Jumanne, 20 Desemba 2016

MAHAKAMA YA TANZANIA KUTOA KIPAUMBELE KATIKA ENEO LA UTOAJI HAKI


Na Lydia Churi-Mahakama, Rukwa

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amesema Mahakama ya Tanzania inatoa kipaumbele katika eneo la utoaji wa haki kwa kuwa ndiyo msingi wa wananchi kupata haki sawa na kwa wakati.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi leo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, Jaji Mkuu alisema ili kulipa uzito unaostahili  suala la utoaji haki,  wamedhamiria kuongeza idadi ya Mahakama mbalimbali nchini ikiwa, ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi wa Mhimili huo wakiwemo Majaji na Mahakimu.  

Alisema hivi sasa Taasisi yake imeanza ujenzi wa Mahakama kwa kutumia teknolojia rahisi, ya muda mfupi na yenye gharama nafuu kujenga majengo ya mbalimbali ya Mahakama, akitolea mfano wa ujenzi wa mahakama za mfano kumi za wilaya  ambazo ziko mbioni kukamilika.

Jaji Mkuu pia amesisitiza ushirikiano baina ya Mahakama na Taasisi ambazo ni wadau wa Mahakama na kuongeza kuwa jambo hili litasaidia umalizikaji wa kesi kwenye mahakama hasa za Mwanzo, wilaya na zile za Hakimu Mkazi kwa wakati.

Kwa mujibu wa Mhe. Chande, asilimia 92 ya kesi zote  zilizoko mahakamani kwa nchi nzima ziko kwenye mahakama za Mwanzo, wilaya na zile za Hakimu Mkazi ambapo asilimia 72 kati ya kesi hizo zipo katika mahakama za Mwanzo.

Akizungumzia suala la maadili kwa watumishi wa mahakama, Jaji Mkuu alisema mahakama imeanzisha mkakati wa kupambana na rushwa  kwa kuanzisha kamati za maadili za wilaya na mkoa zinazochukuliwa kama kamati ndogo za Tume ya utumishi wa mahakama ambapo wakuu wa mikoa na wilaya ndiyo wenyeviti wa kamati hizi.

Aidha, Jaji Mkuu ameipongeza Mahakama kuu kanda ya Sumbawanga kwa kutoa nakala za hukumu kwa wakati kwa wananchi waliokuwa na kesi mahakamani. Alisema kwa utaratibu wa mahakama, nakala za hukumu zinapaswa kutoka ndani ya siku 21 tangu kumalizika kwa kesi lakini suala hili limekuwa ni changamoto kwa mahakama nyingi nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven ameipongeza Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga kwa kutoa nakala za hukumu kwa wakati kwa kuwa suala hili limekuwa ni changamoto kwa muda mrefu.

Alisema amani na usalama uliopo katika mkoa wa Rukwa inachangiwa kwa kiasi kikubwa na Mahakama ya Tanzania kutoa hukumu za haki na kwa wakati na kuitaka Mahakama kuendelea kudumisha amani iliyopo kwa kutenda haki.

Wakati huo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga Mhe. John Mgeta alisema mahakama kuu kanda ya Sumbawanga imeweka mikakati ya kuondokana na mashauri ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya mahakimu kwa mahakama zinazolemewa na mashauri pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya vifungu vya sheria ili kumaliza mashauri yasiyopaswa kuwepo mahakamani.

Aliitaja mikakati mingine kuwa ni kutoa maahirisho ya muda mfupi mfupi ya kesi na kuwashirikisha wadau muhimu wa mahakama wakiwemo mawakili, jeshi la polisi, ustawi wa jamii, madaktari wa mikoa , magereza na Takukuru.

Katika ziara yake mkoani Rukwa, Jaji Mkuu alipata nafasi ya kuzungumza na mawakili wa Serikali na wale wa kujitegemea na kuzungumza na watumishi wa kada zote wa mahakama ya Tanzania kanda ya Sumbawanga.

Jaji Mkuu yuko kwenye ziara ya siku mbili ya kukagua shughuli za mahakama katika mikoa ya Rukwa na Mbeya.


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za mahakama katika Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga jana. 

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Rukwa baada ya kuzungumza na kamati hiyo jana alipomtembelea Mkuu wa Mkoa huo katika ziara ya kukagua shughuli za mahakama katika Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga jana.

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akisalimiana na watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga mara baada ya kuwasili akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za mahakama katika Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga jana.


 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga jana mjini Sumbawanga.
Watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga wakimsikiliza jaji Mkuu jana.

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akipanda mti katika viwanja vya Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga kama ishara ya kutembelea mahakama hiyo jana.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni