Na
Lydia Churi-Mahakama
Majaji Wafawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine wamepongezwa kwa kumaliza vizuri
kesi za uchaguzi zilizofunguliwa katika Mahakama Kuu kanda mbalimbali nchini na
pia kutenga muda wa kujadili changamoto zilizotokana na kesi hizo.
Akizungumza na Majaji
Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo jijini Arusha, Jaji Mkuu wa Tanzania
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amewapongeza Majaji hao kwa kujitoa katika
kusikiliza kesi hizo na kuzitolea hukumu kesi nyingi kwa kipindi kifupi licha
ya kesi chache kubakia mahakamani.
Jumla ya kesi 53 za Ubunge
zilizotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilifunguliwa katika Mahakama Kuu
kanda za Dar es salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza. Kanda
nyingine ni Shinyanga, Songea, Sumbawanga, na Tanga. Kati ya kesi hizo, kesi 31
zilimalizika katika hatua za awali na kesi 22 ziliendelea, mpaka sasa kesi 19 zimemalizika. kesi tatu
bado ziko mahakamani.
Hata hivyo kesi zote 196
zilizotokana na uchaguzi wa madiwani zilimalizika mapema katika Mahakama mbalimbali za Hakimu Mkazi nchini. Katika
kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa uchaguzi Mkuu nchini, zaidi ya
asilimia 94 ya kesi za uchaguzi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu zimemalizika
wakati asilimia 100 ya kesi zote za udiwani zimemalizika.
Aidha, Jaji Mkuu amewataka
Majaji hao kuweka mikakati ya kuhakikisha kasi ya kupunguza kesi mahakamani
hasa zile za muda mrefu inaongezeka ili kupunguza malalamiko yanayotokana na
kuchelewa kutoa hukumu na kutopatikana kwa nakala za hukumu kwa wakati.
Mheshimiwa Chande amewataka
Majaji kusimamia suala la maadili ndani ya Taasisi hiyo ili kurejesha imani ya
wananchi kwa Mahakama yao.
Kuhusu suala la Maadili kwa
Mahakimu, Jaji Mkuu amesema wameomba ushauri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa
endapo hakimu atashtakiwa kwa kosa la rushwa ataondolewa kazini kwa maslahi ya
Umma hata kama atashinda kesi hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman akizungumza na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (hawapo pichani) wakati wa Mkutano Majaji hao uliofanyika leo jijini Arusha. Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu aliwapongeza Majaji hao kwa kumaliza vizuri kesi nyingi zilizotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa Ferdinand Wambali akizungumza wakati wa Mkutano wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliofanyika leo jijini Arusha.
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu wakiwa katika Mkutano wao leo jijini Arusha
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na Wasajili, Mahakimu na Watendaji wa Mahakama waliohudhuria Mkutano huo leo jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni