JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
Simu Na: +255 (026) 2963630 Menejimenti ya Utumishi wa Umma
Nukushi: +255 (026) 2963629 na Utawala Bora,
Barua Pepe: ps@utumishi.go.tz Jengo la Taaluma Na. 1,
Tovuti: http://www.utumishi.go.tz Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
Barabara ya Mkalama,
S.L.P. 670, 40404 DODOMA.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2017
1.0 Utangulizi
Ndugu Wanahabari, maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yatafanyika kuanzia tarehe 14 Juni mpaka 23 Juni, 2017. Maadhimisho haya husherehekewa kila mwaka na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya Nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.
Chimbuko la maadhimisho haya ni uamuzi wa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma uliofanyika Tangiers, Nchini Morocco Mwaka 1994. Uamuzi huu ulizitaka Nchi za Afrika kusherehekea siku hii kwa Kauli Mbiu moja kwa Bara zima la Afrika.
Hapa nchini, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora huratibu maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
2
2.0 Kauli Mbiu ya Maadhimisho kwa mwaka 2017
Kauli Mbiu itakayotumika na Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) katika maadhimisho haya ni:
"Kuimarisha Ushirikishwaji wa Jamii katika Utoaji Huduma: Vijana Washirikishwe kuleta Mabadiliko Barani Afrika".
3.0 Utaratibu wa Maadhimisho kwa Mwaka 2017
Ofisi ya Rais-UTUMISHI imekuwa na utaratibu wa kuendesha Makongamano na Maonesho kuhusu kazi na majukumu mbalimbali yaliyofanikishwa na Utumishi wa Umma wakati wa Wiki ya Utumishi wa Umma tangu Mwaka 2003. Sanjari na hilo, Tuzo zilikuwa zikitolewa kwa Taasisi zilizofanya ubunifu katika kutoa huduma kwa wananchi. Hata hivyo, katika mwaka 2016 Serikali ilitumia Wiki hiyo kwa Viongozi na Maofisa wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutembelea waajiri pamoja na kuzungumza na wadau wa ndani (Watumishi wa Umma) kwa ajili ya kupokea maoni, ushauri na malalamiko kuhusu utendaji na/au utoaji wa huduma wa taasisi za Serikali na Watumishi wa Umma kwa ujumla. Hatua hii ilisaidia Serikali kupata mrejesho wa mambo mbalimbali, kutathmini utendaji wake pamoja na kutatua baadhi ya kero na changamoto zilizobainishwa.
Kwa Mwaka huu wa 2017, Serikali imepanga kutumia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kukutana na waajiri katika Utumishi wa Umma kwa ajili kupata mrejesho wa utekelezaji wa mambo mbalimbali yaliyotokana na Wiki ya Utumishi wa Umma Mwaka 2016 pamoja na kufanya mambo yafuatayo:
3.1. Kutoa mafunzo kwa Maafisa Utumishi wa Serikali kuhusu namna ya kufanya zoezi la uhakiki wa Watumishi kwa kutumia taarifa za Utambulisho wa Taifa na kusimamia zoezi hilo ambalo litatekelezwa na maofisa Utumishi/ Tawala
3
watakaopewa mafunzo wakati wa wiki hii. Zoezi hili litaongeza usahihi wa taarifa za watumishi nchini, kudhibiti watumishi hewa, udanganyifu wa taarifa mbalimbali zinazomhusu mtumishi, na kutekeleza azma ya Serikali ya kuunganisha mifumo ya TEHAMA ili ibadilishane taarifa;
3.2. Hatua zinazoendelea za kugatua Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara Serikalini (HCMIS) hadi sehemu za kutolea huduma (Service Delivery Points) na utayari wa Waajiri katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuutumia Mfumo huo zitaangaliwa. Hivyo, Watendaji wa Ofisi ya Rais-Utumishi wataangalia kiwango cha utekelezaji wa mpango huo katika Idara za Elimu na Afya. Mafunzo yalikwishatolewa kwa Maafisa Elimu na Makatibu wa Afya wapatao 633 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu namna ya kutumia Mfumo;
3.3. Serikali kutumia wiki hii kuwasisitizia Watumishi wa Umma kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kuwahudumia Wananchi wetu ambao ndio wadau wakuu wa huduma zitolewazo na Serikali;
3.4. Usahihishaji wa taarifa za Kiutumishi na malipo ya Mshahara kwa Watumishi wa Umma kwa kuzingatia ukweli kwamba baadhi ya Taasisi za Umma bado zina watumishi wenye taarifa chafu. Mfano wa taarifa hizo ni pamoja na tarehe za kuzaliwa, tarehe za ajira, tarehe za kupandishwa vyeo, taarifa za Mifuko ya hifadhi ya Jamii, Vyeo walivyonavyo Watumishi husika, n.k.
3.5. Kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya kuwaondoa Watumishi wasiostahili kwenye Orodha ya Malipo ya Mshahara (Payroll) ya Watumishi wa Umma pamoja na urejeshwaji wa wale walioondolewa kimakosa kwa mujibu wa
4
maelekezo yaliyokwishatolewa na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;
3.6. Kukumbusha Waajiri kuhusu taratibu mbalimbali za usimamizi na uendelezaji wa rasilimali katika Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa za Serikali, mafunzo kwa watumishi, matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS), Tovuti ya Watumishi (Watumishi Portal) na juhudi mbalimbali za kuboresha utendaji kazi Serikalini; na
3.7. Kubadilishana uzoefu kati ya waajiri na maofisa kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika eneo la usimamizi na uendelezaji wa rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.
4.0 Malengo ya Siku ya Utumishi wa Umma
Kama nilivyokwishaeleza awali, Wiki ya Utumishi wa Umma Barani Afrika itaanza rasmi tarehe 14 Juni na kufikia kilele tarehe 23 Juni 2017. Malengo ya msingi ya wiki hii ni:
4.1. Kutambua mchango na umuhimu wa Watumishi wa Umma katika kuleta maendeleo katika Nyanja mbalimbali za maendeleo katika Nchi;
4.2. Kuwezesha Watumishi wa Umma kutambua Dira, Dhima, na Malengo; Programu na Mikakati; na Mafanikio na Changamoto zinazokabili Utumishi wa Umma;
5
4.3. Kuhamasisha na kuwapa motisha Watumishi wa Umma waendelee na kazi yao nzuri ya ujenzi wa Taifa na kuendelea kuwa wabunifu ili kutatua changamoto mbalimbali katika jamii;
4.4. Kupata mrejesho kutoka kwa wateja/wananchi na wadau wanaowahudumia; na
4.5. Kuandaa Utumishi wa Umma ili uweze kukabiliana na changamoto mbalimbali ili uweze kuleta maendeleo kwa siku zijazo.
5.0 Faida za Siku ya Utumishi wa Umma
5.1 Wananchi kupata fursa ya kufahamu wajibu na haki zao ili pale ambapo wanazikosa waweze kujua namna ya kuzipata;
5.2 Taasisi za Umma kupata fursa ya kubadilishana uzoefu juu ya mbinu na mikakati mipya ya namna ya kutoa huduma bora kwa Umma;
5.3 Taasisi za Umma kupata fursa ya kuonyesha ubunifu waliofanya katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma na kuondoa urasimu usiokuwa na lazima katika michakato mbalimbali ya utoaji huduma;
5.4 Taasisi za Umma kupata fursa ya kupokea ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo Wananchi, Asasi za Kiraia (AZAKI), na Sekta Binafsi juu ya namna bora ya kuboresha utoaji huduma;
5.5 Taasisi za Umma kupata mrejesho na kuutumia mrejesho huo kurekebisha kasoro za utendaji zinazosababisha malalamiko ya wateja ili huduma za Serikali ziboreshwe kufikia matarajio ya Wananchi.
6
6.0 Kwa kuzingatia Kauli Mbiu ya maadhimisho, iliyobainisha umuhimu wa kuimarisha ushirikishwaji katika kutoa huduma kwa Umma ili kuleta mabadiliko, nawakumbusha Watendaji wa Serikali kukutana na watumishi katika maeneo yao kupokea mrejesho kuhusu changamoto mbalimbali na maoni kuhusu utendaji kazi na kupanga siku za kukutana na wadau wa nje na ndani wa Taasisi. Aidha, Taasisi za umma zitumie kipindi hiki kutambulisha huduma mpya kwa wadau na Wananchi, na kupokea mrejesho kutoka kwao, kwani wao ndio watumiaji na wadau wakuu wa Serikali.
7.0 HITIMISHO
Napenda kusisitiza sisi Watumishi wa Umma, kila mtu akitimiza wajibu wake mahali alipo tutaondoa kero kwa Watumishi na jamii kwa ujumla.
Nawatakia nyote maadhimisho mema ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Angellah J. Kairuki (MB.)
WAZIRI WA NCHI - OFISI YA RAIS
(MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA)
13 Juni, 2017
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni