Jumatano, 18 Novemba 2026

MABADILIKO CHANYA KATIKA JAMII HAYALETWI KWA KUPIGANA, BALI KWA KUSHIRIKIANA; JAJI MSTAAFU MUNUO

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mstaafu na Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Eusebia Nicholas Munuo amesisitiza kuwa, juhudi zote za kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, ikiwemo kulinda haki za wanawake na watoto, zinapaswa kuendeshwa kwa pamoja kupitia elimu, mafunzo, na maandishi badala ya migogoro na mabishano.

Akitoa neno la shukrani tarehe 17 Novemba, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kitabu maalum kinachomuenzi kinachoitwa ‘JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer in the Legal Profession in Tanzania,’ kilichoandaliwa chini ya uratibu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Jaji Munuo almaarufu kwa jina la Mama Munuo alieleza kuwa nguvu ya kalamu na maarifa husafiri kila kona na kuleta mageuzi ya kudumu kuliko kutumia nguvu.

Katika hotuba yake iliyojaa hisia na kumbukumbu za safari yake ndefu ya utumishi, Jaji Munuo ameishukuru Mahakama ya Tanzania pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kwa hatua waliochukua ya kuona umuhimu wa kuwa na kitabu hicho.

Kadhalika, Jaji Mstaafu huyo, alikumbushia mchango wa Mwanazuoni na Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Prof. Ruth Meena, ambaye wamefanya naye kazi kwa karibu miongo kadhaa. Alisimulia namna ushirikiano wao ulivyosaidia kufungua milango ya kimataifa, ikiwemo safari yake ya kwanza mwaka 1996 kuhudhuria mkutano wa Chama cha Kimataifa cha Majaji Wanawake (IAWJ) mjini Ottawa, Canada, kwa msaada wa mtandao huo na Ford Foundation.

Aliongeza kuwa, jitihada za pamoja zilizofanywa kupitia asasi za kiraia na mashirika ya kimataifa kama ‘UN Women’ zimesaidia kupiga vita vitendo vya rushwa ya ngono (sextortion), kiasi kwamba leo hii elimu hiyo imefika hadi vijijini na kuongeza uelewa mpana kwa jamii.

Akizungumzia uanzishwaji wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Jaji Munuo alibainisha kuwa mafanikio ya chama hicho hayakujengwa na wanawake pekee, bali yalitokana na ushirikiano thabiti wa Mahakama na Majaji wa kiume (akiwataja viongozi kama aliyekuwa Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Jaji Ignas Kitusi na Mhe. Masati.

Alieleza kuwa, uwepo wa Majaji wa kiume katika mafunzo yaliyotolewa vijijini uliimarisha uaminifu (credibility) kwa jamii, kwani wananchi waligundua kuwa lengo kuu lilikuwa ni maendeleo ya familia nzima na usalama wa watoto, badala ya mgawanyiko wa kijinsia.

Jaji Munuo alihitimisha kwa kutoa rai kwa Majaji, Mahakimu na Wanasheria vijana kwamba, Uongozi wa kimahakama unavuka mipaka ya kusikiliza mashauri mahakamani pekee, bali watumishi wa sheria wanapaswa kujitokeza kama Viongozi na waelezi wazuri katika jamii ili kuhakikisha kuna amani, upendo katika familia na taifa kwa ujumla.

Kitabu hicho kipya kinatazamwa kama hazina kubwa na kifungua macho (eye opener) kitakachonufaisha vizazi vya sasa na vijavyo katika kuimarisha misingi ya utawala wa sheria nchini Tanzania na kimataifa.

Awali akitoa neno la utangulizi wakati wa uzinduzi wa Kitabu hicho kilichozinduliwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo-Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda alisema siku hiyo si ya kuzindua kitabu pekee; bali pia ni siku ya kutambua historia, kuenzi utumishi uliotukuka na kuthamini mchango wa kipekee katika maendeleo ya haki na utawala wa sheria nchini Tanzania wa Jaji Mstaafu, Mhe.  Eusebia Munuo.

“Tukio hili la leo lina umuhimu wa kipekee kwakuwa linaakisi historia ya Jaji Munuo, Mwanamke aliyefungua njia katika taaluma ya sheria Nchini,” alisisitiza Mhe. Dkt. Kisinda.

Aliongeza kuwa, historia ya Jaji Mstaafu, Mhe. Munuo ni fahari ya Mahakama na Nchi kwa ujumla kwakuwa mafanikio yake ni somo la na urithi wa utumishi wake wa umma uliotukuka ni mwongozo wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.


Jaji Mstaafu na Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Eusebia Nicholas Munuo akitoa neno la shukrani wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Jaji Munuo kiitwacho ‘JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer in the Legal Profession in Tanzania, kilichozinduliwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju tarehe 17 Novemba, 2026 kwenye Ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Baadhi ya Majaji, Viongozi, Watumishi wa Mahakama pamoja na Wageni waalikwa walioshiriki katika Hafla ya Uzinduzi wa Kitabu ‘JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer in the Legal Profession in Tanzania, kilichozinduliwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju tarehe 17 Novemba, 2026 kwenye Ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akiwa pamoja na Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo - Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kitabu cha Jaji Mstaafu, Mhe. Eusebia Munuo kiitwacho 
‘JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer in the Legal Profession in Tanzania.' 

(Picha na JAMES BUSANYA & PAUL MAKANILE, Mahakama)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni