Jumatatu, 9 Mei 2016

HOTUBA YA JAJI MKUU-SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI.



Utangulizi:

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania,

Waheshimiwa mabalozi,

Wawakilishi wa balozi mbalimbali hapa nchini,

Waheshimiwa waziri wa habari,

Viongozi wa dini,

Wawakilishi wa mashirika na taasisi mbalimbali,

Wahisani wa maendeleo,

Wanataaluma mliopo hapa,

Wanahabari na wadau wa habari nchini,

Mabibi na mabwana.

Awali ya yote, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii muhimu.

Pili, napenda kuwapongeza kwa kuadhimisha siku hii muhimu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Sherehe hizi zinaambatana na miaka 25 ya Azimio la Windhoek lililoridhia kuanzishwa kwa siku hii, na pia kuanzishwa kwa Taasisi ya Vyombo vya habari Kusini mwa Afrika (MISA).

Tatu, napenda kutambua kuwa tunaadhimisha miaka 250 ya sheria ya kwanza kabisa ya Haki ya Kupata Taarifa ikijumuisha nchi za Sweden na Finland. Kadhaalika, natambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa kwanza kati ya 15 ijayo ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals (SDGs) ya Umoja wa Mataifa.

Ndugu wanahabari,

Labda nianze kwa kuwachangamsha kwa maswali mawili matatu hivi:

Ni kwa kiasi gani vyombo vya habari huripoti kuhusu utawala bora na maendeleo? Vipi kuhusu haki za bianadamu? Je waandishi na wahariri mnapimaje ubora wa habari mnazoandika? Ni kwa kiasi gani unawaza kwamba unachokiandika kitaleta mabadiliko katika maisha ya mtu atakae soma, kusikiliza ama kuona habari hiyo?

Naomba nigusie angalau maeneo manne kati ya mengi ambayo kama mdau wa habari nadhani ni changamoto kwenye uwasilishaji wenu wa habari katika vyombo mbalimbali mnavyotumia.

Kwanza ni eneo la haki za binadamu:

Kwa siku za karibuni, suala la haki za binadamu limekuwa likipigiwa chapuo na  wadau wa eneo hilo kwa kiasi kikubwa. Serikali na viongozi mbalimbali wamekuwa wakirejea misingi ya kimataifa ya haki za binadamu kwenye matamko yao ya sera na hotuba wanazotoa.

Maamuzi mengi ambayo yamekuwa yakitolewa kwa kiasi kikubwa yanahusisha haki za kimsingi za binadamu; kwa mfano kutoa maoni na kujieleza, haki ya kupata taarifa, afya, maji, chakula, elimu na haki ya kuishi.

Kwa hakika utoaji wa taarifa za aina hii utaendelea kukua na hasa kutokana na kupanuka kwa teknolojia ya mawasiliano duniani, na kwa sababu hiyo waandishi na watangazaji mnategemewa sana kutoa taarifa hizo kwa usahihi.

Vyombo vya habari ni sehemu muhimu sana kwenye mapambano dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Napenda niwaambie kwamba, katika jamii yoyote ya kidemokrasia, vyombo huru vya habari ni silaha muhimu sana katika kuhamasisha utawala bora na maendeleo.

Niwape mfano mmoja; katika kazi moja ya kiuandishi iliyohaririwa na  Profesa Amartya Sen, mchumi na mshindi wa tuzo ya Nobel ya Uchumi mwaka 1998, alifanya ulinganisho wa kuvutia kuhusu nchi za China na India. Nchi mbili hizi zilipata uhuru wake karibu muda sawa ila China ilifanya maendeleo ya haraka kwenye mambo ya kijamii na kiuchumi.

“Lakini katika eneo moja, India inaweza kuipiku China”, hapa nakariri maneno ya Profesa Sen, anasema, “India huru iliweza kushinda vita dhidi ya majanga mbalimbali kama njaa. Na hii iliwezekana kwa sababu ya mfumo wa vyama vingi na uhuru wa vyombo vya habari. Vyombo huru vya habari huonya jamii juu ya majanga mbalimbali yanayoweza kutokea. Na maonyo hayo hufanya jamii kujikinga mapema. Uhaba wa upatikanaji taarifa ni aina nyingine ya umasikini. Bila taarifa sahihi huwezi kufanya maamuzi sahihi,” Mwisho wa kunukuu.

Sisi kama Mahakama, kwa kutambua changamoto za upatikanaji na utoaji taarifa, kote kwa watumishi wa mahakama na waandishi wa habari, tuliamua kufanya mambo yafuatayo na tungefurahi sana kama mihimili mingine ya dola ingefuata nyayo.

Kwanza, kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) tulianzisha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari yakilenga namna bora ya kuripoti habari za mahakama. Waandishi zaidi ya 45 wamenufaika na haya mafunzo na matunda yake tunaanza kuyaona kwa kufuatilia habari mbalimbali za mahakama kwenye vyombo vya habari.

Pili, ili kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanapata taarifa za mahakama kwa wakati na urahisi, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tulianzisha mafunzo yahusuyo upatikanaji na utoaji wa taarifa na huduma bora kwa mteja kwa watumishi wa kada mbalimbali za mahakama. Hadi sasa zaidi ya watumishi 150 wamenufaika na mafunzo hayo.

Mtaona kwa hakika juhudi hizo zinaendana kwa kiasi kikubwa na dhima ya mwaka huu ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari nchini.

Eneo la pili ni kuripoti mchakato wa uchaguzi:

Uzoefu unatuonesha kuwa hata katika demokrasia iliyokomaa, bado tabia ya vyombo vya habari kuonesha mapenzi binafsi na vyama ama wagombea hujitokeza. Na hii hupelekea kuripoti malumbano baina ya vyama fulani ama wafuasi wake na hivyo kusahau kabisa mambo ya msingi yahusuyo maendeleo ya wananchi .

Na tabia ya baadhi ya vyombo vya habari kutumika kutoa matusi, kashfa na maneno ya kejeli ni ya kawaida kwenye jamii ambayo viwango vya weledi vinavyozingatia ukweli, usawa na kuwajibika havijafikiwa. Mambo haya yameonekana hapa kwetu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba baadhi ya dhoruba na manyanyaso waliyopata baadhi ya waandishi wa habari kama tulivyosikia yakawa yamechangiwa kwa kiasi fulani na changamoto hizo.

Lakini pia niwapongeze kwa kazi kubwa iliyofanyika mwaka jana kwa kuripoti habari za uchaguzi, toka wakati wa kuchukua fomu, kuteuwa wagombea na kampeni. Mimi naamini kabisa kuwa kazi hii ilichangia kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari kuwahamasisha watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi ule wa kihistoria.

Eneo la tatu: uhuru wa habari na kujieleza

Kama Mahakama, tunaamini katika haki za msingi za uhuru wa kujieleza, ukihusisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa kama Katiba inavyosema. Lakini hatuamini katika kusema chochote bila kujali unakisema wapi, kwa nani na kwa manufaa gani. Haki yoyote ile ni lazima iambatane na wajibu. Ukifanya makosa, ni lazima utaadhibiwa kulingana na sheria husika.

Sisi tunaamini kuwa uwepo wa sheria nzuri za vyombo vya habari na upatikanaji wa taarifa ni chachu kubwa ya maendeleo katika nchi. Sheria hizo haziwezi kupatikana bila ushirikishwaji wa kina wa wadau husika.

Ni rai yangu kwamba wote mnaohusika kutunga sheria mbalimbali (Serikali, Bunge na Wadau wengine) mtashirikiana kufanya kazi hii, sio kwa maslahi ya mtu fulani, bali kwa manufaa ya nchi.

Eneo la nne ni usawa wa kijinsia:

Usawa wa kijinsia unahusisha shughuli maalum kwa makundi maalum na maamuzi sahihi, na hasa pale ambapo wakinamama ama wakinababa wako katika hali ya kunyanyaswa. Utatuzi wa matatizo yanayohusiana na suala hili unaweza kuwalenga aidha wakinamama wenyewe, wanaume wenyewe, watoto, ama wote kwa pamoja kwa kuwawezesha kushiriki na kunufaika na fursa mbalimbali za kimaendeleo. Hili linawezekana sana kama makundi haya yanapata taarifa sahihi.

Upatikanaji wa taarifa sahihi ndio ufunguo kwa utoaji suluhisho kwa matatizo yanayotukabili. Na kama kuna vyombo vya kutetea eneo hili, kwa hakika vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee kabisa.

Ni imani yangu kuwa jukumu la vyombo vya habari kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda sawa hapa nchini litazidi kuwa kubwa na hasa kutokana ka kukua kwa teknolojia ya upashanaji habari.

Tafiti zinaonesha kuwa usomaji wa magazeti kwa nchi za magharibi unapungua kwa kasi sana kutokana na matumizi ya intaneti, lakini hilo bado halijawa tatizo kubwa hapa nchini. Mimi ninaamini na mnaweza kunikosoa, kwamba aina zote za upashanaji habari kama magazeti, redio, televisheni na intaneti zinapanuka kwa karibu kasi sawa. Matumizi ya mitandao ya kijamii  yameongezeka kwa kiwango cha juu sana. Wasiwasi wangu ni jinsi mitandao hii inavyotumika, hususan kufuata maadili yanayoambatana na matumizi hayo.

HITIMISHO

Nihitimishe kwa kusema kuwa jukumu la msingi kabisa la vyombo vya habari ni kusimamia uwajibikaji na utawala bora na kuwa chachu ya maendeleo kwa nchi yoyote. Lakini ni wazi pia kuwa utekelezaji wa jukumu hili hauwezekani kama hakuna sheria huru na endelevu za vyombo vya habari na upatikanaji taarifa.

Naamini kuwa katika siku mbili tulizokaa hapa na kujadiliana masuala mbalimbali yahusuyo tasnia hii, tumepata fursa ya kukosoana hususan katika suala la kuzingatia maadili ya taaluma, lakini pia kukubaliana mkakati wa namna ya kushirikiana na wadau husika ili kuwa na sheria nzuri na endelevu zitakazochangia kuboresha na kuendeleza tasnia hii.

Naomba nimalize kwa kuwaambia kwamba nimefarijika sana kuwa hapa tangu jana na kuzungumza nanyi mchana wa leo, na ni matumaini yangu kuwa pande zote husika mtatekeleza wajibu wenu kwa nafasi zenu ili tuwe na Tanzania yenye mafanikio.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki wanahabari.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni