Alhamisi, 1 Juni 2017

MAHAKAMA KUU KANDA YA MTWARA KUMALIZA MASHAURI YA MUDA MREFU JULAI



Na Lydia Churi
MAHAKAMA Kuu kanda ya Mtwara imejiwekea malengo ya kumaliza mlundikano wa kesi ifikapo Julai, mwaka huu.

Akitoa taarifa ya Kanda kwa Jaji Kiongozi- Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali, Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu-Kanda ya Mtwara Mhe. Fauz Twaib amesema mpaka kufikia mwezi Aprili, Kanda yake ilikuwa na jumla ya kesi 370 zilizobaki Mahakamani.

Akifafanua, Jaji Twaib alisema jumla ya kesi 116 zilisajiliwa kati ya mwezi Januari na Aprili mwaka huu na kesi 117 zilisikilizwa na kumalizika. Kesi 371 ni zile zilizobaki Desemba, 2016.

Aidha; kati ya kesi hizo, kesi 288 ni zile zenye umri wa miaka miwili na pungufu mahakamani, kesi 82 zina umri wa miaka mitatu (3) mpaka nne (4) Mahakamani wakati hakuna kesi iliyozidi miaka mitano (5) Mahakamani.

Amesema Kanda yake ni miongoni mwa Kanda zilizopatiwa fedha za kuendesha vikao vya kumaliza mlundikano wa kesihivyo wamefanya vikao viwili (2) Mtwara na Lindi.
Jaji Mfawidhi huyo amesema kikao cha Mtwara kimepangiwa kusikiliza kesi 32 za madai na ardhi wakati kikao cha Lindi kinasikiliza kesi nyingine tisa (9) na vikao hivi vitamalizika Juni 9, mwaka huu.

Jaji Kiongozi-Mahakama Kuu ya Tanzania yuko kwenye ziara ya kukagua shughuli za Mahakama na kusisitiza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda ya Mtwara inayojumuisha Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni