Jumatano, 14 Juni 2017


            JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 MAHAKAMA

TAARIFA KWA UMMA


1.   Utangulizi                                                                                                                        
Katika gazeti la Raia Mwema Toleo Na.513 Jumatano, Juni 7 – Juni 13, 2017 katika ukurasa wa kumi (10) iliandikwa habari (Makala) yenye kichwa cha habari Majaji: Tuchague idadi au Ubora”. Katika Makala hiyo Mwandishi anaelezea taarifa ya utafiti anaofanya kuhusu Mahakama katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Mwandishi ameainisha mambo kadhaa yanayotokana na utafiti huo ambayo majaji kuchangia vyumba vya ofisi, Uteuzi wa Majaji kutoka nje ya Mahakama ambao hauna tija na kutokuwepo tena kwa umuhimu wa kuteua Majaji.

Mahakama ya Tanzanaia inapenda kuufahamisha Umma kuwa habari katika makala hii si za kweli na ni za upotoshaji. Kufuatia upotoshaji huo, Mahakama ya Tanzania inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao;-
2. Majaji wa Mahakama Kuu kuchangia Ofisi

Siyo kweli kuwa Majaji wa Mahakama Kuu huchangia ofisi wakati wakitekeleza majukumu yao. Aidha, Jedwali hapa chini linaonyesha mtawanyiko wa vyumba vya Majaji kwa kila Kanda.

S/NO
KANDA
IDADI YA VYUMBA
IDADI YA
MAJAJI
UPUNGUFU WA NYUMBA
ZIADA YA VYUMBA
1.
MASJALA KUU NA KANDA YA DSM
18
12
0
4
2.
DIVISHENI YA ARDHI
10
5
0
5
3.
DIVISHENI YA BIASHARA
4
3
0
1
4.
DIVISHENI YA KAZI
4
3
0
1
5.
DIVISHENI YA U/UCHUMI
4
2
0
2
6.
DIVISHENI YA USULUHISHI
2
1
0
1
7.
TABORA
5
3
0
2
8.
SHINYANGA
4
3
0
1
9.
MWANZA
7
7
0
0
10.
MBEYA
4
3
0
1
11.
DODOMA
4
4
0
0
12.
ARUSHA
5
3
0
2
13.
TANGA
4
3
0
1
14.
IRINGA
3
2
0
1
15.
BUKOBA
3
2
0
1
16.
SONGEA
2
2
0
0
17.
MOSHI
3
3
0
0
18.
SUMBAWANGA
3
0
0
1
19
MTWARA
2
2
0
0
 
JUMLA
91
63
0
24

 Kwa jedwali hili, Mahakama Kuu kuna vyumba 91 na Majaji ni 63 na hivyo kuwepo na vyuma vya ziada 21 ambavyo havina Majaji. Hakuna chumba kinachotumika na Majaji wawili kwa wakati mmoja kwani hakuna sababu hiyo kutokana na uchache wa Majaji uliopo kwa sasa.
3. Uteuzi wa Majaji nje ya Mhimili wa Mahakama

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 109 (6) mtu anaweza kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Jaji kama atakuwa na sifa maalumu ambazo zimeelezwa katika ibara ndogo ya 7 na awe amekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka 10.
Sifa hizo maalumu ni kuwa na digrii ya kwanza ya sheria kutoka katika chuo kikuu kinachotambulika na mamlaka za utambuzi pamoja na:-

(a) kuwa hakimu;

(b) ameshika nafasi katika ofisi yo yote ya umma akiwa kama mwanasheria au wakili wa kujitegemea; na

(c) awe na sifa ya kuweza kusajiliwa kama Wakili kwa kipindi cha miaka isiyopungua kumi.
Kwa mujibu wa ibara hii, siyo Mahakimu peke yao wenye sifa ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo mamlaka ya kuteua mtu mwenye sifa kuwa Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania hata kama anatoka nje ya Mhimili wa Mahakama.

Hivyo kusema Majaji ni lazima wateuliwe kutokana na Watumishi walio ndani ya Mahakama pekee ni kuwapotosha watanzania na haina mantiki yoyote.
4. Ushawishi

Mahakama ya Tanzania inapenda kuueleza umma wa watanzania kuwa hakuna mazingira yanayovutia ushawishi kutoka kwa Jaji mmoja kwenda kwa Jaji mwingine kwani hofu ya ushirikiano wa chumba aliokuwa nayo mlalamikaji haipo. Majaji wanafanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na Jaji mwenzao
 5. Umuhimu wa kuendelea kuteua Majaji

Mwandishi wa makala hii amehoji kama bado ni muhimu kuendelea kuteua Majaji akimaanisha kuwa mahitaji hayo yalikuwepo tu kipindi ambacho mlundikano ulikuwa mkubwa. Mahakama inatoa ufafanuzi kuwa, mahitaji ya Majaji bado ni makubwa. Kwa tathmini ya utendaji wa Mahakama iliyofanyika mwishoni mwa mwaka 2016, Mahakama Kuu na Divisheni zake imekuwa na mzigo wa Mashauri 35,878 kwa idadi ya Wastani wa Majaji 75 waliokuwepo kipindi cha 2016. Kwa maana hiyo, kila Jaji alikuwa na mzigo wa Wastani wa mashauri 478. Uwezo wa Jaji kusikiliza kesi unakomea kwenye kesi 198 kwa mwaka. Hivyo Majaji waliopo ni wachache sana na kuna ofisi 24 zipo wazi hazina Majaji. Hoja kwamba ubora wa kazi za Majaji unaathiriwa na ufinyu na uchache wa ofisi haina ukweli wo wote.
6. Ushirikiano kati ya Mahakama na Vyombo vya Habari nchini

Mahakama ya Tanzania inaheshimu na kuthamini uhuru wa vyombo vya habari kama wadau muhimu katika upatikanaji wa taarifa, hivyo, Mahakama itaendelea kushirikiana na vyombo hivi katika kuwapatia wananchi na wadau taarifa sahihi na zenye kutoa taswira iliyo ya kweli kwa Umma wakati wote.  Aidha, Waandishi wa Habari kutoka vyombo vyote vya habari nchini mnaombwa kuendelea kushirikiana na Mahakama katika kujenga taswira chanya kwa muhimili huu wa dola. 
Mahakama inapenda kutoa wito kwa vyombo vyote vya habari nchini kuwasiliana na kitengo chake cha Habari, Elimu na Mawasiliano au Wasajili wa Mahakama  endapo kuna jambo lolote linalohitaji ufafanuzi kwa lengo la kuboresha mazingira ya utoaji haki na utoaji wa habari zilizo sahihi kwa wananchi.
 
IMETOLEWA NA MSAJILI MKUU WA MAHAKAMA YA TANZANIA.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni