Alhamisi, 22 Oktoba 2026

WABUNGE KAMATI ZA KUDUMU MBILI WAIPONGEZA MAHAKAMA KWA HUDUMA ZA MASUALA YA FAMILIA TEMEKE

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama-Dodoma

Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam, wakieleza kuwa, kimechangia kusogeza huduma karibu na wananchi na kurahisisha upatikanaji wa haki, hususan katika masuala ya mirathi, ndoa na watoto.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 22 Oktoba, 2026 wakati wa Kikao kati ya Mahakama na Kamati hizo za Kudumu za Bunge kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damian Ndumbaro kilichofanyika kwenye ukumbi wa Anne Makinda uliopo katika Jengo la Utawala la Ofisi za Bunge jijini Dodoma.

Aidha, Wabunge hao wametoa maoni na mapendekezo mbalimbali kwa Serikali na Mahakama kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa na kituo hicho na kuimarisha zaidi upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Akiwasilisha taarifa ya kituo hicho, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, amesema kuwa, kituo kilianzishwa kwa lengo la kuboresha huduma za utoaji haki katika mashauri ya mirathi, ndoa na Watoto pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Mirathi na Familia Temeke kilianzishwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 640 la mwaka 2021, la tarehe 27 Agosti 2021, huku jengo la kituo hicho likizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 06 Oktoba, 2021.

Kwa mujibu wa Dkt. Jingu, kituo hicho kina Mahakama nne, ambazo ni Mahakama Kuu, Mahakama ya Watoto ya Dar es Salaam, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo. Mahakama hizo zinahudumia mashauri yanayohusu mirathi, ndoa na watoto kwa mujibu wa mamlaka yake ya kisheria.

Aidha, amesema kwamba, katika kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake, kituo hicho kimeendelea kuimarisha usikilizaji wa mashauri na kuwezesha wananchi kupata huduma za haki mapema ipasavyo.

Ameongeza kuwa, mbali na huduma za kimahakama, kituo hicho kina wadau mbalimbali wanaotoa huduma zinazosaidia kukamilisha mchakato wa utoaji haki. Wadau hao ni pamoja na Maofisa Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia la Polisi, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Watoa Msaada wa Kisheria.

Huduma nyingine zinazotolewa kituoni hapo ni pamoja na usaidizi wa uandaaji wa nyaraka za Mahakama, uwasilishaji wa mashauri kupitia mifumo ya Mahakama, ushauri nasaha, usuluhishi, uchunguzi wa kijamii na uandaaji wa taarifa za kijamii. Ushirikiano huo unachangia kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohusiana na haki katika eneo moja.

Viongozi mabalimbali kutoka Mahakama ya Tanzania wamehudhuria kikao hicho.


Sehemu ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ambao ni wajumbe wa kamati hizo waliohudhuria kikao cha pamoja na Mahakama kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Anne Makinda uliopo katika Jengo la Utawala la Ofisi za Bunge jijini Dodoma. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu akiwasilisha taarifa wakati wa Kikao kati ya Mahakama na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kilichofanyika kwenye ukumbi wa Anne Makinda uliopo Bungeni jijini Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe.Mwanabaraka Mnyukwa akijitambulisha wakati wa kikao hicho.

 Sehemu ya Viongozi waliohudhuria kikao hicho kutoka Mahakama ya Tanzania, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum.

 Sehemu ya Baadhi ya Viongozi kutoka Mahakama ya Tanzania wakifuatilia kwa makini kikao hicho wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.

 Sehemu ya Viongozi waliohudhuria kikao hicho kutoka Mahakama ya Tanzania, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Asina Omari, wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Maryprisca Winfried Mahundi na wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni