FUATENI
MAADILI NA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI-JAJI MKUU WA TANZANIA
Na
Lydia Churi-Mahakama, Mbeya
Watumishi wa Mahakama
ya Tanzania wametakiwa kufuata maadili ya kazi, kwa kuongeza nidhamu na kutoa
huduma bora kwa wananchi wanaofika kutafuta haki katika mahakama mbalimbali
nchini ili kuongeza imani ya juu ya utendaji wa mahakama.
Akizungumza na
watumishi wa ngazi zote wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya, Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Mohamed Chande Othman amesema Mahakama ni chombo kinachotoa huduma hivyo watumishi
hao hawana budi kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndiyo wateja wao.
Aliwataka watumishi
hao kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayoletwa mahakamani na kuyapatia
ufumbuzi ili kuzimaliza kero na hoja mbalimbali zinazoelekezwa kwenye taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa pamoja
na watumishi kutoa huduma bora, mahakama itahakikisha inaboresha mazingira ya
kazi kwa watumishi hao.
Alisema Mahakama ya
Tanzania inafanya maboresho ya huduma zake ambapo tayari imeanza kukarabati
majengo yaliyo katika hali mbaya na kujenga majengo mapya hasa ya mahakama za
Mwanzo na wilaya ikiwa ni pamoja na
kuongeza idadi ya watumishi wa kada mbalimbali.
Kwa mujibu wa Sheria,
kila wilaya inapaswa kuwa na mahakama ya wilaya. Kwa upande wa Mahakama za
Mwanzo, zipo 960 tu wakati mahitaji ni kuwa na mahakama za mwanzo katika kila
kata ambapo kuna kata zaidi ya 3000 nchi
nzima.
Jaji alisema mahakama
ya Tanzania tayari imeanza ujenzi wa mahakama za mfano kumi za wilaya zinazojengwa
kwa kutumia teknolojia rahisi, ya muda mfupi na yenye gharama nafuu. Mahakama
hizo ziko mbioni kukamilika.
Naye
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Mhe. Noel Chocha alisema kasi ya
upunguzaji wa mlundikano wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo zilizoko kanda
ya Mbeya ni nzuri kwa kuwa mashauri yaliyobaki mahakamani ni 670 tu yenye umri
wa siku moja mpaka miezi sita mahakamani. Jumla ya mashauri 12,448 yamemalizika
katika mahakama za Mwanzo.
Alisema
changamoto katika kanda yake ni ufinyu wa fedha inayotengwa kwa ajili ya
kuendesha mashauri hali inayoweza kudumaza mfumo wa wa utoaji haki katika kanda
yake.
Alisema hadi sasa, Mahakama
Kuu kanda ya Mbeya inayo mashauri 177 ya madai, 398 yanayohusu migogoro ya
Ardhi na 394 ni mashauri ya jinai.
Jaji Mkuu wa Tanzania
leo amehitimisha ziara ya siku mbili kwa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga
pamoja na kanda ya Mbeya ambapo alikagua shughuli za Mahakama kwenye kanda
hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni