Jumamosi, 24 Oktoba 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA PWANI WAFANYA MATENDO YA HURUMA KITUO CHA WATOTO YATIMA BULOMA

Na EUNICE LUGIANA & ZAKIA ALLY, Mahakama-Kibaha

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Emmael Lukumai amewaongoza Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani kufanya ziara ya matendo ya huruma katika Kituo cha Kulea Yatima na Watoto Wenye Uhitaji wanaoishi katika Mazingira Magumu cha Buloma (Buloma Foundation Orphanage Centre) kilichopo Sofu, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza baada ya kukabidhi mahitaji hayo jana tarehe 23 Oktoba, 2026, Mhe. Lukumai alisema lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuwaona, kuwafariji na kuwakabidhi mahitaji mbalimbali watoto wanaolelewa katika kituo hicho, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali na jamii katika kusaidia makundi yenye uhitaji na kuimarisha mahusiano mema kati ya Mahakama na jamii wanayoitumikia.

Kadhalika akizungumza na watoto hao, Mhe. Lukumai amewahimiza kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu ili waweze kufikia ndoto zao na wawe wenye tija kwa Taifa hapo baadaye.

Amesema Mahakama Kibaha itaendelea kuwa karibu na kituo hicho na jamii kwa ujumla katika matendo ya kijamii na kusaidia pale inapowezekana.

Kwa upande wao, watoto wa kituo hicho wametoa shukrani zao za dhati kwa watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha kwa msaada waliowapatia, wakisema msaada huo umekuja wakati muafaka na utawasaidia katika mahitaji yao ya kila siku.

Naye Mratibu wa Kituo cha Buloma cha Kulelea Watoto Yatima (Buloma Foundation Orphanage Centre), Bw. Baraka Peter ambaye ni aliwaeleza Watumishi wa Mahakama Pwani kuwa, kwa sasa kituo  kinahudumia jumla ya watoto 69 wenye umri kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 22. Watoto hao wapo katika ngazi mbalimbali za elimu kuanzia shule ya awali, shule ya msingi, sekondari hadi elimu ya vyuo vikuu. 

Aidha, katika ziara hiyo watumishi walipata fursa ya kutembelea mabweni ya watoto hao ambapo wamebaini kuwa yapo katika hali nzuri ya usafi na utunzaji mzuri huku kila mtoto akiwa na kitanda chake.

Pamoja na hali hiyo nzuri, kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo, uongozi wa kituo umetoa wito kwa wadau, taasisi mbalimbali, makampuni na watu binafsi kujitokeza kutoa msaada ili kuendelea kulea watoto hao katika mazingira bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuwalipia Bima ya Matibabu ambayo inagharimu kiasi cha Shilingi za Kitanzania 50,400/= kwa kila mtoto mmoja kwa mwaka.

Pia Mkurugenzi wa kituo hicho, Bi. Anna Kyando aliwashukuru Watumishi wa Mahakama Pwani kwa msaada walioutoa na kusema kwamba, kutoa ni ibada na ipo katika Dini zote kwamba tuwahurumie wahitaji na kwa kufanya hivyo unakuwa umemgusa Mwenyezi Mungu moja kwa moja.

Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha wakiwa katika picha ya pamoja na Watoto wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Buloma (Buloma Orphanage Foundation Centre) baada ya kupokea mahitaji waliyopeleka tarehe 23 Oktoba, 2026.

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Emmael Lukumai akizungumza na Watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Buloma (Buloma Foundation Orphanage Centre) walipowatembelea kituoni hapo tarehe 23 Oktoba, 2026.

Watumishi wa Mahakama wakipokelewa na Watoto wa Kituo cha Buloma Foundation walipowasili katika kituo hicho kwa ajili ya kutoa misaada.

Mratibu wa Kituo cha Buloma Foundation Orphanage Centre, Bw. Baraka Peter akitoa maelezo kuhusu kituo hicho kwa watumishi wa Mahakama Pwani (hawapo katika picha) walipotembelea Kituo hicho tarehe 23 Oktoba, 2026.

Watoto wa Kituo cha Watoto Yatima cha Buloma (Buloma Foundation Orphanage Centre) wakiwafurahia na kuwakaribisha watumishi wa Mahakama Pwani walipofika kituoni hapo.

Ofisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bi. Stumai Hozza akizungumza neno la kuwatia moyo Watoto wa kituo hicho.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Serengeti)

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni