Jumatano, 7 Juni 2017

MAHAKAMA YA TANZANIA KUANZISHA KITUO MAALUM CHA PAMOJA KUSHUGHULIKIA KESI ZA MIRATHI NA MAMBO YA FAMILIA.


Na   Magreth   Kinabo
Mahakama ya Tanzania,  kupitia  Mpango  Mkakati  wake wa Miaka  Mitano 2015/16  2019 /2020 inatarajia kuanzisha  Kituo  Maalum cha Pamoja  cha  kushughulikia masuala ya mirathi ikiwa  ni hatua  ya   kupanua wigo  wa huduma  kwa watu wenye mahitaji maalum.
Kupitia  Mpango  huo, Mahakama  ya  Tanzania  inaanzisha  kituo hicho  ikiwa   hatua ya kuwapunguzia wananchi gharama za fedha  wanazozitumia na muda wanaoutumia sambamba na utoaji wa haki kwa wakati.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Mkutano wa Mashauriano kuhusu  uanzishaji   wa Kituo  Maalum  cha  kushughulikia masuala ya mirathi, ambaye ni Msajili ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ilvin  Mugeta kwenye ukumbi wa mikutano wa Tume ya Kurekebisha  Sheria,uliopo Jijini Dar es Salaam.
“Tuna  mpango wa kuanzisha  kituo hicho cha  huduma  za  Mahakama   kuhusiana  na masuala  ya mirathi, ambacho  kitakuwa na wadau  mbalimbali wa Mahakama  ya Tanzania ili  kuhakikisha  huduma za mirathi  zinatolewa kwa wakati  bila kupoteza muda  na gharama,” alisema Mwenyekiti huyo.
 

   Baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na wadau wa mkutano huo wakiwa  katika picha ya pamoja .

 

Aidha kituo hicho pia kitawasaidia  kupunguza mlundikano  wa  kesi  zilizo kaa muda mrefu Mahakamani,ikiwa ni moja ya mkakati wa Mahakama wa kupitia mpango huo.

“Katika  Mpango huo Mahakama  inatarajia kujenga  Kituo  Kimoja cha Pamoja kitakachoshughulikia masuala ya mirathi, hivyo huduma  hizo zitakuwa zinapatikana kwenye jengo moja ili kuweza kuwaondolea usumbufu   watu wanaohitaji huduma za Mahakama,” alisema  Mhe. Mugeta.
Mhe . Mugeta   alisema kituo hicho, kitakuwa  na huduma  za  Mahakama  ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya na Mahakama Kuu.   Pia  kitasaidia watu wanaohitaji huduma  hiyo kupatiwa haki zao kwa wakati  na kuwazesha kuendelea  kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kuchangia  kuinua pato la Taifa.

Kituo  hicho cha pamoja,   kinatarajiwa kuanza kufanya kazi mwaka 2019 katika jiji la Dar es Salaam katika wilaya ya Temeke karibu  na kituo cha  polisi Chango’mbe kwenye eneo ilipo, Mahakama  ya Mwanzo  Temeke.

Mhe. Mugeta aliongeza kwamba  kituo hicho, kinajengwa katika jiji hilo, kwa sababu  asilimia 10 ya  Watanzania  wanaishi kwenye eneo hilo.
Alifafanua kwamba  kwa mujibu wa uchunguzi  uliofanywa  na  vyanzo  vya  habari mbalimbali mirathi  na mambo  ya kifamilia, ni maeneo  yamekuwa na changamoto nyingi.

Hali  inayosababisha  kuhitaji mtazamo  wa pekee ili kuongeza  ufanisi na tija katika kushughulikia  kesi  zinazohusiana  na masuala ya mirathi  na mambo  kifamilia.

Mahakama  ya Tanzania  iliandaa  Mkutano  Maalum wa Mashauriano na Wadau  wa Mahakama  ili  kuweza kujadiliana  na kubadilisha uzoefu katika changamoto  zinazojitokeza kila wakati   kwenye   kesi  zinazohusiana na maeneo hayo.  
Akizungumzia kuhusu  changamoto  wanazokabiliana  nazo  katika  kesi  hizo, Mhe. Mugeta  alisema  upatikanaji  wa haki kwa wakati mwingine unakuwa ni mgumu kwa sababu baadhi ya  ndugu au familia  kutowasilisha vilelezo Mahakamani kwa wakati.

Aidha Mhe. Mugeta ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisema kituo hicho, kitaanzishwa  katika jiji hilo kwa  sababu   hilo, limeonekana  kuwa ni  kubwa kwa sababu   lina wakazi wengi.
Aliitaja sababu ya kuanzishwa kituo hicho, kimetokana  kwamba Mahakama ya Tanzania huwa inapokea maoni 3,000 kila siku  kuhusiana na masuala hayo.

“Kituo hicho kitakuwa na huduma za Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Mahakama Kuu, ili kuweza kuondoa vipingamizi  katika utoaji wa huduma hizo.

Mhe. Mugeta alisema  katika kituo hicho,  kinatarajiwa  kuwa  na  huduma za  kibenki  pamoja  na huduma za mafao  kutoka mifuko  ya hifadhi  ya jamii, huduma  za msaada wa kisheria, usajili wa vizazi na vifo  na huduma nyinginezo.
Baadhi ya wadau  wa mkutano huo, walipendekeza kwamba elimu zaidi  itolewe kuhusiana na masuala ya mirathi.

Miongoni  mwa wadau walioshirikishwa katika mpango huo ni  umewashirikisha  baadhi ya viongozi wa Mahakama  ya Tanzania, wakiwemo wadau hao, ambao  ni  Chama  cha Wanasheria Wanawake  Tanzania (TAWJA), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambayo ni Mfuko  wa Taifa  wa Hifadhi  ya Jamii (NSSF), Mfuko  wa Pensheni Mafao  kwa Watumishi  wa Umma  (PSPF), Mamlaka  ya Usimamizi   Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Chama  cha Mawakili Tanganyika(TLS) na Baraza Kuu la Waislaamu Tanzania(BAKWATA).

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni