Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maudhui ya Wiki ya Sheria nchini.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amesema kuwa Mahakama ya Tanzania
itawachukulia hatua za kinidhamu na za kisheria Mahakimu wa Mahakama za
Mwanzo,Wilaya na wale wa Mahakama za Hakimu Mkazi wapato 508 kote nchini
waliotekeleza majukumu yao chini ya kiwango na kushindwa kutimiza wajibu wa
Mahakama wa Utoaji wa Huduma Bora kwa wananchi katika mwaka wa Sheria wa 2015.
Akizungumza
na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam alipokua akitoa ufafanuzi
kuhusu kuanza kwa mwaka mpya wa Sheria wa 2016 na Maadhimisho ya Wiki ya
Sheria ambayo kilele chake kitakua Januari 4,2016 Jaji Mkuu amesema kuwa
kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa Mahakama
na upimaji wa viwango vya utendaji kazi vilivyowekwa, Mahakimu hao wa Mahakama
za wilaya na Hakimu Mkazi 121 na 387 wa Mahakama za Mwanzo watatakiwa
kutoa maelezo ndani ya siku 7 juu ya sababu zilizowafanya washindwe
kutimiza lengo lililowekwa la kushughulikia mashauri 260 kila mmoja.
Amesema
watakaothibitika kamati za nidhamu na maadili za kila wilaya na Mikoa
ambazo ni Kamati ndogo za Tume ya Utumishi wa Mahakama zitawafungulia kesi za
kinidhamu ndani ya siku 21.
“Wale
watakaobainika watakumbwa na adhabu ya kupewa Onyo, kushushwa vyeo na kufukuzwa
kazi ili iwe fundisho kwa wengine, ninajua wapo baadhi ambao waliajiliwa
katikati ya mwaka, wengine kwenda mafunzo ya vitendo vyuoni, wajawazito na
baadhi vituo vyao kuwa na kesi chini ya 260 kwa mwaka” Amesisitiza.
Aidha,
katika hatua hiyo amewapongeza Mahakimu waliofanya vizuri katika utendaji wao
wakiwemo 14 walioshughulikia mashauri zaidi ya 700 kila mmoja, Mahakimu 50
walioamua kesi zaidi ya 500 kila mmoja baadhi wakitokea wilaya ya Mkuranga,
Rufiji na Bukoba mjini na wengine wawili kutoka Dar es salaam walioamua
kesi zaidi ya 900 kila mmoja na kuvuka lengo la utendaji lililowekwa la
kushughulikia mashauri 260 kwa mwaka.
Akitoa
tathmini ya utendaji wa Mahakama kwa mwaka wa sheria uliopita amesema kuwa
Mahakama ya Tanzania ina Mahakama za Hakimu Mkazi kila Mkoa na Mahakama za
Wilaya 111 katika wilaya za Kiserikali 133 pamoja na Mahakama za Mwanzo ambazo
hupokea asilimia 93 ya mashauri yanayofunguliwa kote nchini.
Amesema
mwaka 2015 Mahakama zote nchini zilipokea jumla ya mashauri 206,115, kati ya
hayo mashauri 220,815 yaliamuliwa kukiwa na ziada ya mashauri 14700 jambo
linaloonyesha kuwa Mahakama zinapokea mashauri na kuyashughulikia kwa kasi
inayoridhisha huku mashauri yanayosababisha mrundikano ni yale yaliyo nje ya
idadi iliyopangwa.
Ameongeza
kuwa katika katika kipindi cha mwaka huo wa 2015 Mahakama za Mwanzo zilipokea
mashauri 141,025 ambapo kati ya hayo Mashauri 149,757 yalishughulikiwa huku
idadi ya Mahakimu walioshughulikia mashauri hayo ikiwa 1240.
“Ukiangalia
mwenendo wa ufunguaji wa mashauri yote kote nchini hasa Tanzania Bara utagundua
kuwa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na zile za Hakimu Mkazi zinapokea
mashauri mengi kwa asilimia 93 ,katika kila mashauri 4 yanayofunguliwa nchini 3
yako mahakama za mwanzo ambako wananchi wengi wanatafuta ufumbuzi wa kesi zao
lazima tuweke mkazo” Amesema Jaji Mkuu Mhe.Othman.
Kuhusu
kuanza kwa mwaka mpya wa Sheria mwaka 2016 amesema Mahakama inauanza chini ya
Kauli Mbiu Isemayo “Huduma Bora kwa Wananchi ni Wajibu wa Mahakama na Wadau
wake” ikiwa na kesi 20,431 ikilinganishwa na 34,126 ilizoanza nazo mwaka
2015 na kuongeza kuwa licha ya changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania
mkakati uliopo ni kupunguza idadi hiyo hadi kufikia 0 kwa kila mwanzo wa mwaka
wa sheria.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa Nakala za hukumu amesema Serikali inaendelea
kuijengea uwezo wa kifedha Mahakama wa kuajiri wachapaji wa nakala wengi zaidi
ili Nakala za Hukumu za Kesi ziweze kupatikana pindi tu kesi zinapomalizika
katika mahakama zote nchini tofauti na ilivyo sasa ambapo hupatikana Mahakama
Kuu na Mahakama za Rufani
Aidha,
amesema Mahakama inaendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo majengo na
ujenzi wa mahakama mpya katika maeneo yasiyo na huduma hiyo katika mwaka 2016.
“ Hivi sasa tuna wilaya 23 hazina Majengo ya Mahakama za wilaya, kwenye baadhi
ya maeneo kesi zinasikiliziwa Ofisini kwa Hakimu wakati ilitakiwa ziwe kwenye
jengo lenye ukumbi wa wazi,tumejiandaa kwa michoro ya majengo kwa mahakama zote
ili tuanze kujenga kwa gharama nafuu”
Mhe.
Othman ametoa wito kwa wananchi kutosita kuitumia Mahakama ya Tanzania katika
kupata ushauri wa kisheria kupitia wataalamu wake, kuhudhuria maonesho
mbalimbali ya kisheria yanayofanyika nchini huku akitoa angalizo kwa baadhi ya
watu wanaochangia kuwepo kwa mrundikano wa kesi kwa kufungua kesi za madai au
kupeleka mashauri Mahakamani kama sehemu ya maegesho ya masuala yao.
“Baadhi
ya watu wamekuwa wakipeleka kesi Mahakamani kama sehemu ya maegesho, huzifungua
kisha hushindwa kujitokeza Mahakamani hizi ni tofauti na zile zenye vipengele
vingi ndani ya kesi moja au zile ambazo mashahidi wake wamehama kutoka eneo
moja kwenda lingine, hizi nawahakikishia tutazifuta ili kupunguza mrundikano wa
kesi kwenye Mahakama zetu” Amesisitiza Mhe. Othman.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni