- Awaasa kuwa Waadilifu, kuheshimu watu, kutumia teknolojia kwa busara...
- Awashauri kutokimbilia mafanikio ya haraka
- Afurahishwa na kupongeza maboresho ya miundombinu ya Shule hiyo kama mmoja wa Wanafunzi waliosoma hapo
Na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya
Sekondari Lake kutumia vema maarifa waliyopata kutoka katika shule hiyo kama mwanzo
wa safari na si kikomo cha ndoto.
Mhe. Masaju ameeleza hayo leo tarehe
02 Novemba, 2026 jijini Mwanza alipokuwa akitoa hotuba yake akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali
ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza shule ambayo
naye alisoma katika safari yake ya kitaaluma.
“Leo nimesimama kama mmoja wa watu
ambao safari yao ilipita katika shule hii. Sitaki mnaponisikia mseme tu kwamba
mwanafunzi wa zamani wa Lake amefika katika nafasi hii. Nataka mjifunze jambo
pana zaidi: safari ya maisha hujengwa kwa hatua, kwa watu wanaotusaidia, kwa maamuzi
tunayofanya na kwa juhudi tunazoweka kila siku. Msifikiri kwamba lazima muanze
mkiwa na kila kitu. Anzeni kwa kutumia vizuri kile mlicho nacho, muda wenu,
nafasi ya kujifunza, ushauri mnaopewa na vipaji mlivyonavyo,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amewataka Wahitimu hao
kuendelea kujifunza, kuwa waadilifu, kutobadili misingi yao kwa faida ya muda
mfupi, kuheshimu watu, kutumia teknolojia kwa busara, kuipenda Tanzania kwa
vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu sheria, kulinda mali za umma na
kutatua matatizo ya jamii.
“Msisubiri mazingira yawe kamili
ndipo mfanye bidii. Jengeni uwezo wenu katika mazingira mliyopo, huku
mkiboresha mazingira hayo kwa manufaa ya wengine,” amesisitiza Jaji Mkuu na
kusema kwamba, angependa siku zijazo, asikie simulizi za wahitimu wa leo:
walioboresha huduma za afya, waliobuni teknolojia, walioanzisha biashara na
ajira, waliotetea haki, waliofundisha vizazi vipya na walioleta mabadiliko
chanya katika jamii zao. Hizo ndizo simulizi zinazojenga heshima ya taasisi.
Ameongeza kuwa, Kidato cha Nne ni hatua muhimu, lakini si mwisho wa elimu wala mwisho wa kujijenga. Ni mlango unaofunguka kuelekea hatua nyingine. Amesema, “baadhi yenu mtaendelea na Kidato cha Tano na Sita; wengine mtachagua mafunzo ya ufundi na stadi; wengine mtajiandaa kwa njia nyingine za kujifunza na kujenga taaluma. Njia zinaweza kutofautiana, lakini wajibu ni mmoja: kuendelea kujifunza na kujitengeneza.”
Aidha, amewakumbusha wahitimu hao kutokimbilia kutafuta mafanikio yanayoonekana kabla hawajajenga msingi wa mafanikio ya kweli kwakuwa Dunia ya sasa inaweza kumfanya kijana aamini kwamba mafanikio ni kuonekana, kuwa maarufu au kupata fedha haraka. Amesema, huo si msingi salama wa maisha kwani mafanikio ya kudumu yanahitaji maarifa, ujuzi, nidhamu, uvumilivu, uaminifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayewaangalia.
Kadhalika,
Jaji Mkuu amewaasa Wahitimu hao wa Kidato cha Nne kumcha Mungu na wawe na
dhamira inayowaongoza kutenda yaliyo mema huku akinukuu Biblia Takatifu, katika
Mithali 4:13, inayohimiza kuishika elimu na Qur’ani Tukufu, katika Suratul
Al-Alaq (96:1–5), inatukumbusha umuhimu wa kusoma na kujifunza ambapo mafundisho
hayo yanatuelekeza kuona elimu kama wajibu na neema inayopaswa kutumiwa kwa
busara. Vilevile, amewataka kuwaheshimu wazazi, walezi na walimu wao na
kusisitiza kuwa heshima si udhaifu; ni alama ya ukomavu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewataka
Wahitimu hao kutosubiri Taifa liwaite viongozi ndipo waanze kuonesha uongozi
hivyo, amewasisitiza kuanza kuongoza maisha yao kwa nidhamu, kwa kuwa
waaminifu, kwa kuwaheshimu wengine na kwa kutimiza wajibu wao kwakuwa Uongozi
huanza kabla ya cheo.
Akiizungumzia Shule ya Sekondari
Lake, Jaji Mkuu amesema anaiheshimu na kusisitiza Lake isiwe shule inayojivunia
tu watu waliopita hapo bale iwe shule inayowaandaa watu ambao Taifa litajivunia
kesho. “Kila mhitimu anayekuwa muadilifu, kila mtaalamu anayefanya kazi kwa
ubora, kila kiongozi anayewajibika na kila kijana anayebuni suluhisho jipya,
anaongeza ukurasa katika historia ya Lake,” amesisitiza.
Kadhalika, Mhe. Masaju amewakumbusha
watu mbalimbali waliomaliza katika shule hiyo na katika shule nyingine nchini kuwa na utaratibu
wa kuzitembelea shule walizosoma. Amesisitiza kwa kusema, “Tunaporejea
mashuleni tulikosoma, tunapata fursa ya kutoa shukrani na kukutana na wale
waliochangia kutujenga.”
Jaji Mkuu amesema, amerudi shuleni
hapo akiwa na dhamira ya kutoa shukrani, kutambua mchango wa shule hiyo na,
muhimu zaidi, kuwaambia wanafunzi wa leo kwamba ndoto zao zinaweza kuwapeleka
mbali zaidi ya mipaka wanayoiona sasa.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu
ameushukuru Uongozi wa Shule hiyo kwa kumualika na kumpa nafasi ya kurejea
katika Shule ya Sekondari Lake mahali pa kumbukumbu, malezi na sehemu ya safari
ya maisha yake na wengine wengi waliopita katika shule hiyo. Ameomba shule hiyo
iendelee kung’aa, si kwa historia yake tu, bali kwa ubora wa watu inaowaandaa
kwa ajili ya Tanzania.
“Nimepokea mwaliko huu kwa heshima
kubwa. Lakini niseme wazi: kwangu mimi, leo si siku ya kutembelea shule
nyingine tu; ni siku ya kurejea mahali ambapo sehemu ya safari yangu ya maisha
ilianzia. Kabla ya vyeo vyetu, kabla ya ofisi zetu, kabla ya majukumu yetu
kitaifa na kabla ya heshima tuliyokuwa nayo, tulikuwa wanafunzi. Nasi pamoja na
Madaraka yetu tulikuwa vijana wenye safari mbele yetu, wenye mambo ya
kujifunza, wenye ndoto na wenye wajibu wa kufanya bidii,” amesema Mhe. Masaju.
“Ningependa niwaambie jambo moja mapema: msinitazame leo kwa kuona tu cheo nilichonacho. Nitajeni pia kama mmoja wa wanafunzi waliowahi kukaa madarasani hapa, kusoma, kufundishwa na kuandaliwa kwa maisha. Cheo ni dhamana ya leo; lakini historia ya mtu hujengwa hatua kwa hatua, na mara nyingi hatua hizo huanzia katika madarasa kama haya,” ameeleza.
Kadhalika, Jaji Mkuu amekiri kupokea kwa furaha taarifa ya wazo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Lake (Lake University) ambapo amewapongeza viongozi na wadau wa shule kwa kuwa na ndoto hiyo. Amesema, Taasisi inayothubutu kufikiria hatua inayofuata inaonesha kuwa haitaki kuishi kwa kutegemea historia pekee; inataka kushiriki katika kuandika historia mpya.
“Nimeelezwa pia kuhusu changamoto ya eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya mradi huo. Changamoto hiyo isitumike kuzima ndoto, bali iwe nafasi ya kutathmini upya mpango. Hata hivyo, ndoto ya chuo kikuu inahitaji maandalizi ya kitaalamu na ya muda mrefu: upembuzi yakinifu, mahitaji ya jamii na soko la ajira, maeneo ya kitaaluma yatakayopewa kipaumbele, uwezo wa kifedha, miundombinu, rasilimali watu, usimamizi na utii wa taratibu za mamlaka husika,” amesisitiza.
Ameushari uongozi wa shule hiyo uandae mpango kabambe wa hatua kwa hatua, ukiangalia mahitaji ya sasa na ukuaji wa taasisi kwa miaka mingi ijayo. Eneo la chuo lisitazamwe kwa mahitaji ya leo pekee; litazamwe kwa uwezo wa kupanuka, usafiri, huduma, mazingira na mahitaji ya wanafunzi na wafanyakazi. Ndoto kubwa inahitaji maandalizi makubwa, lakini utekelezaji wake uanze kwa hatua zinazopimika.
Kadhalika, ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kuwekeza katika walimu, maabara, maktaba, teknolojia, michezo, ushauri nasaha na mazingira salama ya kujifunzia na si kuwekeza katika majengo pekee bali wawekeze pia kwa watu, mifumo na maadili yanayofanya majengo hayo yawe na maana.
Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake, Mwalimu Lucas Bunuma amesema jumla ya Wanafunzi 76 wamehitimu kidato cha nne, 30 Wanawake na 46 Wanaume.
Mwalimu
Bunuma amemshukuru Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwa heshima na fadhila kubwa ambayo amefanya
kwa uongozi wa shule hiyo kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa siku hiyo muhimu.
“Tunajua
una majukumu mengi na katika shughuli zako ikiwa ni pamoja na familia, bado
umetupa kipaumbele siku hii ya leo, na umetupa hadhi kubwa ya kitaifa, wewe
ambaye ulikuwa mwanafunzi wa shule hii, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wengine
waliosoma hapa na wamehudhuria mahafali ya leo,” amesema Mkuu wa Shule huyo.
Akizungumzia
kuhusu maendeleo ya Taaluma, Mwalimu Bunuma ameishukuru Bodi ya Wamiliki ya
Shule hiyo kwa kuboresha mazingira mazuri yanayohamasisha wanafunzi kujifunza
na kufundisha. “Tumepata ushindi wa daraja la kwanza, la pili, la tatu pekee
kwa mwaka 2025. Kidato cha nne na cha sita ufaulu wetu ni asilimia 100. Kwa
mfano mwaka 2025, kidato cha nne daraja la kwanza tulikuwa na wanafunzi 44,
daraja la pili wanafunzi 33, daraja la tatu wanafunzi 4. Kidato cha sita daraja
la kwanza walikuwa ni wanafunzi 20, daraja la pili walikuwa ni wanafunzi 36, na
daraja la tatu walikuwa ni wanafunzi 10,” amesema.
Katika Mahafali hayo Kadhalika Jaji Mkuu alipata wasaa wa kutembezwa katika maeneo mbalimbali ya shule hiyo ikiwemo Maabara, Maktaba na sehemu nyingine kadhaa ambapo alijionea maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika shule hiyo. Kadhalika, Mhe. Masaju amekutana na Mwalimu aliyemfundisha Somo la Kemia (Chemistry), Mwalimu Kiran Mody ambapo ameonesha furaha baada ya kukutana na Mwalimu huyo.
Miongoni
mwa Viongozi waliosoma katika shule hiyo ni pamoja na Rais wa Awamu ya Tano wa
Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Mhe. Dkt. Stegomena Tax, aliyekuwa
waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, lakini pia alikuwa katibu mtendaji
wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Angelina
Mabula na wengine kadhaa.
Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Wahitimu, Wanafunzi na Kikundi cha Ngoma za Asili cha Bujora igizo la uendeshaji wa Mahakama ya Mazoezi (Moot Court).
Matukio katika picha ya Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza.






























Hakuna maoni:
Chapisha Maoni