahimbali alieleza kuwa, ziara za
kitalii kwa watumishi wa Mahakama zina umuhimu mkubwa katika ustawi wa mtumishi
na ufanisi wa utendaji kazi huku akisisitiza kuwa, ziara kama hizo hazipaswi
kuonekana kama anasa, bali ni sehemu muhimu ya kuboresha mazingira ya kazi na
kuongeza tija katika utoaji haki.
“Majukumu ya kila siku ya utoaji haki yanaweza kuwa mazito na kuleta msongo wa mawazo kwa watumishi ambao hukabiliana nayo, baadhi yakiwa mazito na yenye hisia kali. Ziara za kitalii huwapa watumishi fursa ya kupumzika, kuondoa msongo huo na kurudi kazini wakiwa na ari mpya,” alisema Jaji Mahimbali.
Aliongeza kuwa, ziara za kitalii hujenga mshikamano baina ya
watumishi. Watumishi wanaofahamiana vizuri na wenye uhusiano
mzuri wa kikazi huwa na uwezo mkubwa wa kushirikiana katika kutatua changamoto
zinazojitokeza katika utendaji wao wa kila siku, akieleza kuwa, hatua hiyo inachangia kuimarisha
utendaji wa Mahakama kwa ujumla na kuongeza kasi ya utoaji haki.
Amesema, mbali na mshikamano, ziara hizo pia huongeza motisha kwa watumishi.
Mtumishi anayejiona kuwa sehemu ya timu inayomjali na kumthamini huwa na ari
kubwa ya kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu. Motisha hii ni muhimu katika
sekta ya Mahakama, ambapo uadilifu na umakini ni mambo ya msingi katika kila
hatua ya utoaji haki.
Ziara hizi pia huchangia juhudi za Serikali katika kukuza utalii wa ndani. Watumishi wamepata fursa ya kujionea vivutio vya asili kama Hifadhi ya Ngorongoro na kujifunza kuhusu historia, uhifadhi, na utalii endelevu. Hii inawasaidia watumishi kuthamini na kujivunia urithi wa nchi yao, huku wakichangia uchumi wa ndani kupitia matumizi yao.
Utalii wa ndani ni moja ya
nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania, na watumishi wa Mahakama wana nafasi ya
kuchangia katika kukuza sekta hiyo.
Kwa ujumla, ziara ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Arusha katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara imewapa watumishi fursa ya kupumzika na kujifunza, kuimarisha mshikamano, motisha na afya nzuri ya akili kwa watumishi.
Uongozi wa Mahakama Arusha umesisitiza kuwa, ziara hizo za kitalii zitakuwa endelevu kwani zina nafasi kubwa katika kuboresha utendaji kazi wa Mahakama na ustawi
wa watumishi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arumeru, Mhe. Theresia Sedoyeka wakati wa ziara ya kitalii ya Watumishi wa Mahakama Arusha tarehe 03 Oktoba, 2026 katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Picha za makundi ya Watumishi mbalimbali wa Mahakama Arusha
wakiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara walipotembelea Hifadhi hiyo
tarehe 03 0ktoba, 2026 kwa lengo la kutalii.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni