1 Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe.
Christopher Kourakis (katikati), akiongea jambo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Mohamed Chande Othman katika ofisi ya Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji
Kourakis yupo nchini kwa ziara ya siku tatu lengo likiwa ni kujenga ushirikiano
katika utendaji wa Mahakama. Kushoto ni Bi. Emma Gorman, Katibu wa Jaji Mkuu wa
Australia Kusini.
Jaji Mkuu wa Australia Kusini akisoma
kitabu kinachohusu Chama cha Majaji Wanawake Tanzania alipotembelea ofisini kwa
Mwenyeji wake ambaye ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Bw. Hussein Kattanga (katikati), Bi. Katarina Revocati (wa kwanza kulia), wakiwa kikao cha mazungumzo kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na
Jaji Mkuu wa Australia Kusini mapema tarehe 05.10.2016.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman akisisitiza jambo katika mazungumzo baina yake na Jaji Mkuu wa
Australia Kusini, Mhe. Christopher Kourakis.
Wakiendelea na mazungumzo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman akizungumza jambo mbele ya baadhi ya Wahe.Majaji wa Mahakama ya
Rufani na Watendaji wa Mahakama, katika mkutano huo, Mhe. Jaji Mkuu wa
Australia Kusini . Katika mkutano huo Mhe. Jaji Mkuu wa Australia ya Kusini pia alizungumza na Majaji hao masuala mbalimbali yahusuyo
Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman (katikati), Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe. Christopher
Kourakis (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa
Mahakama ya Rufani mara baada ya kuzungumza nao.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman (katikati), Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe. Christopher
Kourakis (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa
Mahakama ya Rufani na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania.
J Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe.
Christopher Kourakis akisisitiza jambo alipokuwa katika mkutano wa pamoja kati
yake, Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na waandishi wa habari,katika mkutano huo
alizungumzia juu ya umuhimu wa maboresho ya Mahakama pamoja na kupeana uzoefu
juu ya masuala ya Mahakama baina ya nchi hizo mbili.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman akizungumza jambo katika Mkutano na Waandishi wa Habari, wa
kwanza kushoto ni Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe. Christopher Kourakis na
kulia ni Msajili Mahakama ya Rufani, Mhe. John Kahyoza.
1 Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa
katika mkutano huo.
Waandishi wa Habari na baadhi ya Maafisa wa
Mahakama wakiwa katika mkutano huo.
Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ilvin Mugeta akitoa ufafanuzi juu ya shughuli mbalimbali za kimasjala pindi Jaji Mkuu wa
Australia Kusini alipotembelea Masjala hiyo ya wazi iliyopo Mahakama Kuu, Kanda
ya Dar es Salaam.
Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe.Ilvin Mugeta akimuonyesha Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe. Christopher
Kourakis sehemu ya Mapokezi ya Mahakama Kuu ambapo watu wenye kesi mbalimbali
hupata msaada wa nini cha kufanya kuhusiana na taratibu za Kimahakama, wa
kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand
Wambali.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Ferdinand Wambali akifafanua kitu walipokuwa katika moja ya kumbi za Mahakama
Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi akiongeza jambo na
baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania walipokuwa kwenye Mkutano pamoja
na Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe. Christopher Kourakis.
Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Mhe. Christopher
Kourakis (katikati), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand
Wambali wakiwa katika picha ya pamoja na Wahe.Majaji wa Mahakama Kuu mara baada
ya mazungumzo.
TEKNOLOJIA YA KISASA KUTUMIKA KUENDESHA MASHAURI MAHAKAMANI
Na Lydia Churi- Mahakama
Mahakama ya Tanzania inakusudia kushirikiana na Mahakama ya
Australia ya Kusini katika teknolojia za kuendesha mashauri mahakamani ili
kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa Haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Akizungumzia ziara ya Jaji Mkuu wa Australia ya Kusini
Mheshimiwa Christopher Kourakis iliyoanza leo nchini, Jaji Mkuu wa Tanzania
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amesema ziara ya kiongozi huyo inalenga
kuimarisha na kujenga ushirikiano katika maeneo matatu likiwemo eneo la
teknolojia ya kuendesha mashauri mahakamani.
Alisema Australia ya Kusini inaendesha mashauri mahakamani
kwa kutumia teknolojia ya kisasa hivyo Mahakama ya Tanzania haina budi kuhama
kutoka mifumo ya kuendesha mahakama kwa mkono kwenda kwenye teknolojia ya
kidijiti.
Alisema Mahakama inakusudia kuwapeleka wasajili na watendaji
wa mahakama nchini Australia ya Kusini ili wakajifunze mifumo hiyo kwa ajili ya
kuanza kuitumia kuendeshea mahakama za Tanzania.
Aliyataja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa ni eneo la
utoaji wa mafunzo kwa Majaji, Mahakimu na Wasajili wa Mahakama ya Tanzania huku
akisema eneo la tatu ni la namna ya kuanzisha Kada mpya ya Wapiga Chapa Maalum
wa Mahakama watakaokuwa wakitumia mashine ndogo inayochapa wakati mashauri
yakiendelea Mahakamani.
Akiielezea kada hiyo mpya, Jaji Mkuu alisema itawezesha
kupatikana kwa nakala za mashauri ndani ya siku moja na kwamba watumishi hao ni
tofauti na makatibu Muhtasi ambapo mishahara yao itakuwa ni mikubwa kuliko ile
ya Makatibu Muhtasi.
Naye Jaji Mkuu wa Australia ya Kusini alisema Mahakama za
nchini kwake zinaendesha mashauri kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kidijiti
hivyo nchi yake itashirikiana na Tanzania ili nayo iweze kuendesha
mashauri mahakamani kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Akizungumzia kuhusu adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa
kesi za mauaji nchini Australia ya Kusini, Mheshimiwa Kourakis alisema adhabu
hiyo iliondolewa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo msukumo wa Haki za
Binadamu.
Alisema nchi yake pia ina mfumo ambapo endapo mtuhumiwa
wa mauaji atakiri kosa ndani ya wiki sita basi atapunguziwa adhabu yake kwa
asilimia 40. Aliongeza kuwa adhabu ya kifo nchini kwake ni kifungo cha maisha
na endapo atakiri kosa atapunguziwa adhabu. Kiwango cha chini cha adhabu ya
kifo ni kifungo cha miaka 20 jela.
Jaji Mkuu wa Australia ya Kusini leo ameanza ziara ya kikazi
ya siku tatu nchini ambapo ametembelea Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu na pia
anatarajia kutembelea Mahakama ya Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni