Na
Lydia Churi- Mahakama ya Tanzania
Mahakama ya Tanzania imeamua
kuchukua juhudi za makusudi ili kubadilisha muonekano wake na kuwa chombo
kitakachojibu maswali na kuondoa kiu ya watanzania katika kupata haki kwa
wakati.
Akifungua Mkutano wa
Mahakama ya Tanzania na wadau wake wa kujadili utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
mhimili huo leo mjini Dodoma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma
Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko amesema Mahakama ya Tanzania inakusudia kukibadilisha chombo hicho ili kiweze kutoa
haki kwa wakati kwa mujibu wa jukumu ililopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Alisema katika kufanikisha
azma hiyo, Mahakama ya Tanzania inaendelea na mafunzo ya wiki mbili kwa
watumishi wake yanayolenga kuuboresha Mpango Mkakati wake kwa kushirikiana na
wadau ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na taswira ya mahakama
inakuwa chanya wakati wote.
Jaji Kwariko amesema
Mahakama imeamua kuwashirikisha wadau kwenye Mpango Mkakati wake kwa kuwa umuhimu
na nguvu waliyonayo Sitasaidia kufanikisha utendaji wa Mahakama katika
kuyafikia malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Jaji Kwariko
aliwataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kufanya kazi kwa bidii katika
kuutekeleza Mpango Mkakati kwa kuwa utendaji kazi wao utapimwa kwa jinsi
watakavyotekeleza majukumu yao kulingana na Mpango Mkakati huo. Aliongeza kuwa
Mahakama ya Tanzania itaelekeza rasilimali zake zote kama vile watu, fedha na
muda katika kuleta matokeo makubwa yanayotarajiwa.
Alisema endapo watumishi
hao watajikita katika kufanikisha uimara wa nguzo zote tatu za Mpango Mkakati huo,
upatikanaji wa haki kwa wakati na uhusishwaji
wa wadau na imani ya wananchi vitakifanya chombo hicho kutimiza ndoto yake na
kuifikia dira yake. Nguzo tatu za Mpango Mkakati huo ni Utawala bora, Uwajibikaji
na Usimamizi wa rasilimali.
Naye Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati alisema baada ya Mpango
Mkakati wa Mahakama kukamilika, watumishi watasaini kadi itakayokuwa ikionyesha
namna ya utekelezaji wa Mpango Mkakati na kadi hiyo itaweka alama za kuonyesha
ufaulu katika utekelezaji, endapo mtumishi atapata alama ndogo atachukuliwa
hatua.
Akizungumzia namna Mahakama
inavyopambana na rushwa, Msajili huyo alisema Mahakama imeweka mazingira ya
uwazi katika utoaji wa huduma zake pamoja na kuweka mifumo ya kielekitroniki na
kuhusisha wadau wake katika utendaji kazi wake.
Mahakama ya Tanzania
inaendelea na Mafunzo ya wiki mbili kwa watumishi wake kuhusu uandaaji na utekelezaji
wa Mpango Mkakati wake ambapo leo ilikutana na wadau wake ili kujadili namna ya
utekelezaji wa Mpango huo.
Wadau waliohudhuria,
mafunzo hayo leo ni Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Polisi Makao Makuu, Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU na Wakala wa Majengo Tanzania-TBA.
Wengine ni pamoja na Baraza
la Habari Tanzaia-MCT, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Usuluhishi wa
Migogoro, Ofisi ya Nyaraka za Taifa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa-TAMISEMI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni