Na
Mary Gwera,
Mahakama
ya Tanzania
KAIMU Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma amewataka wananchi wote nchini kutembelea
katika Maonyesho ya Wiki ya Sheria 2017, ili kuwawezesha kupata utatuzi na
uelewa zaidi juu ya masuala mbalimbali ya kisheria.
Alisema hayo mapema leo
Januari 26, 2017 katika Ukumbi wa Maktaba, Mahakama ya Rufani (T), Dar es Salaam alipokuwa akiongea
na Waandishi wa Habari juu ya kuanza rasmi kwa Maonyesho ya Wiki ya Sheria nchini
yatakayoanza rasmi Januari 28, 2017 hadi Februari 01, 2017.
Alisema kuwa Maonyesho
haya yatafunguliwa rasmi Februari, 29 mwaka huu kwa matembezi maalum
yatakayoongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi
na kuongeza kuwa kilele cha wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini
kitahitimishwa Februari 02, ambapo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli atakuwa Mgeni Rasmi.
“Kama sehemu ya
Maadhimisho hayo, Mahakama ya Tanzania itatoa elimu ya Sheria, elimu hii
itatolewa sehemu mbalimbali nchini kote ambapo watakuwepo Wataalam wa Sheria wakiwa
tayari kuwahudumia wananchi,” alisema Mhe. Kaimu Jaji Mkuu.
Aliongeza kuwa katika
kufanikisha maadhimisho haya, Mahakama kama mwenyeji wa shughuli hii itakuwa
ndio Mratibu Mkuu wa kuhakikisha kuwa lengo na madhumuni ya kuanzisha elimu ya
sheria yanafanikiwa ipasavyo, kwa kuwashirikisha wadau wengi wanaojihusisha na
masuala ya Sheria.
Aliwataja wadau hao
kuwa ni Mahakama yenyewe kama mwenyeji, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama Kuu Zanzibar, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Mahakama (AGC), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),
Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo cha Uongozi wa Mahakama IJA, Mkuu wa Kitivo cha
Sheria, Chuo Kikuu Huria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Wengine ni Tume ya
Kurekebisha Sheria , Taasisi zinazotoa msaada wa Kisheria (Legal Aid), TAKUKURU
(PCCB), Polisi, Magereza, Msajili, Mabaraza ya Ardhi, TLS, Tume ya Kurekebisha
Sheria, RITA, TAWJA, TAWLA, Sekretarieti ya Msaada wa Sheria, Tume ya
Ususluhishi na Uamuzi (CMA), `Tanzania Network of Legal Aid Provider (TANLAP)`,
Legal Aid and Human Centre na NHIF.
Kwa upande wake, Jaji
Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali alisema kuwa lengo
kuu la Maonyesho hayo ni kujenga zaidi imani ya wananchi na wadau juu ya
Mahakama.
“Maonyesho ambayo lengo
lake kuu ni kurejesha imani ya wananchi dhidi ya Mahakama ambayo ni nguzo
mojawapo katika Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania, hivyo
basi hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango huo,” alisisitiza Mhe. Wambali.
Mhe. Jaji Kiongozi
aliongeza kuwa katika maonyesho hayo wananchi watapatiwa pia elimu juu ya
utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR).
Naye, Msajili Mkuu,
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati alizitaja huduma zitakazotolewa
kuwa ni pamoja na Taratibu za ufunguaji mashauri katika ngazi mbalimbali za
Mahakama, kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Rufaa.
Huduma nyingine ni
Taratibu za Kesi za Mirathi, taratibu za dhamana, Taratibu za Rufaa, ndoa na
talaka, Taratibu za kupokea na kushughulikia malalamiko na Msaada wa Kisheria
(Legal Aid).
Mahakama ya Tanzania
huadhimisha Siku ya Sheria nchini kila mwaka ambayo inaashiria mwanzo wa
shughuli za Mahakama kwa mwaka husika, maudhui ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria
na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha
Ukuaji wa Uchumi.’
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Jaji
Ibrahim Juma (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) leo kuhusu
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yatakayoanza
Januari 28, mwaka huu yanayoashiria kuanza kwa Mwaka wa Mpya wa Shughuli za Mahakama yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja
jijini Dar es Salaam. Maadhimisho
hayo yatazinduliwa Januari 29, mwaka huu kwa matembezi ya hiari
na kilele chake kitakuwa
Januari 2,mwaka huu. Kushoto ni Jaji Kiongozi, Mhe. Ferdinand Wambali na
(kulia) ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni