Na
Lydia Churi-Mahakama
Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema Serikali kupitia Mahakama ya Tanzania iko kwenye
mkakati wa kusogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi ili kuwapatia haki
kwa wakati.
Waziri Mwakyembe ameyasema
hayo leo jijini Dar es salaam wakati akikagua maendeleo ya
ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kigamboni linaloendelea kujengwa kwa
kutumia teknolojia ya gharama nafuu ya Moladi.
Alisema kuwa mpango
wa Serikali ni kujenga Mahakama nyingi katika ngazi zote na hasa Mahakama za
Mwanzo ambazo zinatakiwa kuwepo kwenye kila kata hapa nchini. Kwa mujibu wa
waziri huyo, idadi ya Mahakama za Mwanzo mpaka ni 960 tu wakati kuna kata zaidi
ya 3000.
Akizungumzia kasi ya
upunguzaji wa mlundikano wa kesi mahakamani, Waziri Mwakyembe alisema Mahakama
ya Tanzania kupitia mpango mkakati wake wa miaka mitano inalenga kupunguza
idadi ya kesi za zamani zilizopo kwenye mahakama mbalimbali nchini.
“Alisema asilimia 60
ya kesi zilizopo kwenye mahakama zetu ni zile za zamani na kwa sasa
tumefanikiwa kuzipunguza kesi hizi na kubaki asilimia 15 tu”, alisema Waziri
huyo.
Kuhusu suala la
rushwa mahakamani, Mhe. Mwakyembe alisema Wizara yake iko kwenye mapambano
makali dhidi ya vitendo hivyo ambapo hivi karibuni imepeleka bungeni Muswada wa
Sheria ya kumlinda mtoa taarifa ili wananchi wengi zaidi waweze kutoa taarifa
za vitendo hivyo bila hofu yoyote juu ya usalama wao.
Naye Mbunge wa
Kigamboni Mhe. Faustine Ndungulile ambaye pia alifuatana na Waziri Mwakyembe
katika ukaguzi wa jengo la mahakama aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kujenga
mahakama ya kisasa Kigamboni ambayo itasaidia kusogeza karibu huduma za
mahakama hasa kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Kigamboni.
Akitolea mfano
wananchi wa eneo la Pemba Mnazi ambalo lipo umbali wa zaidi ya kilometa 70
kutoka mahali inapojengwa Mahakama hiyo kuwa sasa wataweza kujua haki zao
kupitia huduma zinazotelewa na mahakama.
Alisema wananchi wa jimbo
la Kigamboni wanakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo zile za mashauri
kusikilizwa kwa muda mrefu, na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wa
Mahakama wasio waaminifu.
Jengo la Mahakama ya Mwanzo
Kigamboni linalojengwa kisasa zaidi na kwa kutumia teknolojia yenye gharama
nafuu linatarajiwa kukamilika ifikapo Februari mwakani.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison mwakyembe (Kushoto) akizungumza na Mbunge wa Kigamboni Mhe. Faustine Ndunguulile wakati walipotembelea Mahakama ya Mwanzo ya Kigamboni ili kukagua ujenzi wa Mahakama hiyo jana jijini Dar es salaam
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Ndugu Solanus Nyimbi akimwelezea jambo waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati alipotembelea Mahakama ya Mwanzo ya Kigamboni ili kukagua ujenzi wa
Mahakama hiyo jana jijini Dar es salaam. Kulia ni Mbunge wa jimbo la Kigamboni Mhe. Faustine Ndungulile.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison mwakyembe akielezea jambo wakati alipotembelea Mahakama ya Mwanzo ya Kigamboni ili kukagua ujenzi wa
Mahakama hiyo jana jijini Dar es salaam mwenye shati la kijani ni Mbunge wa Kigamboni Mhe. Faustine Ndungulile.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni