Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewaasa viongozi wa Magereza na wadau wote katika sekta ya sheria kutumia mbinu za ubunifu kutatua changamoto zinazoikumba Magereza nchini.
Mhe. Dkt. Siyani aliyasema hayo jana tarehe 25 Machi, 2025 alipofanya ziara ya kikazi katika Magereza mawili yaliyopo katika Manispaa ya Tabora ambayo ni Gereza Kuu Uyui na Gereza la Mahabusu maarufu kama Gereza la Zuberi.
"Nimeona kwenye taarifa yenu kuwa kwa sasa hakuna msongamamo katika magereza haya, ninatambua pia kuna changamoto ya uhaba wa rasilimali, binafsi ninawaasa viongozi wa Magereza na wadau wote katika sekta ya haki kutafuta na kutumia mbinu za ubunifu kutatua changamoto zinazoikumba magereza. Ni muhimu kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashirika ya kijamii, asasi zisizo za kiserikali na taasisi za Serikali ili kutatua changamoto zinazohusiana na haki za wafungwa na ustawi wa magereza," alisema Mhe. Dkt. Siyani.
Jaji Kiongozi alikagua maeneo mbalimbali ya magereza ikiwa ni pamoja na malazi ya wafungwa, sehemu za kuandalia chakula na vifaa vya kisasa vilivyotolewa na Mahakama kwa ajili ya kuboresha huduma za kisheria kwa wafungwa kupitia mfumo wa Mahakama ya Mtandao (Virtual Court) ambao unawezesha kusikiliza mashauri ya wafungwa kwa njia ya mtandao hivyo kupunguza idadi ya wafungwa wanaohitaji kusafirishwa kwenda mahakamani na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Mahakama.
Aidha, Mhe. Dkt. Siyani alikubaliana na juhudi za magereza katika kutumia nishati mbadala kwa ajili ya kuandaa chakula cha wafungwa kwa njia ya kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vya kiasili na pia kutunza mazingira ambapo alikiri kuwa hatua hiyo muhimu inayosaidia kupunguza athari za mazingira.
Ziara hiyo ililenga katika kuangalia hali ya mazingira, miundombinu na huduma zinazotolewa kwa wafungwa katika magereza hayo. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Mahakama ya Tanzania katika kuhakikisha haki za wafungwa zinaheshimiwa na mazingira ya magereza yanaboreshwa ili kuendana na viwango vya kimataifa.
Jaji Kiongozi aliongozana na viongozi wa Mahakama ya Tanzania na Wakuu wa Taasisi mbalimbali ambao ni wadau muhimu katika utendaji wa haki na usalama wa jamii. Viongozi hao ni Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza na vyombo vingine Pamoja na taasisi za haki jinai na madai.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akipokelewa na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora alipofika katika Mahakama hiyo kabla ya kwenda Magereza kwa ukaguzi jana tarehe 25 Machi, 2025.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akisaini kitabu cha wageni kwenye Ofisi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa kwanza kulia). Wengine katika picha ni viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu na wa Kanda hiyo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani wa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mbalimbali alioambatana nao katika gereza Kuu Uyui mkoani Tabora.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)