Jumatano, 1 Mei 2024

WATUMISHI WA MAHAKAMA YA TANZANIA DODOMA WASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI 2024

Na Arapha Rusheke , Mahakama Kuu Dodoma 

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dodoma na Watumishi wa Makao Makuu ya Mahakama leo tarehe 1 Mei, 2024 wameungana na Watanzania wengine kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi, inayojulikana kama Mei Mosi, inayosherekewa kote duniani.

Maadhimisho hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri katika  Jiji la  Dodoma na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Pilikapilika za maadhimisho hayo zilianza mapema asubuhi ambapo watumishi wa Mahakama waliojitokeza kwa wingi waliungana na wananchi wengine katika eneo la viwanja vya Bunge na baadaye kushiriki kwenye maandamano hadi kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na Bendi ya Jeshi la Magereza yalipita katika barabara ya Bunge kupitia wimpy  baadaye Uwanja wa Jamhuri na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule.

Mbali na watumishi kupita mbele ya mgeni rasmi kwenye maandamano hayo, magari nayo kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yalipita mbele yake na kupamba sherehe hizo.

Baada ya maandamano hayo, ratiba ya maadhimisho hayo iliendelea, ikiwemo viongozi mbalimbali wa Chama cha Wafanyakazi (TUCTA) na Serikali ya Mkoa walipata nafasi ya kutoa salamu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Senyamule amewapongeza wafanyakaizi wote kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu wa 2024 yamebeba kauli mbiu inayosema, “Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya Maisha.


Sehemu ya watumishi wa Mahakama wa  makao makuu na watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma wakiwa katika maandamano ya Meimosi yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

 

Sehemu ya watumishi wa Mahakama wa  makao makuu na watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma wakiingia uwanjani Jamhuri Dodoma na kupita jukwaa kuu  katika maandamano ya Meimosi yaliyofanyika Ki Mkoa katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi bora wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma.


(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam) 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni