Jumatatu, 5 Juni 2017

JAJI KIONGOZI AWATAKA WANANCHI KUIAMINI MAHAKAMA

Na Lydia Churi-Lindi
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali amewataka watanzania kuendelea kuwa na Imani na Mahakama kwa kuwa ina mchango mkubwa katika kuleta Amani na kujenga uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua shughuli za mahakama wilayani Nachingwea, Jaji Wambali alisema kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama, hivi sasa kesi zinamalizika kwa haraka mahakamani ili wananchi wapate muda zaidi wa kushiriki shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Alisema Mahakama imejipangia kuwa kesi zote zilizopo Mahakama Kuu zinatakiwa kuwa zimemalizika ndani ya kipindi cha miaka miwili, na katika Mahakama za Mikoa na wilaya kesi zimalizike ndani ya miezi 12 wakati kwenye Mahakama za Mwanzo kesi zisikae kwa zaidi ya miezi sita kabla ya kuwa zimesikilizwa na kumalizika.
 Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Nachingwea pamoja na viongozi wa Mahakama wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati alipotembelea Mahakama hiyo akiwa katika ziara ya kukagua kazi zinavyofanyika pamoja na kusisitiza juu yya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania katika kanda za Songea na Mtwara. 
  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Nachingwea baada ya kuzungumza nao wakati alipoitembelea Mahakama hiyo akiwa katika ziara ya kukagua kazi zinavyofanyika pamoja na kusisitiza juu yya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania katika kanda za Songea na Mtwara.

Akizungumzia Mpango Mkakati wa Mahakama, Jaji Wambali alisema kupitia nguzo yake ya kwanza, mahakama inawajibika katika kuhakikisha inatumia vizuri rasilimali fedha inayopatikana katika kutekeleza malengo iliyojiwekea.   

Alisema katika nguzo ya pili ya mkakati huo, Mahakama imeanza kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi ikiwa ni pamoja na kuboresha taratibu za sheria ili ziwe rafiki na kueleweka vizuri kwa wananchi.

Aidha, Jaji Kiongozi alisema katika nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati huo, Mahakama inakusudia kuendelea kujenga taswira bora kwa wananchi. Alisema taswira bora itajengwa kwa watumishi wa mahakama kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya haki nchini.     

Akizungumzia Maadili kwa watumishi wa Mahakama, Jaji Kiongozi aliwataka watumishi wote wa Mahakama wilayani humo kuwajibika ipasavyo katika kuwahudumia wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki zao. “Mahakama haiwezi kuwajibika endapo watumishi wake hawatawajibika, hivyo ni vizuri mkazingatia maadili ya kazi katika kuwahudumia wananchi wanaofika Mahakamani”, alisema Jaji Wambali.   

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi akimkaribisha Jaji Kiongozi ofisini kwake alisema Mahakama na Serikali ni wamoja katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania hivyo ili nchi iende vizuri ni muhimu kwa kila mhimili kutimiza wajibu wake kwa wananchi.

Aliishauri Mahakama kuwakutanisha wakuu wa mikoa pamoja na wa wilaya na kuwapa mafunzo yatakayowajengea uwezo kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ili hatimaye kama serikali wawe ni kitu kimoja katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Jaji Kiongozi amemaliza ziara yake katika kanda za Songea na Mtwara za Mahakama Kuu ya Tanzania. Alikuwa akikagua shughuli za Mahakama pamoja na kusisitiza juu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi  wakati alipoitembelea Mahakama hiyo akiwa katika ziara ya kukagua kazi zinavyofanyika pamoja na kusisitiza juu yya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania katika kanda za Songea na Mtwara. 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi  wakati alipoitembelea Mahakama hiyo akiwa katika ziara kwenye kanda ya Mtwara.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni