Jumatatu, 2 Novemba 2026

MASJALA NDOGO SABA ZA MAHAKAMA KUU ZAKUTANA MANYARA KWENYE BONANZA LA KIHISTORIA

Na CHRISTOPHER MSAGATI - Mahakama, Manyara.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Manyara, imeandaa Bonanza la michezo lililowakutanisha watumishi kutoka Masjala Ndogo saba za Mahakama Kuu pamoja na wadau mbalimbali, katika tukio lililoelezwa kuwa la kwanza kufanyika kwa ukubwa huo katika historia ya Mahakama nchini.

Bonanza hilo lilifanyika tarehe 31 Oktoba 2026, katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, wilayani Babati, na kushirikisha Masjala Ndogo za Manyara, Arusha, Moshi, Dodoma, Singida, Shinyanga na Tabora. Wadau wengine walioshiriki ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mawakili wa Kujitegemea na Kampuni ya Mati Superbrands ya mkoani Manyara.

Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi, alisema lengo la kuandaa tukio hilo ni kuimarisha mahusiano baina ya watumishi wa Mahakama, kuwajengea fursa ya kufahamiana na kukuza afya zao kupitia michezo.

Alieleza kuwa mikusanyiko ya aina hiyo ni muhimu kwa watumishi kwa kuwa inawawezesha kujenga mshikamano na kudumisha afya bora, jambo linaloweza kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mhe. Mbwana Kambangwa, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Martin Shigela, alisema Mahakama ina nafasi muhimu katika jamii, hivyo shughuli za kimichezo ni njia mojawapo ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wake.

Aidha, aliipongeza Mahakama kwa kuandaa bonanza hilo na kueleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika shughuli zinazolenga kuboresha ufanisi na kuimarisha ushirikiano kati ya mihimili hiyo miwili.

Washiriki walishindana katika michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kukimbia na yai kwa kutumia kijiko, mbio za magunia, kucheza muziki, kutambua ladha za soda, pool table na drafti. Washindi walikabidhiwa makombe na medali baada ya kukamilika kwa mashindano.

Katika matokeo ya mashindano hayo, Masjala Ndogo ya Shinyanga ilishinda mchezo wa mpira wa miguu, huku Dodoma ikiibuka mshindi wa mpira wa pete. Masjala Ndogo ya Moshi ilipata ushindi katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume, pamoja na pool table.

Masjala Ndogo ya Manyara, ambayo ilikuwa mwenyeji, ilifanya vizuri katika michezo mbalimbali, ikiwemo kukimbia na yai kwa kutumia kijiko, mbio za magunia, kukimbiza kuku, riadha ya mita 1,500, drafti na bao.

Katika ushindani wa mchezo wa kukimbiza kuku kwa Majaji wa Kike, Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora, aliibuka mshindi. Kwa upande Majaji wa Kiume Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali, aliibuka mshindi mchezo wa kukimbiza kuku na mchezo wa mbio fupi.

Kutokana na kufanya vizuri katika michezo mbalimbali, Masjala Ndogo ya Manyara ilikabidhiwa kombe la mshindi wa jumla baada ya kupata ushindi katika michezo mingi zaidi ikilinganishwa na Masjala nyingine zilizoshiriki.

Akizungumzia mipango ya baadae, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara, ilieleza kuwa ina mpango wa kuandaa bonanza jingine litakalokuwa kubwa zaidi na kushirikisha idadi kubwa ya Masjala za Mahakama pamoja na wadau wengine. Bonanza hilo limeweka msisitizo katika umuhimu wa michezo kama nyenzo ya kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa Mahakama na wadau wake.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe Dkt. Adam Mambi akitoa neno la ufunguzi katika Bonanza la michezo lililokutanisha Masjala Ndogo saba za Mahakama Kuu.

Wachezaji wa mchezo wa mpira wa pete kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara wenye nguo za rangi ya kijani wakichuana vikali na timu ya Mahakama Kuu, masjala Ndogo ya Tabora.

Nahodha wa timu ya kuvuta Kamba kwa upande wa Wanaume kutoka Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Moshi akikabidhiwa Kombe baada ya timu yake kushinda


Wachezaji wa mchezo wa Pool table kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Shinyanga wakichuana vikali na wenzao kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma

Timu za mpira wa miguu ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara na Tabora zikikaguliwa na mgeni rasmi kabla ya kuanza kwa mechi.

Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akimuonesha kwa furaha kuku wake aliyefanikiwa kushinda katika mbio za kukimbiza kuku upande wa Majaji Wanawake.

Timu ya mchezo wa kuvuta Kamba kwa upande wa wanawake kutoka Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Moshi wakichuana vikali na wenzao wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Shinyanga hawapo pichani.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu kutoka Masjala Ndogo Saba wakifanya mazoezi ya viungo katika viwanja vya Tanzanite Kwaraa kabla ya kuanza kwa Michezo kwenye Bonanza.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu kutoka Masjala Ndogo mbalimbali, wakiwa jukwaani wakifuatilia michezo ikiendelea uwanjani.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent kansha & James Busanya - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni