Jumatatu, 2 Novemba 2026

MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMA GEITA YAANGAZA TANZANIA KUTOKEA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO

Na INNOCENT MWANDOJE-Mahakama, Geita

Kutoka katika shughuli za kila siku za utoaji wa haki hadi kilele cha juu zaidi barani Afrika, Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Geita, imeendelea kuonesha kuwa ubunifu hauna mipaka.

Safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro imegeuka kuwa jukwaa la kipekee la kuitangaza Mahakama ya Tanzania na kuufikisha ujumbe wa mafanikio ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma za kimahakama kwa wakati.

Katika zama hizi ambazo teknolojia imekuwa nyenzo muhimu katika kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita imeendelea kujipambanua kwa matumizi ya mifumo ya kidigitali katika uendeshaji na usimamizi wa mashauri pamoja na shughuli za kiutawala. Jitihada hizo zimekuwa sehemu muhimu ya kuimarisha ufanisi wa kazi na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Hata hivyo, kwa Masjala ya Geita kuitangaza dhamira hiyo ya kidigitali haikubaki katika kuta za mahakama wala kwenye mifumo ya kiteknolojia pekee. Safari ya ujumbe huo ilielekezwa hadi Mlima Kilimanjaro, ambapo wazo la kipekee lilizaliwa na kutekelezwa kwa lengo la kuufikisha ujumbe huu katika kilele cha juu zaidi barani Afrika.

Wazo hilo lilianzishwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Kharumwa, Mhe. William Msuya, ambaye akiwa katika likizo yake ya mwaka aliamua kutumia fursa hiyo kufanya utalii wa ndani kwa kupanda Mlima Kilimanjaro.

Mbali na kutimiza azma yake ya kutalii na kujionea uzuri wa rasilimali za nchi, Mhe. Msuya aliona safari hiyo kuwa fursa adhimu ya kuitangaza Mahakama ya Tanzania, hususan Mahakama Kuu Masjla Ndogo Geita, kwa kubeba bango lenye ujumbe maalumu kuhusu mafanikio ya matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za kimahakama.

Kwa mtazamo wake, kufikisha ujumbe huo katika kilele cha Uhuru Peak kungekuwa ishara yenye maana kubwa: kama Mlima Kilimanjaro ulivyo kilele cha Afrika, ndivyo Masjala ya Geita inavyodhamiria kuendelea kupiga hatua katika matumizi ya teknolojia ili kuboresha huduma za kimahakama.

Baada ya kulibuni wazo hilo, Mhe. Msuya alimshirikisha Naibu Msajili wa Mahakama Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, ambaye alipongeza ubunifu huo na kuonesha kuunga mkono dhamira ya kuitangaza Taasisi kupitia ujumbe wa maendeleo ya kidigitali.

Mhe. Lukuna alibariki wazo hilo na kuunga mkono maandalizi ya bango maalumu lililolenga kuitangaza Masjala ya Geita pamoja na mafanikio yake katika matumizi ya teknolojia katika usikilizaji wa mashauri na utekelezaji wa shughuli za kiutawala.

Katika kuhakikisha kuwa ujumbe huo unawakilisha ipasavyo taswira na dhamira ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Msuya alishirikiana kwa karibu na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Ally Mgomba, katika kujadili na kuandaa maudhui ya bango hilo.

Kwa pamoja, walilenga kuandaa ujumbe mfupi wenye maana pana na unaoonesha dhamira ya Masjala ya Geita katika kuimarisha matumizi ya teknolojia, uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utoaji wa haki.

Baada ya kukamilisha maandalizi, ujumbe huo uliwasilishwa kwa Naibu Msajili, Mhe. Lukuna ambaye aliupitisha na kuunga mkono utekelezaji wake.

Akieleza namna maandalizi hayo yalivyofanyika, Mhe. Msuya alisema kuwa ushirikiano huo ulikuwa muhimu katika kuhakikisha kuwa ujumbe uliobebwa unawakilisha vyema mafanikio na mwelekeo wa Kanda ya Geita katika matumizi ya TEHAMA.

Bango hilo lilibeba ujumbe ufuatao: “MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA” “Teknolojia, Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji Madhubuti ndiyo msingi mkuu wa kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.” “GEITA TUNAFANYA TOFAUTI KIDIGITALI.”

Ujumbe huo ulikuwa na lengo la kuonesha kuwa matumizi ya teknolojia yanakwenda sambamba na misingi ya utawala bora, uwajibikaji na dhamira ya Mahakama ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hatimaye, tarehe 20 Oktoba, 2026, safari ya kutekeleza dhamira hiyo ilianza chini ya usimamizi wa kampuni ya utalii ya Popote Africa Adventure Ltd. Safari hiyo ilihusisha kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia maarufu ya Machame, inayotumiwa na watalii wanaotamani kufikia kilele cha mlima huo.

Kwa mujibu wa Mhe. Msuya, safari hiyo ilihusisha siku tano za kupanda mlima, huku akipitia vituo mbalimbali vya mapumziko na malazi kabla ya kuelekea katika kilele cha Uhuru Peak.

Safari hiyo haikuwa tu safari ya kawaida ya utalii. Ilikuwa safari iliyobeba dhamira ya kuitangaza Mahakama Kuu Kanda ya Geita na kuufikisha ujumbe wake katika eneo la kipekee linalotambulika duniani kote.

Kupanda mlima mrefu kama Kilimanjaro kunahitaji maandalizi, uvumilivu, nidhamu na dhamira thabiti. Kwa Mhe. Msuya, kila hatua aliyopiga kuelekea kileleni ilimsogeza karibu zaidi na kutimiza azma yake ya kufikisha ujumbe wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita katika paa la Afrika.

Kwa neema ya Mwenyezi Mungu, pamoja na maandalizi aliyokuwa amefanya, Mhe. Msuya alifanikiwa kufika katika kilele cha Uhuru Peak, sehemu ya juu kabisa ya Mlima Kilimanjaro na barani Afrika. Mafanikio hayo yalithibitishwa kwa kutunukiwa cheti rasmi kinachoonesha kuwa alikamilisha safari ya kupanda mlima huo hadi kileleni.

Kufika kileleni hakukuwa mwisho wa safari yake, bali kulikuwa wakati wa kutimiza lengo kuu lililokuwa nyuma ya safari hiyo.

Akiwa katika kilele cha Uhuru Peak, Mhe. Msuya aliinua na kuonesha bango lililobeba ujumbe wa Mahakama Kuu Geita, akiuweka ujumbe huo katika eneo lenye umuhimu mkubwa wa kijiografia na utambulisho wa Tanzania duniani.

Tukio hilo lilikuwa ishara ya ubunifu, uzalendo na dhamira ya kuitangaza taasisi ya Mahakama kupitia njia zisizo za kawaida. Lilionesha namna watumishi wa umma wanavyoweza kutumia vipaji, mawazo na fursa mbalimbali kuhamasisha maendeleo ya taasisi zao na kuonesha mafanikio yaliyofikiwa katika maeneo yao ya kazi.

Kupitia kaulimbiu ya “Geita Tunafanya Tofauti Kidigitali,” Masjala ya Geita ililenga kuonesha dhamira yake ya kuendelea kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika usikilizaji wa mashauri na usimamizi wa shughuli za kiutawala.

Kama vile Mlima Kilimanjaro unavyoendelea kuitangaza Tanzania duniani kwa kuwa mlima mrefu zaidi barani Afrika, ujumbe wa Mahakama Geita nao ulipata fursa ya kuonekana katika kilele hicho maarufu, ukiwasilisha dhamira ya kuboresha utoaji wa huduma za kimahakama kupitia matumizi ya TEHAMA.

Kwa namna hiyo, safari ya Mhe. Msuya iliunganisha mambo mawili yenye umuhimu kwa Taifa: kuitangaza taasisi ya Mahakama na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Mbali na kuitangaza Mahakama Geita, safari hiyo ilikuwa na lengo jingine muhimu la kuhamasisha utalii wa ndani miongoni mwa watumishi wa umma na Watanzania kwa ujumla.

Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyotambulika kimataifa, vikiwemo Mlima Kilimanjaro, ambao huvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani. Hata hivyo, kuhamasisha Watanzania wengi zaidi kutembelea na kujionea vivutio hivyo ni njia mojawapo ya kuongeza uelewa kuhusu utajiri wa rasilimali za nchi na kukuza utamaduni wa utalii wa ndani.

Kupitia safari yake, Mhe. Msuya alionesha kuwa watumishi wa umma wanaweza kutumia likizo zao kushiriki shughuli za utalii, kujifunza mambo mapya, kujenga afya ya mwili na akili, pamoja na kuitangaza nchi na taasisi wanazozitumikia.

Safari hiyo inatoa hamasa kwa watumishi wengine na Watanzania kwa ujumla kuthamini vivutio vya ndani na kutumia fursa zilizopo kujionea maajabu ya nchi yao.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya safari hiyo, Mhe. Msuya alitoa shukrani kwa Uongozi wa Mahakama Geita kwa kuendelea kujenga mazingira yanayohamasisha ubunifu, uzalendo na jitihada za kuitangaza taasisi ya Mahakama.

Pia alimshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita Mhe. Projestus Kahyoza, ambaye ni mlezi wa Masjala hiyo, kwa uongozi wake makini na imani aliyompa. Alieleza kuwa Jaji Mfawidhi alimpa baraka zake na kumuombea safari njema na salama tangu mwanzo hadi mwisho wa safari hiyo.

Vilevile, alimshukuru Mhe. Ally Mgomba kwa mawazo yake chanya na mchango wake katika kujadili na kuandaa ujumbe uliobebwa hadi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Shukrani hizo zinaonesha umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha mawazo yenye lengo la kuleta matokeo chanya. Wazo lililoanzishwa na mtumishi mmoja liliweza kupata uungwaji mkono wa viongozi na ushirikiano wa watumishi wengine, na hatimaye kutekelezwa katika eneo lililolipa tukio hilo uzito wa kipekee.

Ujumbe wa “Geita Tunafanya Tofauti Kidigitali” ulipofika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, haukuwakilisha tu mafanikio ya safari ya mtu mmoja, bali pia dhamira ya kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika kuboresha ufanisi wa shughuli za kimahakama na kiutawala.

Kwa hakika, kilele cha Mlima Kilimanjaro kimekuwa jukwaa la kipekee la kuufikisha ujumbe wa Mahakama Geita kwa Watanzania na dunia kwa ujumla: Geita inafanya tofauti kidigitali, ikidhamiria kuendelea kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuboresha huduma za kimahakama na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Hakimu Mkazi, Mhe. Kharumwa Msuya, akiwa Machame Gate, eneo la kuanzia kupanda mlima Kilimanjaro.

Mhe. Kharumwa Msuya pamoja na kampuni ya utalii ya Popote Africa Adventure Ltd wakiwa katika kituo cha Machame Camp, mahali ambapo walilala kwa usiku mmoja na kuendelea na safari asubuhi iliyofuata.

Mhe. Kharumwa Msuya pamoja na kampuni ya utalii ya Popote Africa Adventure Ltd wakiwa katika kituo cha Shira Cave Camp.

Lava Tower Camp, kituo hiki si cha kulala bali Mhe. Msuya alikula na kupumnzika tu kisha akaendelea na safari.

Mhe. Kharumwa Msuya alifika Baranco Camp siku ya tatu ya safari, hiki ni kituo cha nne katika kupanda mlima Kilimanjaro.

Karanga Camp, siku ya nne kwenye safari ya kupanda mlima Kilimanjaro Mhe. Msuya alilala katika kituo hiki.

Siku ya tano Mhe. Kharumwa Msuya pamoja na kampuni ya utalii ya Popote Africa Adventure Ltd walilala Barafu Camp, hapa ni kituo cha mwisho cha kulala kabla ya kufika kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro.

Hapa ni Kituo cha Stella Point ambacho unapita kabla ya kufika Uhuru Peak au Kilimanjaro Summit. Hii ni siku sita asubuhi.

Bango lililobeba ujumbe wa “Geita Tunafanya Tofauti Kidigitali” likipepea katika kilele cha Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak).

Mhe. Kharumwa Msuya akipeperusha bango lenye ujumbe kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro.

Mhe. Kharumwa Msuya akiwa Mweka Gate, kituo ambacho vyeti hutolewa kwa wote waliofanikiwa kufika kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro.

 Picha ya Cheti rasmi alichopatiwa Mhe. Msuya baada ya kufanikiwa kufika kilele cha mlima Kilimanjaro.

Makala hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni