Jumapili, 28 Mei 2017

MAHAKAMA YASHAURIWA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI


Na Lydia Churi-Mahakama, Songea
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Luckness Amlima ameishauri Mahakama ya Tanzania kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mhimili huo ili wananchi waufahamu vizuri na kuondokana na dhana kuwa mahakama imekuwa ikichelewesha kumalizika kwa kesi.

Akimkaribisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali wilayani kwake, Mkuu huyo wa wilaya alisema wananchi wengi hawana uelewa mpana wa sheria pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama hivyo wamekuwa wakiilalamikia Mahakama  kuchelewesha kesi.
Alisema kuchelewa kumalizika kwa kesi kwenye Mahakama mbalimbali kumesababisha kujengeka kwa dhana kuwa Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Mahakama hutaka kupewa rushwa ili kumaliza kesi.
Aidha, bibi Amlima alisema kuwa ni wakati sasa kwa Mahakama  kutoa elimu kwa jamii pamoja na viongozi mbalimbali ambao wamekuwa wakiwaelimisha wananchi kuwa kumalizika haraka kwa kesi ni matokeo ya ushirikiano baina ya wadau wote wa mahakama katika kuwapatia wananchi haki zao.
Baadhi ya wadau wa Mahakama ni pamoja na jeshi la Polisi, Magereza, Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu wa serikali, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na Mawakili. 
Akizungumzia hali halisi ya wilaya yake, Mkuu wilaya ya Namtumbo alisema wilaya yake haina gereza hivyo wafungwa husafirishwa kutoka Songea mjini mpaka Namtumbo kwa ajili ya kusikilizwa kesi zao jambo ambalo limekuwa likisababisha kesi kuchukua muda mrefu kumalizika kutokana na umbali.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa Ferdinand Wambali amesema Mahakama itashirikiana na wadau wake ili kuhakikisha kesi zinamalizika kwa haraka kwenye mahakama mbalimbali nchini.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea katika ziara ya kukagua shughuli za Mahakama pamoja na Kusisitiza Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda ya Songea.

Alisema kupitia nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa mahakama ya Tanzania ambayo inasisitiza kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za mahakama, Mahakama itatoa elimu kwa wananchi pamoja na viongozi wakiwemo wakuu wa wilaya juu ya masuala mbalimbali yanayohusu utoaji wa haki kwa wananchi.
Jaji Kiongozi amesema Mahakama imejiwekea mikakati ya kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati na kwa haraka ukiwemo mkakati wa kesi kutokukaa kwa zaidi ya miaka 2 kwenye  Mahakama Kuu, miezi 12 Mahakama za mikoa na Wilaya pamoja na miezi sita kwenye Mahakam za Mwanzo.
Mikakati mingine ni ile ya kesi kusikilizwa kwa mfululizo na kuwekwa kwa maahirisho mafupi mafupi ya kesi kwenye Mahakama mbalimbali nchini na Majaji na Mahakimu kupangiwa idadi ya kesi watazosikiliza katika kipindi cha mwaka moja. Aidha, kila Jaji amepangiwa kusikiliza na kumaliza kesi 220 kwa mwaka ambapo Mahakimu wamepangiwa kumaliza kesi 250 kwa mwaka.
Akizungumzia Maadili kwa watumishi wa Mahakama, Jaji Wambali amewataka watumishi hao kuwahudumia wananchi wanaofika mahakamani kwa bidii, uaminifu, na uadilifu ili kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama.
Amesema watumishi wa Mahakama hawana budi kufanya kazi kwa upendo na ushirikiano kwa kuwa kazi za mahakama zinategemeana ambapo kila kada ina umuhimu wake katika wananchi kufikia haki zao za msingi.
Jaji Kiongozi yuko kwenye ziara katika kanda za Songea na Mtwara kwa ajili ya kukagua shughuli za kimahakama pamoja na kusisistiza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania. Tayari ametembelea mahakama zilizoko Songea mjini na zile za wilaya za Mbinga, Nyasa, Namtumbo, na Tunduru.     

 Mtendaji wa Mahakama, Samson Mashalla akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yahusuyo Utumishi kwa watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea (hawapo Pichani) wakati wa ziara ya Jaji Kiongozi kwenye kanda hiyo. 
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa wa Ruvuma (hawapo Pichani) alipomtembelea Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Binilith Mahenge ofisini kwake akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za Mahakama pamoja na Kusisitiza Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda ya Songea. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
 
  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea katika ziara ya kukagua shughuli za Mahakama pamoja na Kusisitiza Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda ya Songea.
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Mhe. David Mrango akizungumza na waatumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea(hawapo Pichani) wakati wa Ziara ya Jaji Kiongozi kwenye kanda hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Binilith Mahenge akizungumza na baadhi ya watumishi wa Mahakama walioambatana na Jaji Kiongozi ofisini kwake mjini Songea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni