Jumanne, 24 Mei 2016

MAHAKAMA YA TANZANIA YAONGEZA KASI YA USIKILIZWAJI WA KESI.


Kwa mujibu wa Kifungu 107 (A) Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa Mahakama. Na kazi kubwa ya Mahakama kama mhimili ni kutafsiri sheria zilizotungwa na Bunge.Tangu mwaka 2012 baada ya kupitishwa kwa Sheria mpya namba 4 ya Mwaka 2011 ya uendeshaji wa Mahakama, imekuwa katika maboresho ya utendaji kazi zake. Maboresho haya yanafanyika ili kuimarisha huduma ya utoaji wa haki nchini.  

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman aliwataka watumishi wote wa mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na kwa malengo ili kuweza kufanikisha malengo waliyojiwekea ya kuimarisha huduma ya utoaji haki nchini. 

Alisema katika kipindi cha maboresho, ni jukumu la kila mtumishi kuwajibika ili kutoa haki kwa wananchi na kwa wakati.”Hatuwezi kufanya kazi kama tulivyozoea, lazima tubadilike, lazima tufanye kazi kwa malengo na kwa uadilifu mkubwa kuhakikisha watu wanapata haki zao na kwa wakati”, alisema Jaji Mkuu. Aliongeza kuwa kwa muda mrefu mahakama imekuwa ikilalamikiwa hasa kwa suala la ucheleweshwaji wa kesi. 

Katika kuboresha utendaji wake wa kazi, mahakama imejipanga kuwa karibu zaidi na wananchi kwa katika kueleza taratibu na huduma zake inazozitoa kwa uwazi kabisa (Transparency) ikiwa ni pamoja na kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi. Maboresho haya pia ni pamoja na mabadiliko ya uongozi wa Mahakama kutokana na Sheria namba 4 ya uendeshaji wa Mahakama ya mwaka 2011. 

Miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na Mahakama ya Tanzania kuhakikisha inaondoa mlundikano wa mashauri yaliyopo mahakamani kwa sasa. Katika hili, Majaji na Mahakimu wamepangiwa idadi ya kesi watakazosikiliza kwa mwaka kwa mfano, Majaji wa Mahakama ya Rufani na wale wa Mahakama kuu wamepangiwa kusikiliza mashauri 220 kwa mwaka, wakati mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya pamoja na Mahakama za Mwanzo watatakiwa kusikiliza mashauri 250 kwa mwaka.  

Hata hivyo pamoja na juhudi za Mahakama ya Tanzania za kuhakikisha inaondosha mashauri yaliyokaa muda mrefu mahakamani, bado Majaji wa Mahakama ya Rufani na wale wa mahakama kuu waliamua kujitolea kuacha likizo zao wanazoenda kati ya mwezi Desemba na Januari ili kusikiliza mashauri mbalimbali ukiwa ni mkakati wao waliojiwekea ili kupunguza mlundikano wa mashauri yaliyoko mahakamani. 

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman (kushoto) akiwa na Jaji Mfawidhi kanda ya Songea Mheshimiwa John Mgetta wakisoma majalada ya kesi katika mahakama ya Mwanzo ya Songea mjini mkoani Ruvuma.
 
Kufuatia mkakati huo, jumla ya mashauri 295 yalisikilizwa na kutolewa hukumu katika mwezi Januari mwaka huu katika mahakama kuu zote nchini. Aidha Mahakama ya Rufani ambayo vikao vyake hukaa kwa jopo la Majaji watatu kwa kila kesi, Majaji walifanikiwa kusikiliza mashauri au kesi 30 katika kipindi cha mwezi januari peke yake ambapo walitakiwa kuwa mapumzikoni kama ambavyo utaratibu wao wa likizo ulivyo.

Juhudi hizi pamoja na kujitoa kwa dhati kwa Majaji hawa wa Tanzania hakuna budi kupongezwa na kila raia wa Tanzania hasa kwa uzalendo wa juu waliouonyesha kwa Taifa lao. Hakika huu ni mfano unaopaswa kuigwa na taasisi nyingine za Serikali ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi wote.

Hata hivyo, mahakimu wa mahakama zote nchini nao pia hawana budi kupongezwa kwa dhati kutokana na uzalendo wa hali ya juu waliouonyesha katika kuhakikisha wanaondoa mlundikano wa mashauri ya muda mrefu na mfupi yaliyopo Mahakamani. Mahakimu hawa pia walijitolea kuachia likizo zao na kusikiliza mashauri mahakamani katika kipindi cha mwezi Januari. 

Jengo la Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
 
Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA katika Mahakama ya Tanzania Bwana Machumu Essaba alisema jumla ya mashauri 1414 yaliamuliwa katika kipindi hicho cha likizo katika mahakama za mahakimu wakazi nchini kote. Katika mahakama zote za wilaya nchini, jumla ya mashauri 2563 yaliamuliwa katika kipindi hicho. Aidha, katika Mahakama za Mwanzo zote nchini, jumla ya mashauri 24,473 yaliamuliwa katika kipindi hicho cha likizo za mahakimu cha mwezi Januari mwaka huu.
Alisema kutokana na kiwango cha juu cha usikilizwaji wa mashauri yaliyopo mahakamani, mlundikano wa mashauri hayo umeweza kupungua kutoka asilimia 20 na kufikia asilimia 16 ya mashauri yaliyokaa mahakamani kwa zaidi ya miaka miwili (backlock) kwa mwezi Februari mwaka huu katika Mahakama kuu ya Tanzania. Aidha, kulikuwa na jumla ya kesi 3511 mwezi Januari mwaka huu ambapo hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu, kesi hizo zimepungua na kufikia kesi 2305.
Bwana Essaba anaendelea kusema kuwa yo, kasi ya uondoshwaji wa mashauri kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka kati ya Januari na Machi 2016 katika mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ni zaidi ya asilimia 100. Aidha, katika Mahakama ya Rufani, wastani wa kasi ya uondoshwaji wa mashauri ni asilimia 142 na kwa upande wa Mahakama kuu kasi hiyo ni asilimia 116. Hii inamaanisha kuwa katika kipindi hicho mahakama hizo zimeweza kusikiliza kwa asilimia 100 mashauri yaliyokuwepo mahakamani na yale yaliyoingia.    
Kwa hatua hii iliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania, Majaji na Mahakimu hawana budi kupongezwa kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa wa kuendelea kuondoa mlundikano wa mashauri yaliyokuwepo na yale yanayoingia mahakamani.
Hata hivyo kwa kuwa mahakama ya Tanzania inafanya maboresho yanayolenga katika kuimarisha huduma ya utoaji wa haki nchini, wadau wa mhimili huu muhimu pamoja na wananchi kwa ujumla hawana budi kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha jukumu hili muhimu la utoaji wa haki nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni