Jumanne, 3 Januari 2017

WASAIDIZI WA KUMBUKUMBU & MAAFISA TEHAMA WA MAHAKAMA YA TANZANIA WAPEWA MAFUNZO YA UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU KWA NJIA ZA KISASA/KIELETRONIKI

Na, Mary Gwera, Mahakama- LUSHOTO

Mahakama ya Tanzania inakusudia kuendelea kuboresha utunzaji kumbukumbu kwa njia ya kiielektroniki ili kurahisisha huduma ya utoaji haki nchini.

Hayo yalisemwa mapema leo na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto (IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa akifungua mafunzo ya Utunzaji wa Kumbukumbu kwa njia za Kisasa “Training on Modern Record Keeping and Document Management” yanayoshirikisha Wasaidizi wa Kumbukumbu/Makarani kutoka Mahakama mbalimbali nchini pamoja na Maafisa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uelewa zaidi juu ya utunzaji sahihi wa kumbukumbu za Kimahakama ikiwemo kutumia njia za Kiielektroniki (TEHAMA) ili kurahisisha uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama na hatimaye kufikia lengo la uboreshaji wa huduma ya utoaji haki kwa wananchi na umma kwa ujumla” alisema Mkuu huyo wa Chuo.

Aliongeza kuwa katika Mafunzo hayo ambayo yameshirikisha kada mbili tofauti ya Wasaidizi wa Kumbukumbu na Maafisa TEHAMA, ni kuwawezesha kuwa kitu kimoja kwakuwa wao ndio watakaotengeneza na kutumia mifumo hiyo. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi-Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu alisema mafunzo haya ambayo yameshirikisha jumla ya Washiriki 51 yanalenga katika kuwajengea uwezo juu ya utunzaji wa kisasa wa kumbukumbu.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yameshirikisha Washiriki kutoka Makao Makuu Dar es Salaam, Arusha, Manyara, Bukoba, Divisheni zote za Mahakama Kuu ambazo ni Divisheni ya Biashara, Kazi, Ardhi na Divisheni ya Makosa ya Rushwa na  Uhujumu Uchumi, Kibaha, Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Songwe, Sumbawanga, Shinyanga na Simiyu.

Aidha; Bi. Ngungulu alisema kuwa, baada ya mafunzo hayo ya siku 10 yanayofanyika chini ya ufadhili wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Kimahakama chini ya Benki ya Dunia ‘WB’ wanatarajia kuona wahitimu hao wanaboresha utunzaji sahihi wa kumbukumbu katika maeneo yao ya kazi na pia kutoa ujuzi kwa wale ambao hawakushiriki ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Mafunzo haya ni muendelezo wa mafunzo kwa Wasaidizi wa kumbukumbu (RMAs) yaliyokwishafanyika mkoani Dodoma chini ya Mradi wa Mapambano dhidi ya Rushwa ‘STACA,’ ambapo kwa sasa mafunzo haya yatatilia mkazo juu ya utunzaji wa kisasa wa nyaraka na kumbukumbu za Mahakama ikiwemo matumizi ya vitendo vya kutumia mfumo wa Kielektroniki katika kutunza na kushughulikia kumbukumbu hizo kwa ujumla.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-IJA-Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo akifungua rasmi Mafunzo ya Utunzaji wa Kumbukumbu kwa njia za kisasa “Training on Modern Record Keeping and Document Management” yanayoshirikisha Wasaidizi wa Kumbukumbu na Maafisa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania. Kulia ni Mkurugenzi wa Utawala, Bw. Edward Nkembo.

Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo wakimsikiliza Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-IJA- Lushoto alipokuwa akifungua mafunzo hayo ya siku yanayofanyika katika chuo hicho kilichopo mkoani Tanga.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Mhe. Jaji. Dkt. Paul Kihwelo, (wa pili     kulia), Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania, Bw. Edward Nkembo (wa pili kushoto), Mkurugenzi-Msaidizi-Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, wa kwanza kushoto na Mratibu wa Mafunzo ya Mahakama toka  Chuo cha Uongozi wa Mahakama-IJA, Bw. Lameck Samson (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa TEHAMA na Wasaidizi wa Kumbukumbu wanaoshiriki katika mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu- Mahakama ya Tanzania, Bw. Edward   Nkembo akieleza jambo kwa washiriki wa Mafunzo.
   Baadhi ya washiriki wa Mafunzo




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni