Na Lydia Churi- Mahakama, Bukoba
Jaji Mfawidhi-Mahakama kuu kanda ya Bukoba
Mheshimiwa Salvatory Bongole amewataka watumishi wa Kanda yake kuwa na utu na
kutokupenda vitu ili waweze kuepukana na tamaa itakayowafanya waingie kwenye
vitendo vya rushwa.
Akizungumza
jana alipokuwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Jaji Bongole
alisema Kanda yake inaendelea na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano
wa Mahakama ya Tanzania kwa kuhakikisha vitendo vya rushwa vinabaki kuwa
historia katika kanda ya Bukoba ili wananchi wapate haki na kwa wakati.
“Rushwa
inaweza kuwepo kwa baadhi lakini si tatizo kubwa kwa Kanda ya Bukoba ila wakati
mwingine inaweza kuwa ni mitazamo ya watu kuwa Mahakimu na watumishi wengine wa
Mahakama wanakula rushwa”, alisema Jaji Bongole.
Jaji
Mfawidhi huyo alisema mara kwa mara amekuwa akikutana na Mahakimu pamoja na
watumishi wengine wa Mahakama na kuwakumbusha kufuata maadili ya kazi zao kwa
kutojishirikisha na vitendo vya rushwa.
Ametoa
wito kwa watumishi wote wa Mahakama ya Bukoba kuridhika na wanachopata na
kuacha tamaa kwa kuwa ndizo zinazosababisha rushwa. “Ukiwa na utu hutakula
rushwa, rushwa inaletwa na tamaa ya vitu”, alisisitiza.
Wakati
huo huo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Karagwe na Kyerwa
Mheshimiwa Magolyo Faustine Paul alisema Mahakama zake zinajitahidi
kuwashughulikia wananchi wanapofika Mahakamani
ili kuendelea kujenga imani yao kwa chombo hiki muhimu.
Akizungumzia
mabango na matangazo yaliyosambazwa na Mahakama ya Tanzania ya kupambana na
vitendo vya rushwa, Hakimu huyo Mkazi alisema yamesaidia kwa kiasi kikubwa
kupunguza idadi ya malalamiko yaliyokuwa yakiletwa na wananchi kwenye dawati la
malalamiko.
Alisema
hivi sasa idadi ya malalamiko imepungua kutoka 5 hadi 6 yaliyokuwa yakiletwa
kwa mwezi kabla ya kusambazwa kwa mabango, na mpaka kufikia malalamiko 2 hadi 3
kwa mwezi baada ya kusambazwa kwa mabango hayo.
Katika
mwendelezo wa mapambano dhidi ya Rushwa, Mahakama ya Tanzania kupitia Mradi wa
Kupambana na Rushwa ndani ya Mahakama (STACA) ilisambaza vifaa mbalimbali kwa lengo
la kupambana na rushwa yakiwemo mabango yenye jumbe mbalimbali zenye kukemea
vitendo vya rushwa na vitendo vinavyohusiana na ukiukwaji wa maadili, simu za
mkononi kwa ajili ya kupokea malalamiko mbalimbali, Vifaa vya kufanyia kazi
kama Kompyuta, Vinakilishi (Photocopy machines) n.k
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni