Pichani ni Muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya-Kibaha, jengo hili lilijengwa kwa kutumia teknolojia ya MOLADI TANZANIA.
Mahakama ya Hakimu
Mkazi na Wilaya Kibaha mkoani Pwani imeanza rasmi kufanya shughuli zake katika
jengo jipya lililopo barabara ya Magereza eneo la Mkoani, Kibaha-Pwani.
Mwandishi wa habari hii ameshuhudia shughuli za Kimahakama zikiendelea katika jengo hilo jipya lililopo barabara ya Magereza eneo la mkoani, Kibaha-Pwani.
Akizungumza na
Mwandishi wa habari hizi Hakimu Mkazi Mfwaidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-
Pwani, Mhe. Elizabeth Nyembele ameipongeza Serikali na Mahakama kwa ujumla kwa
kufanikisha ujenzi wa jengo hilo ambalo limekuwa ni msaada mkubwa kwa Mahakama.
“Jengo hili ni kubwa na
la kisasa zaidi, tunafurahi sana kuwepo katika jengo hili” alisema Mhe.
Elizabeth Nyembele.
Vilevile amewaomba
wananchi wanaotaka kupata huduma za Kimahakama kufika katika jengo hilo jipya
ili kupata huduma hizo kwani limeshaanza kufanya kazi.
Nae Kaimu Mtendaji wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi- Pwani, Bi. Stumai Hozza ametoa pongezi zake kwa
Serikali na uongozi wa Mahakama kwa ujumla kwa kufanikisha ujenzi wa jengo
hilo.
“Tunaiomba Serikali
iwafikirie na mikoa mingine ili nao waweze kupatiwa jengo kubwa na zuri kama
hili,” alisema Bi. Stumai Hozza.
Jengo hili la Mahakama
ya Hakimu Mkazi na Wilaya Kibaha na Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama pamoja na Mpango Mkakati wa miaka mitano wa
Mahakama ya Tanzania, vilizinduliwa rasmi na Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, Septemba, 21, 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni