Na
Nurdin Ndimbe
Mahakama
Kuu, Kanda ya Mtwara imefanikiwa kwa asilimia 86 kumaliza kesi zote zenye umri
unaozidi miaka miwili Mahakamani katika Kanda hiyo.
Akizungumza hivi karibuni Mjini
Mtwara Naibu Msajili-Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe.Hussein Mushi alisema kuwa
Kanda ya Mtwara ilianza zoezi la usikilizwaji wa mashauri ya zamani mapema kabla ya mpango huu
maalumu wa kumaliza mlundikano wa mashauri.
Naibu
Msajili Mahakama Kuu kanda ya Mtwara Mhe. Hussein Mushi akiwa ofisini kwake.
Zoezi la uondoshaji mashauri nchini
ulianza rasmi katika kanda zote Aprili 24, mwaka huu. “Kwa upande wetu zoezi la
kumaliza mlundikano wa mashauri kwa Kanda yetu tulianza mapema kabla ya mpango
huu mkubwa , Machi 7 mwaka huu tayari tulikuwa na kesi 15 zilizokuwa zimepangwa
kusikilizwa’’ alisema Bw.Mushi.
Kati ya kesi hizo kesi 7 zilizobaki
zilingizwa kwenye mpango Maalum ya kumaliza mashauri ya zamani ambapo kesi 3
tayari zilikuwa zimeisha mpaka tarehe Mei, 23. “Kwa ujumla mashauri yote yaliyofunguliwa
katika Kanda ya Mtwara yalikuwa 32 ambayo ni ya jinai, madai pamoja na ardhi” alisisitiza
Naibu Msajili huyo.
Ukilinganisha yale tuliyoanza nayo pamoja na nyongeza ya mpango maaalum ‘Backlog
Clearance’ utaona tuna wastani
wa 86% ya umalizaji wa mashauri kwa kanda yetu na nakuhakikishia kwa upande wa jinai
na madai tutaendelea nayo kwa pamoja mpaka tutamaliza kama sio yote kabla ya
Mwezi wa Sita kwa kesi zote zenye umri wa miaka miwili’’ alisisitiza Bw.Mushi.
Hata hivyo alisema kuwa, changamoto
kubwa kwa kesi za jinai katika kanda ya Mtwara ni kwa upande wa mashtaka kukata
rufaa na kuzifanyia matangazo ili ziendelee. “Jumla ya kesi zilizokatiwa rufaa
ni 23 hadi kufikia Mei 2017 kati ya hizo 13 ni zamani kuanzia Mwaka 2013 kesi
1, 2014 kesi 3 na 2015 kesi 9” alifafanua.
Kuhusu upatikanaji wa nakala za
hukumu, Naibu Msajili huyo alisema licha ya changamoto zilizopo katika Mkoa wa
Mtwara, na Kanda yake kwa ujumla imekuwa ikitoa nakala za hukumu pamoja na
mienendo ya kesi kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa idadi ya Wahe.Majaji
pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi, lakini kwa Mhakama za Wilaya bado kuna
matatizo ya uhaba wa Mahakimu kwani kwa ujumla kanda ina Mahakimu Wakazi 24 tu
ukilinganisha na mahitaji.
Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni
kwa wananchi kujichukulia sheria mkononi kwani ikumbukwe wakati wa mchakato wa
ujenzi wa bomba la mafuta toka Mtwara hadi Dar Es Salaam Mahakama mbili za
Mikindani na Mtwara Mjini zilichomwa moto na wananchi wenye hasira kali.
Aidha changamoto nyingine ni uhaba
wa majengo ya Mahakama kwani hata Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara inatumia
jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mtwara.
Akizungumzia kuhusu mlundikano wa
Mashauri kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi/Mkoa Mtwara, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama hiyo Mhe.Elizabeth Missana alisema kuwa,katika Mkoa huo mlundikano wa
kesi sio mkubwa, hivyo wao kwa mwaka mzima kesi zilizo na zaidi wa miezi 12 ni
kesi 10 tu na tayari kesi 6 zilishatolewa maamuzi na kubaki kesi nne (4).
“Kwa ujumla kuanzia Januari hadi
Aprili 2017, jumla ya mashauri 511 yalifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi/Mkoa Mtwara na 454 yalimalizika hii ni sawa na wastani wa 75.6% ya
mashauri yote yaliyofunguliwa” alieleza Mhe. Missana.
Mhe.Missana. aliongeza kuwa; kwa mwaka 2016,
jumla ya mashauri 1397 yalifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa, hivyo
wastani wa umalizwaji wa mashauri kwa mkoa huo ni 99.5% nje ya mpango huu
maluum wa umalizwaji wa mashauri ya zamani ambapo kuna kesi 3 bado hazijatolewa
maamuzi. Mahakama ya Mkoa wa Mtwara ina jumla ya wafanyakazi 164 wa kada mbalimbali ikiwemo
Mahakimu 24.
Mahakama ya Tanzania ipo
katika maboresho ya maeneo kadhaa mojawapo ikiwa ni kuboresha huduma ya utoaji
haki nchini ili wananchi waweze kuufanya Mhimili huu kama kimbilio la
upatikanaji wa haki.
Katika kuhakikisha kuwa
Mahakama inafikia malengo yake, hivi sasa Mhimili huu upo katika utekelezaji wa
Mpango Mkakati wake ambao kwa ujumla umejikita katika kuboresha huduma
zitolewazo na Mahakama kwa ujumla hususani suala ya utoaji haki ambalo ndio
Jukumu muhimu linalosimamiwa na Chombo hiki.
Kwa minajili hiyo, Kanda
ya Mtwara ni moja ya Kanda 14 za Mahakama Kuu, na ngazi nyingine za Mahakama
nchini ambayo inatekeleza agizo lililotolewa na Makao Makuu- Mahakama la
kuhakikisha kuwa zinamaliza mlundikano wa mashauri Mahakamani na tatizo la
msongamano wa kesi kuwa historia katika Mahakama zetu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni