Jumatano, 20 Julai 2016

JAJI MKUU WA TANZANIA AFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA SABA WA TAASISI YA WAAMUZI TANZANIA.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.  Mohamed   Chande Othman, akitoa hotuba yake leo  wakati akifungua mkutano mkuu wa saba  wa Taasisi ya Waamuzi Tanzania uliofanyika leo jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mkutano wa Luther House.  Katika mkutano huo, alisisitiza suala la kuzingatia maadili ya taaluma hiyo katika kushughulikia migogoro dhidi ya masuala ya kibiashara na sekta ya ujenzi.Kushoto ni Mwenyekiti wa taasisi hiyo,Kesogukewele Msita na kulia ni Mweka Hazina wa taasisi hiyo Dkt. Fetus Limbo.      

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.  Mohamed   Chande Othman, akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi  ya  wajumbe  wa taasisi hiyo  leo  mara baada ya kufungua mkutano mkuu wa saba  wa Taasisi ya Waamuzi Tanzania.

HOTUBA YA UFUNGUZI WA KIKAO KAZI CHA MAHAKAMA NA WADAU KUHUSU MPANGO MKAKATI



HOTUBA YA JAJI MFAWIDHI MAKAHAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA DODOMA  KATIKA KIKAO KAZI CHA MAHAKAMA YA TANZANIA NA WADAU WAKE KWENYE KUKAMILISHA MPANGO MKAKATI WA MAHAKAMA YA TANZANIA ILIYOTOLEWA KWENYE UKUMBI WA MIKUTANO WA HAZINA DODOMA TAREHE 19 JULAI, 2016.

Mhe Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe Mtendaji wa Mahakama Kuu, Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika, Mkemia Mkuu wa Serikali, Washiriki wote wa Kikao kazi hiki kutoka ndani ya Mahakama ya Tanzania na kutoka Taasisi mbali mbali ambazo ni wadau wetu, waandishi wa habari, mabibi na mabwana,
Ninawasalimu. 

Awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema katika shughuli zetu za kila siku na hivyo kutuwezesha kukutana hapa siku hii ya leo. Pia kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania ninawakaribisha wadau wetu wote waliohudhuria leo katika ukumbi huu.

Ndugu wadau wetu na wanasemina, ninayo furaha kubwa kupata nafasi hii adhimu ya kukutana na hadhira hii kwa lengo la kushirikiana katika hatua za kupeana mrejesho na kuendelea kuuboresha Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania. Suala hili kwa hakika linanipa faraja ya kiwango cha juu kwa kuwa linazidi kutuweka karibu na kutujengea uwezo wa pamoja katika uelewa, ujenzi na hatimaye utekelezaji wa Mpango Mkakati huu. Nimefajirika pia kupata taarifa kuwa wadau wetu mmeitikia wito na kufika hapa. Hii inadhihirisha kuwa mnathamini sana shughuli za Mahakama ya Tanzania. Na hivyo ni imani yangu kuwa ushiriki wenu utakuwa na athari chanya.

Vile vile taarifa nilizozipata zimenidhihirishia kuwa wakati semina hii inapoendea ukingoni matunda yaliyopatikana ni ya thamani kubwa katika kuongeza uelewa wa juhudi za makusudi ambazo tumeamua kuzichukua kuibadilisha Mahakama ya Tanzania kuwa chombo chenye kujibu maswali na kiu ya wananchi katika kupata haki kwa mujibu wa jukumu tulilokabidhiwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara.

Ndugu wadau na wanasemina nia ya kazi hii ambayo inafanyika hapa Dodoma kwa wiki mbili ni kuhakikisha kuwa, tunachukuana wote katika hatua zote za msingi za uundwaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania, kuyaelewa kwa undani malengo yetu ya msingi, kuyaoanisha na Dira yetu, Misingi tuliyojiwekea, Maeneo ya Matokeo makubwa, Malengo ya kimkakati, maeneo ya kuyafanyia kazi, hatua muhimu za kuchukua kwa kila kazi inayotakiwa kufanyika na hatimaye kujua viashiria vikuu vinavyoonesha endapo mafanikio yamepatikana au la. Zoezi hili linasaidia kuhakikisha kunakuwa na uendelevu usio na maswali katika utekelezaji hata pale ambapo sisi tuliouandaa Mpango hatupo.

Vile vile mpango huu unatoa fursa  kwetu kujua umuhimu, nguvu na nafasi waliyonayo wadau wetu kufanikisha utendaji wa Mahakama katika kuyafikia malengo ya kutoa huduma kwa wananchi.Tunatambua kuwa peke yetu hatuwezi na kwa hali hiyo utendaji wa pamoja unahitajika sana kuanzia ngazi za Mahakama yenyewe na kwa kushirikiana na wadau wetu.
Kwa kuelewa kuwa wadau wetu ni chachu ya mafanikio ya Mahakama na kwa sekta nzima ya Sheria katika utoaji wa haki, tumeweza kuainisha maeneo makuu ya mashirikiano na aina ya msaada mahsusi ambao tutahitaji kutoka kwenu. Kama usemi usemao kuwa ‘Kidole kimoja hakivunji chawa’ ndivyo ambavyo Mahakama ya Tanzania inatambua kuwa ‘Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’. Suala hili limeainishwa katika mawasilisho yatakayofanywa na  makundi tofauti muda mfupi ujao.

Kwa wadau wetu mtakumbuka kuwa katika juhudi zetu mbalimbali tumehakikisha kuwa tunashirikiana nanyi katika hatua zote za kuandaa Mpango wetu huu  bila kificho ili kuwawezesha nanyi kwa upande wenu kutoa nafasi ya kutuweka katika mipango yenu kwenye hatua za uandaaji na utekelezaji. Kuna usemi usemao ‘Ukikimbia peke yako utafika haraka bali ukitembea na wenzako utafika mbali’. Mahakama inataka kufika mbali katika kutoa huduma zake ambazo zinamlenga mwananchi ndiyo maana tunaomba tutembee pamoja.

Ndugu wanasemina, katika kipindi mlichokuwa hapa wapo ambao lugha kuhusu Mpango mkakati huu ilikuwa ngumu kuiielewa; ilionekana kuwahusu zaidi wataalam wa uchumi na menejimenti tu na najua wengi wetu walikuwa wanaipa kisogo kwa kuona kama hawataelewa chochote. Lakini naamini kuwa kwa sasa hali ni tofauti. Nimepata ushuhuda wa walio wengi ni jinsi gani sasa mnaongea lugha moja. Basi kwa kuwa sasa mmeelewa na kwamba nyenzo hii iko akilini na mikononi mwenu, ninaamini kwamba Mahakama yote ya Tanzania pamoja na wadau wetu sasa tutaimba wimbo mmoja. Tutakuwa na utekelezaji unaoendana na malengo kwa kufuata barabara tuliyoichonga kwa pamoja. Mtakaposikia yale mtakayoelezwa na wawasilishaji, tafadhali toeni tena michango ya kuendelea kuboresha mpango huu na tutaizingatia kwa kadri itakavyowezekana.

Kwa wadau wetu wote, matarajio yangu na ya Mahakama ya Tanzania kwa ujumla kwenu ni kwamba msaada tunaouhitaji kutoka kwenu utapatikana kwa wakati kwa kuwa mahitaji yetu kwenu sasa yatakuwa sio mageni tena na kwamba, kwa kutekeleza jukumu lenu mtakuwa mnaelewa kuwa hamuifanyii Mahakama tu bali mnafanya hivyo kwa ajili ya watanzania wote na walipa kodi wa Taifa hili.

Ndugu wadau na wanasemina, aidha, nimejulishwa kuwa mara baada ya kukamilika kwa kazi hii hapa wiki hii, wiki ijayo timu ya wataalamu katika Mahakama na baadhi ya washiriki wa semina hii watakuwa na kazi ya kuufikisha Mpango Mkakati huu katika mikoa yote ya Tanzania bara. Hili ni jambo zuri na hatua hiyo ambayo itaifanya Mahakama ya Tanzania kuwa Taasisi ya kipekee katika kuandaa Mpango Mkakati huu kwa njia shirikishi na kuufikisha nchi nzima kwa wakati mmoja. Ninawataka kuhakikisha kuwa wadau wetu huko katika ngazi za mikoa na wilaya wanahusishwa katika mrejesho huu ili nao waweze kuumiliki na kuufanyia kazi.
Ni rai yangu kuwa wenzetu katika ngazi zote wataendelea kutoa mafunzo kuhusu Mpango Mkakati huu ili uweze kumfikia kila mtumishi kwa nia ya kuwafanya waelewe njia tunayopaswa kutembea. Hatutakiwi tena kupit kwenye vichaka; barabara nzuri imetengenezwa tunapaswa kuitumia na kuendelea kuikarabati ili vizazi vingine viweze kufurahia kazi nzuri iliyofanywa na watangulizi wao.

Kwa watumishi wa Mahakama, ninapenda kuwakumbusha kuwa utendaji wetu wa kazi utapimwa kwa kuzingatia jinsi tunavyotekeleza majukumu yetu kulingana na Mpango Mkakati huu. Hivyo, ni matarajio yetu sote kuwa kazi hii yote haitaishia katika makaratasi bali itatupeleka kuishi kwa matendo yenye kuleta matokeo chanya. Kwa hali hiyo tutaelekeza rasilimali zetu zote, yaani  watu, fedha na muda katika kuleta matokeo makubwa yanayotarajiwa. Na tusikubali nguvu hii iwe ni nguvu ya soda na kuishia hewani bure.
Aidha, nina imani kwamba endapo  tutajikita katika kufanikisha uimara wa nguzo zetu tatu za Mpango Mkakati wetu yaani, utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali; upatikanaji wa haki kwa wakati na uhusishwaji wa wadau na imani ya wananchi hakika tutatimiza  ndoto ya kuifikia Dira yetu. Hakuna lisilowezekana, kila mmoja atimize wajibu wake.
Ndugu wanasemina, ninapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya na ninawatakia kila heri katika utekelezaji wake.

Ndugu wadau na wanasemina, mwisho ninawatakia heri na Baraka za Mwenyezi Mungu katika ushiriki wa uboreshaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa siku ya leo.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

M.A. KWARIKO,
JAJI MFAWIDHI,
MAHAKAMA KUU YA TANZANIA,
DODOMA .




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni