Na
Mary Gwera, Mahakama, Njombe
JAJI Mfawidhi, Mahakama
Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali ametoa wito kwa Mahakimu na wadau wa
Mahakama nchini kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma ya haki kwa
wananchi.
Aliyasema hayo mapema
Juni 07, alipokuwa akiongea na Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe baada ya
kuhitimisha ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama katika Mahakama za
Mwanzo na Wilaya za Njombe, Ludewa na Makete pamoja na Gereza la Ludewa na
Makete.
“Ushirikiano wa karibu
na Wadau wa Mahakama kama Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Mawakili na Watumishi wa Mahakama n.k ni
muhimu katika kutekeleza shughuli yetu ya utoaji haki kwa wananchi, jambo hili
lina faida nyingi mojawapo ikiwa ni kusaidia kupunguza mlundikano wa kesi
katika Mahakama zetu,” alifafanua Mhe. Shangali ambaye pia ni Jaji namba moja (1)
wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa upange mwingine,
Mhe. Jaji Shangali alibainisha changamoto alizokumbana nazo katika ziara yake
ya kukagua shughuli za Mahakama mkoani Njombe kuwa ni tatizo kubwa la usafiri
wa kuwachukua Mahabusu kutoka Magerezani na kuwarudisha.
“Hii ni moja ya
changamoto kubwa niliyokumbana nayo katika Mahakama zote nilizozitembelea
mkoani Njombe, changamoto hii haiihusu Mahakama moja kwa moja ipo chini ya Jeshi
la Polisi, lakini kwa kuwa tunafanya kazi kwa kutegemeana changamoto hii
inatuathiri na inaweza kusababisha mlundikano wa mashauri na Mahabusu
magerezani kutokana na Wahusika wa kesi kutofikishwa Mahakamani kwa ajili ya
kusikiliza kesi zao kwa wakati stahiki,” alisema Jaji Shangali.
Aliongeza kuwa, katika
ziara hiyo malalamiko mengine yaliyotolewa yaliwahusisha baadhi ya Mahakimu
kuwa na tabia ya kutowasikiliza Washitakiwa kwa makini na hatimaye kutoa
maamuzi tofauti na uhalisia wa shauri husika.
“Naomba niwaombe ninyi
Mahakimu mliopo hapa na baadhi ya Mahakimu nchini kutekeleza jukumu la utoaji
haki kwa Weledi, kwani Mahakama ndio kimbilio la wananchi hivyo ni vyema kutoa
nafasi kusikiliza kwa makini na usahihi pande zote ili kufanya maamuzi
yanayostahili,” alieleza Jaji Mfawidhi huyo.
Aidha; Mhe. Jaji
Shangali amesisitiza juu ya utoaji wa Adhabu Mbadala kwa watuhumiwa wenye
makosa madogo madogo ili kuepuka mlundikano usio wa lazima magerezani.
Akiongelea juu ya Programu
maalum ya kuondosha mlundikano wa Mashauri linaloendelea nchini, Jaji Mfawidhi
alisema kwa sasa Mahakama kanda ya Iringa inaendelea na kikao maalum cha
Mahakama (special session) cha awamu ya tatu (3) kilichoanza rasmi Mei 29
kinachofanyika Njombe chini ya Mhe. Paul Kihwelo ambapo katika kikao hicho
jumla ya mashauri 32 yatasikilizwa na kutolewa maamuzi.
“Kikao cha awamu ya
kwanza kilianza rasmi Aprili, 24 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa na Makao
makuu na kumalizika Mei, 26 mwaka huu, katika kikao hicho jumla ya mashauri 41
yalipangwa kusikilizwa na kutolewa maamuzi, hata hivyo hadi kufikia Mei 26,
jumla ya mashauri 37 yalimalizika huku mengine yakiwa yanaendelea na
usikilizwaji wa awali na mengine yakiwa katika hatua ya mwisho ya kutolewa
maamuzi,” alisema Jaji Shangali.
Aliongeza kuwa kikao
kingine cha pili kilifanyika Mafinga huku jumla ya mashauri 28 kati ya mashari
42 yaliyopangwa kusikilizwa kumalizwa, hata hivyo alisema kuwa mashauri mengine
yaliyobaki yapo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuyatolea maamuzi.
Waheshimiwa Majaji wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa wamejiwekea utaratibu wa kukagua Mahakama na
utendaji kazi wake pindi wanapomaliza kufanya kikao maalum katika sehemu
husika, hali ambayo huwawezesha kujua changamoto na mafanikio mbalimbali
yaliyopo katika maeneo hayo, lengo kuu likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji
haki kwa wananchi.
Hata hivyo Mahakama ya
Tanzania kupitia Maafisa wake imekuwa na utaratibu wa kufanya kaguzi za mara
kwa mara kwa nyakati tofauti kwa lengo la kufuatilia kwa karibu kuona hali ya
utendaji wa Mahakama mbalimbali kama zinaendana na matakwa ya Mhimili huu
muhimu wenye dhamana ya kutoa haki kwa wananchi.
Zifuatazo ni baadhi ya picha za kikao Kati ya Mhe. Jaji Mfawidhi na Wahe. Mahakimu
Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali akisisitiza jambo alipokuwa akiongea
na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe baada ya kukamilisha ukaguzi
katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya zilizopo mkoani humo.
Mhe.
Jaji Mfawidhi akiongea jambo huku akiwaonyesha baadhi ya Mahakimu (hawapo
pichani) nakala ya kitabu cha Muongozo wa kufanya ukaguzi wa Mahakama alipokuwa
akiongea nao mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua, Mahakama za
Mwanzo na Wilaya- Njombe.
Pichani ni Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto akiendelea na kazi, Mhe. Jaji Dkt. Kihwelo yupo Njombe akiendelea na vikao maalum vya kuondosha mlundika wa mashauri linaloendelea kwa sasa.
Baadhi ya Wahe. Waliohudhuria
katika kikao kati ya Mhe. Jaji Mfawidhi na Mahakimu Mkoani Njombe.
Wahe. Mahakimu
wakiandika baadhi ya masuala muhimu aliongelea Mhe. Jaji Mfawidhi katika kikao
hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mahakama ya Wilaya-Njombe mapema Juni 8.
Wahe.
Mahakimu wakiandika masuala kadhaa aliyoyaongelea Mhe. Jaji Shangali katika
kikao hicho.
Hakimu wa Mahakama ya
Mwanzo-Lupembe iliyopo mkoani Njombe, Mhe. Godfrey Msemwa akiuliza swali ili
kupata ufafanuzi.
Mmoja wa Mahakimu
Naibu Msajili, Mahakama
Kuu-Kanda ya Iringa , Mhe. Agatha Chugulu (aliyesimama) akitoa ufafanuzi juu ya maswali kadhaa
yaliyoulizwa katika kikao hicho, aliyeketi kushoto ni Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali.
Naibu
Msajili, Mhe. Chugulu akiendelea kutoa ufafanuzi.
Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe mara baada ya kika, wa
tatu kushoto ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Agatha
Chugulu.
Muonekano wa jengo la
Mahakama ya Hakimu Mkazi-Njombe, jengo hili limegawanyika sehemu mbili (2),
ambapo upande mwingine ipo Mahakama ya Wilaya- Njombe.
Muonekano wa sehemu ya
jengo la Mahakama ya Wilaya-Njombe.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni