Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akisalimiana na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa pindi alipowasili katika
viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha mapema leo
kwa ajili ya kuzindua rasmi Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na Mradi wa Maboresho
wa Huduma za Mahakama, katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi. Evarist
Ndikilo.
Waziri
wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akionyeshwa michoro
mbalimbali ya miundombinu ya majengo ya Mahakama pamoja na nyumba za Mahakama pindi
alipowasili katika hafla fupi ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Mahakama
uliofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya
Kibaha.
Waziri
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akitoa hotuba yake
wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Mahakama uliofanyika katika viwanja vya
Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha, katika hotuba yake Mhe.
Waziri Mkuu amesifu jitihada za Mahakama katika kuboresha huduma zake na
kuzitaka Taasisi nyingine kuiga mfano wa Mahakama kwa kuwa na mikakati
itakayowezesha maboresho ya huduma zao.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akitoa hotuba yake wakati wa
uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Mahakama, katika hotuba yake Mhe. Jaji Mkuu aliongelea juu ya nguzo tatu za Mkakati huo
ambazo ni Utawala bora, Uwajibikaji na usimamizi wa Rasilimali, Upatikanaji na
utoaji wa haki kwa wakati pamoja na Kuimarisha imani ya jamii na ushirikishaji
wa wadau katika shughuli za Mahakama.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akijadili jambo na Mhe. Waziri
Mkuu katika hafla ya uzinduzi rasmi
Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama.
Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi.Bella Bird akitoa hotuba yake wakati wa hafla hiyo,
katika hotuba yake Bi. Bird alisema kuwa Benki ya Dunia itasaidia utekelezaji
wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania.
Baadhi
ya Watumishi wa Mahakama pamoja na Wananchi wakiwa katika hafla fupi ya
uzinduzi rasmi Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama pamoja na Mradi wa Maboresho
wa Huduma za Mahakama.
Waziri
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi
wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama, wanaoshuhudia ni Waziri wa
Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, (wa kwanza kushoto), Naibu
Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansansu (wa
tatu kulia), wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi. Evarist Ndikilo
na wa kwanza kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand
Wambali.
Waziri
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi
wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama, anayeshuhudia kulia ni Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansansu.
Mhe.
Waziri Mkuu akionesha nakala za vitabu
vya Mpango Mkakati wa Mahakama mara baada ya kuzindua rasmi.
Waziri
Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akifurahia jambo pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Mohamed Chande Othman (kulia), Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi. Evarist
Ndikilo (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Bella Bird
(kushoto) muda mfupi baada ya uzinduzi wa Mpango Mkakati.
Waziri
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja baadhi
ya Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Pwani,wa nne kushoto ni Jaji Mkuu wa
Tanzania,Mhe. Mohamed Chande Othman, wa nne kulia ni Naibu Spika wa Bunge la
Tanzania, Dkt. Tulia Ackson Mwansansu, wa tatu kushoto ni Waziri wa Katiba na
Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe, wa tatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Mhandisi. Evarist Ndikilo, wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wa kwanza kushoto ni Bi. Bella Bird, Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia na wa kwanza kulia ni Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia.
Meza
Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Kada mbalimbali wa Mahakama
mbele ya jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ya
Kibaha ambalo Mhe.Waziri Mkuu amelinzidua pia katika hafla hiyo.
Meza
Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi na baadhi
ya wananchi wengine waliohudhuria katika hafla hiyo.
TAASISI
ZA SERIKALI ZATAKIWA KUIGA MFANO WA MAHAKAMA- WAZIRI MKUU
Na
Mwandishi, MAHAKAMA YA TANZANIA
Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi za
serikali kuiga mfano wa Mahakama ya Tanzania katika kuwapatia wananchi huduma
bora na kwa wakati.
Akizindua Mpango
Mkakati wa miaka mitano pamoja na Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama,
Waziri Mkuu ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha uandaaji wa Mpango
Mkakati unaolenga katika kuimarisha Utawala bora, Upatikanaji na utoaji wa haki
kwa wakati pamoja na kuimarisha imani kwa wananchi na Ushirikishwaji wa wadau
katika shughuli za mahakama.
Alisema Mpango Mkakati
wa Mhimili huu si tu kwamba ni muhimu kwa Mahakama bali pia ni muhimu kwa
Serikali na watanzania wote kwa ujumla kwa kuwa umelenga katika kuboresha
huduma zinazotolewa na Mahakama katika ngazi zote nchini na kuzisogeza karibu
na wananchi.
Waziri Mkuu alisema
azma ya Mahakama ya kuandaa Mpango Mkakati inakwenda sambamba na malengo ya
Serikali ya kudhamiria kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa kufanya maboresho katika
utendaji wa vyombo vya maamuzi ikiwemo Mahakama.
Aidha, Waziri Mkuu ameishukuru
Benki ya Dunia kwa kukubali kuikopesha Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 141
zitakazosaidia kuboresha Huduma za Mahakama katika kipindi cha miaka mitano.
Aliihakikishia Benki ya Dunia kuwa Serikali kupitia Mahakama itatumia fedha
hizo kwa uangalifu na uaminifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naye Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amesema Mahakama ya Tanzania
imejipanga kuhakikisha inaongeza idadi ya mahakama zake ili kuondokana na
tatizo la upungufu wa mahakama katika ngazi zote.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania na Mradi wa
Maboresho ya Huduma za Mahakama, Jaji Mkuu alisema katika kipindi cha miaka
mitano, Mahakama inatarajia kujenga majengo ya mahakama Kuu 5 hadi 7 ili
kupunguza umbali wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa mikoa isiyo na Mahakama Kuu.
Aliitaja mikoa
isiyokuwa na Mahakama kuu kuwa ni Lindi, Katavi, Geita, Simiyu, Njombe, na Songwe.
Mingine ni pamoja na Singida, Manyara, Pwani na Morogoro. Aliongeza kuwa kati ya mikoa 25 ya Tanzania
Bara ni mikoa 14 tu ndiyo yenye Mahakama kuu mpaka sasa.
Kwa upande wa Mahakama
za wilaya, mahakama itakuwa na uwezo wa kujenga mahakama kati ya 30-40,
mahakama za hakimu Mkazi kati ya 5-8 na aina mbalimbali za mahakama za Mwanzo
kati ya 70-100 katika kipindi cha mwaka mmoja kwa kutumia teknolojia ya ujenzi
ya kisasa.
Akizungumzia upatikanaji
na utoaji wa haki kwa wakati, Jaji Mkuu alisema hadi kufikia Agosti 30, mwaka
huu. Mahakama kwa ngazi zote , imefanikiwa ndani ya miaka mitatu kufikia lengo
la kuwa na mashauri asilimia 80 ya mashauri yenye umri unaokubalika kimataifa
wa kati ya miezi 6-24.
Alisema, katika mwaka
wa fedha wa 2016/2017 mahakama inalenga kuondoa mashauri yote ya zaidi ya miezi
3-6 kwa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na zile za Hakimu Mkazi (Mkoa) ili kuwa na
asilimia 90 ya mashauri yote yaliyoko kwenye ngazi hizo za Mahakama yawe ndani
ya miezi 3-6. Aliongeza kuwa nguvu nyingi inaelekezwa huko kwa kuwa ndiko
kwenye watanzania zaidi ya asilimia 80.
Mpango Mkakati wa
Mahakama ya Tanzania ni mwongozo wa kuhakikisha mikakati ya Taasisi
inatekelezwa ili kufikia Dira ya Mahakama yenye lengo kuu la kuifanya Mahakama
iendelee kutoa huduma zinazolenga upatikanaji wa haki sawa kwa wote na kwa
wakati.
Mpango huu utatekelezwa
Katika kipindi cha miaka mitano 2015/16- 2019/2020 kwa kufuata nguzo tatu
ambazo ni Utawala na Menejimenti bora ya Rasilimali, Upatikanaji na utoaji wa
Haki kwa wakati na kuimarisha imani ya Jamii na Ushirikishaji wa wadau katika
shughuli za Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni