Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha wamepongezwa kwa kuendelea kulitunza vizuri jengo jipya walilokabidhiwa hivi karibuni na kulitumia kama chachu ya kuwafanya waongeze juhudi katika utendaji kazi.
Akizungumza na
watumishi hao wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani, Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam Mhe. Lugano Mwandambo alisema ni vizuri
jengo hilo likatunzwa ili lidumu na kuwasaidia wananchi katika kupata haki zao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam Mhe. Lugano Mwandambo akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha alipofanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Pwani.
Katika ziara yake
aliyoambatana na Msajili wa Mahakama hiyo pamoja na Afisa Utumishi, Jaji
Mfawidhi huyo pia alipata nafasi ya kutembelea na kukagua shughuli za Mahakama
katika Mahakama zote za Mwanzo zilizopo kwenye wilaya ya Kibaha.
Jengo la Mahakama ya
Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani na Mahakama ya wilaya ya Kibaha ni miongoni mwa majengo
ya mfano yanayojengwa na Mahakama kwa kutumia teknolojia ya gharama nafuu na ya
muda mfupi ijulikanayo kama Moladi.
Mahakama nyingine za mfano
zinajengwa katika maeneo ya Kinyerezi, Kigamboni, Kawe, Mkuranga, na Bagamoyo.
Majengo haya yanatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Aidha, ujenzi wa majengo
haya unalenga katika kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi na
kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati ambao ndiyo jukumu la msingi la kikatiba
la Mahakama ya Tanzania.
Jengo la Mahakama
lililoko mjini Kibaha lilizinduliwa rasmi Septemba mwaka jana na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akizindua Mpango
Mkakati wa Miaka mitano (2015-2020) wa
Mahakama ya Tanzania pamoja na Maboresho ya Huduma za Mahakama.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na wa Mahakama ya wilaya ya Kibaha wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Lugano Mwandambo(hayupo pichani) akizungumza nao alipofanya ziara mkoa wa Pwani hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni