Na
Mary Gwera, Mahakama, Iringa
Mahakama ya Hakimu Mkazi
Iringa imefanikiwa kuondosha Mashauri/kesi kwa zaidi ya asilimia tisini (90) na
kuifanya Mahakama hiyo kuendana na azma ya Mahakama ya Tanzania ya kutoa haki
kwa wakati ili kuondokana na mlundikano wa mashauri katika Mahakama zake
nchini.
Akizungumza ofisini
kwake katika mahojiano maalum na Mwandishi wa taarifa hii aliyepo Kanda ya
Iringa, mapema Juni 6, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi-Iringa,
Mhe. David Ngunyale alisema hali ya uondoshaji wa Mashauri katika Mkoa wa Iringa
inaridhisha na kufafanua kuwa kwa upande wa Mahakama za Mwanzo ambazo jumla
yake zipo 21, hakuna kesi inayozidi miezi sita (6) katika Mahakama hizo.
Akiongelea katika ngazi
ya Mahakama za Wilaya, Mhe. Ngunyale alisema kuwa Mahakama hizo zina jumla ya
kesi 12 za mlundikano (ambazo zimezidi umri ya miezi 12 Mahakamani), huku kesi 8
zikiwa ni za Jinai na nne (4) zikiwa ni kesi za Madai.
Pichani ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi-Iringa, Mhe. David Ngunyale
Hata hivyo; Mhe.
Ngunyale alidai kuwa kuna sababu kadhaa ambazo zilipelekea kuchelewa kutolewa maamuzi kwa kesi hizi ambazo zipo chini ya asilimia tano (5) ya kesi zilizopo, huku akitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kutopatikana kwa mashahidi kwa wakati, upelelezi
kutokamilika kwa wakati na kadhalika.
“Hata hivyo tunaweza
kusema kuwa suala la umalizwaji wa kesi kwa wakati lipo vizuri kwa Kanda hii,
na tumefanikiwa kwa asilimia 95, na hivyo kwenda sawia na Mpango Mkakati wa
Mahakama wa kuhakikisha kuwa Mahakama zake zinatoa haki kwa wakati,”
alisisitiza Mhe. Ngunyale.
Akiongelea juu ya
upatikanaji wa nakala za hukumu, Mhe. Ngunyale alisema kuwa Wateja hupatiwa
nakala za hukumu ndani ya siku 21 tangu kuamriwa kwa shauri/kesi husika.
Akizungumzia kuhusiana
na Programu maalum ya uondoshaji mlundikano wa Mashauri Mahakamani linalohusisha
mahakama zote nchini, Mhe. huyo alisema kuwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa
ni miongoni mwa Mahakama zilizotekeleza wito huo.
“Mahakama ya Hakimu
Mkazi-Iringa ilianza Programu hii kwa mara ya kwanza Machi, 27 mwaka huu kama
ilivyopangwa na Makao makuu ya Mahakama, na katika awamu hii ya kwanza
iliyokamilika Aprili 30, mwaka huu, tulifanikiwa kumaliza jumla ya mashauri 8
kati ya mashauri 9 yaliyokuwa yamepangwa kusikilizwa katika Programu hiyo,”
alifafanua Hakimu Mkazi huyo.
Kwa upande mwingine
Hakimu huyo Mfawidhi aliongeza kuwa, wamekuwa pia wakifanya kaguzi za mara kwa
mara katika Mahakama za chini za mkoani humo (Mahakama za Wilaya na Mwanzo), lengo
likiwa ni kufuatilia kwa karibu zaidi hali ya utoaji haki katika Mahakama hizo
na endapo kuna madhaifu kuyafanyia kazi ili Mahakama zote katika Mkoa wa Iringa
ziendane na kasi moja ya kumaliza mashauri kwa wakati.
Akizungumzia juu ya
uhifadhi wa kumbukumbu za kesi za miaka ya nyuma na zinazoendelea, Mtendaji wa
Mahakama, Kanda ya Iringa, Bw. Elvin Mwakajinga, alisema kuwa Kanda yake
imefanikiwa katika kuhifadhi kumbukumbu zake za kesi.
“Mafaili ya kumbukumbu za
kesi/mashauri ya miaka ya nyuma na zinazoendelea zimewekwa katika Maboksi
maalum, mafaili hayo ya kumbukumbu za kesi yapo yaliyomalizika kati ya mwaka
1982 na 2005 yamepangwa kulingana na mwaka wa kesi husika kukamilika,”
alifafanua Bw. Mwakajinga.
Afisa Tawala, Mahakama ya Hakimu Mkazi/Mkoa-Iringa, Bi. Dorice Kisanga akionesha maboksi ambapo mafaili ya kesi zilizomalizika yalipohifadhiwa, kwa urahisi wa rejea ya kumbukumbu za kesi za nyuma.
Pichani ni muonekano wa jengo la Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, katika uwanja huu, yapo pia majengo ya Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi-Iringa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni