Jumatatu, 31 Julai 2017


HOTUBA YA KAIMU JAJI MKUU PROFESA IBRAHIM HAMIS JUMA, KUSHEHEREKEA MABORESHO YA JENGO LA MAHAKAMA KUU KANDA YA MBEYA NA KULIGEUZA KUWA KITUO JUMUISHI CHA KISASA KATIKA KUTOA HUDUMA ZA KIMAHAKAMA (INTEGRATED JUSTICE CENTRE)
TAREHE 27-07-2017

 
Mhe. Ferdinand Wambali, Jaji Kiongozi,

Mhe. Jaji Noel Peter Zaudin Chocha, Jaji Mfawidhi, Mbeya

Mhe. Jaji John Samwel Mgetta, Jaji Mfawidhi, Sumbawanga

Mhe. Jaji Atuganile Florida Ngwala

Mhe. Jaji Dkt. Mary Caroline Levira

Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi

Mhe. …. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya

Mhe…… Mkuu wa Mkoa wa Songwe

Bw. Dennis Biseko, Muwakilishi wa Benki ya Dunia

Prof. Angelo Mapunda, Mjumbe Tume ya Utumishi wa Mahakama

Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu Mahakama

Mhe. Katarina Revocati, Msajili Mkuu

Mhe. John Rugalema Kahyoza, Msajili Mahakama ya Rufani

Wah. Wasajili na Watendaji

Wadau wa Jengo hili

Wafanyakazi na wageni wote mliohudhuria;

1.0 UTANGULIZI—

Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya kiasi cha kufika na kushuhudia kukamilika kwa maboresho makubwa katika Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na kuweka huduma za wadau muhimu wa Mahakama katika jengo moja na huduma za mahakama katika ngazi kuanzia Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ni kuliita hili jengo kama KITUO JUMUISHI CHA KUTOA HUDUMA ZA KIMAHAKAMA (Integrated Justice Centre).

Hii dhana ya kuwa na huduma mbali mbali ambazo kwa kawaida huwa katika sehemu tofauti na mara nyingi hata kwa umbali na kuziweka ndani ya jengo au eneo moja sio geni hapa Tanzania. Katika fani ya biashara, wengi wetu tunafahamu sokoni unapoenda kupata kununua mahitaji yako au maduka makubwa ya supermarket ambayo utaweza kununua kila kitu unachotaka kununua katika jengo moja. Mwaka 2015, Bunge la Tanzania lilitunga Sheria Maalum [ONE STOP BORDER POSTS ACT NO. 17/2017] iliyoanzisha kituo kimoja cha mpakani kwa nchi mbili zinazopakana, kwa ajili ya kutoa huduma za VISA, UHAMIAJI na maswala ya ushuru.

Hivyo hivyo, tutegemee jengo hili litatoa huduma za kimahakama kwa ngazi mbali mbali, na pia huduma za wadau wa karibu wa mahakama kama WANASHERIA WA SERIKALI, MAWAKILI WA KUJITEGEMEA, USTAWI WA JAMII, POLISI na MAGEREZA. Kwa sababu MKONGA WA TAIFA unaopitisha mawasiliano ya haraka tayari yameunganishwa na JENGO HILI, huduma za mahakama na za wadau ndani ya jengo zitaunganishwa kwa urahisi kwa mfumo wa utakaosambaa Tanzania na dunia nzima.


1.1 UTEKELEZAJI WA MPANGO MKAKATI KWA VITENDO

Maboresho ya huduma ndani ya Jengo hili ni mfano tu wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama kwa vitendo sio maneno. Mpango Mkakati ulizinduliwa rasmi tarehe 21/09/2016  huko Kibaha na Waziri Mkuu, Mhe.  Majaliwa Kassim Majaliwa (MB) kwa niaba ya Mhe. Rais. Kwa sasa, ni Mpango Mkakati huo ndio unaongoza shughuli za Mahakama zinazolenga kumuwezesha mwananchi kupata haki kwa wakati. Mpango Mkakati umegawanyika katika nguzo kuu tatu:

NGUZO YA KWANZA NI: Utawala bora, Uwajibikaji na Usimamiaji wa Rasilimali. Wananchi watapenda kuona utawala bora, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilmali unnaonekana kwa vitendo ndani ya jengo hili.

NGUZO YA PILI NI: Upatikanaji na utoaji haki kwa Wakati. Wananchi watataka kuona kuwa ngazi zote za Mahakama na wadau wote walio ndani ya jengo hili la kisasa, wanakamilisha utoaji wa haki kwa haraka.

NGUZO YA TATU NI: Kuimarisha Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau. Tayari wadau wamesogezwa na kuwekwa ndani ya jengo hili. Ni lazima hawa wadau na ngazi za kimahakama, kwa pamoja zihakikishe kuwa wananchi wanakuwa na imani kuwa haki iliyo na ubora inapatikana kwa haraka bila kugubikwa na vitendo vya rushwa au utovu wa maadili.

1.2 Jengo hili ni Picha ya Huduma za Mahakama zitavyokuwa 2025
Jana, nilipokuwa naongea na wafanyakazi wa Mahakama na kuwasihi walinde na kutunza uwekezaji mkubwa uliofanyika, niliwakumbusha kuwa huduma zilizopo ndani ya Jengo, hili ni huduma ambazo Tanzania ya DIRA 2025 inategemea kutoka Mahakama zote nchini. Hivyo basi, jengo ni ishara tosha kuwa Mahakama ya Tanzania inaachana na ujenzi wa kizamani na itakuwa ikijenga majengo shirikishi kwa wadau wengine katika utoaji haki. Ishara ya dunia ya leo kuwa majengo ni lazima yarahisishe matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji haki.

 2.0 WAKUU WA MIKOA NA WILAYA NI WADAU MUHIMU MPANGO MKAKATI

Napenda kutambua umuhimu wa uwepo wa wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Songwe— Amos Gabriel Makalla (Mkuu wa Mkoa Mbeya) na Mhe. Luteni Mstaafu Chiku Galawa (Mkuu wa Mkoa wa Songwe). Hawa viongozi ndio wanaotegewa na wananchi katika mikoa yao kuratibu shughuli za ustawi na maendeleo ya wananchi kama Katiba ya Jamhuri inavyoagiza kuwa kazi kubwa ya Serikali itakuwa ni ustawi wa wananchi.

Napenda pia kusisitiza kuwa katika utoaji haki, Mhimili wa Mahakama Wakuu unasaidia kuleta amani na kutatua migogoro ambayo inaweza kuchelewesha ustawi na maendeleo ya wananchi. Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wakuu wa Wilaya vile vile ni wadau muhimu sana katika mfumo wa utoaji haki hapa Tanzania. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wana nafasi kubwa na muhimu katika kusaidia kupatikana kwa majengo mapya ya Mahakama. Wakuu wa Mikoa na Wilaya ni sehemu muhimu katika taratibu za kinidhamu za Mahakimu kupitia Kamati za Maadili za Wilaya na Mikoa wanazoziongoza kanma wenye viti.

Mhimili wa Mahakama unatambua kuwa ushiriki wa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya katika maswala ya utoaji haki ni utekelezaji wa mfumo wetu wa Kikatiba na kisheria ulio shirikishi na unaotaka Mihimili yote ya Dola ishirikiane katika lengo la kuiwezesha Mahakama kibajeti ili iweze kutoa haki kwa wakati kwa mujibu wa sheria za nchi.

 
3.0 JENGO HILI LA KISASA LITUKUMBUSHE SAFARI NDEFU MBELE YETU YA KUPELEKA UTOAJI WA HAKI KARIBU NA WANANCHI

Jengo hili linatukumbusha safari ndefu ambayo iko mbele yetu watanzania ya kuiwezesha Mhimili wa Mahakama kuwa majengo ya kisasa, ya kutosha na yaliyo na vifaa vya kisasa ili Mahakama ishiriki kikamilifu katika utoaji haki kwa wakati kwa wananchi.

Mahakama bado inayo changamoto kubwa ya kupeleka Mahakama karibu zaidi na wananchi kwa sababu upungufu wa rasilmali ya kutosha. Vile vile, Mahakama inachangamoto ya kuifuata nyuma pale serikali inapoamua kuanzisha mikoa na wilaya mpya. Kuna umuhimu kwa MIHIMILI YA BUNGE wakati inakubaliana kuanzisha mikoa na wilaya, basi Hazina itenga rasilmali ya fedha za kutosha mahsusi kwa Mahakama. Aidha, ujenzi wa makao makuu ya mikoa na wilaya iambatane na ujenzi wa majengo ya Mahakama  ili huduma za utoaji haki katika mikoa na wilaya mpya ziwe sambamba na huduma zinazotolewa na Serikali Kuu na Halmashauri mbali mbali. Kwa sasa Mkoa wa Njombe unasubiri jengo lake la Mahakama Kuu wakati inahudumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa. Mkoa wa Songwe unasubiri kupata jengo la Mahakama Kuu na Mhakama za ngazi nyingine.

4.0 KITUO KINATUKUMBUSHA MCHANGO WA BENKI YA DUNIA
Napenda kuchukua nafasi hii kutambua uwepo wa Mwakilishi wa Benki ya Dunia. Benki ya Dunia inatambua kuwa Mahakama iliyo karibu na wananchi, ni mdau mkubwa katika ujenzi wa uchumi na uwekezaji katika nchi husika.

Leo ni siku nzuri ya kutafakari mchango mkubwa wa Benki ya dunia kusaidia azma ya Mahakama ya Tanzania kuwapelekea wananchi wengi huduma bora za utoaji haki. Kutokana na ushirikiano wa karibu na muda mrefu kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia inafahamu kwa undani changamoto zinazozikabili Mahakama za Tanzania, wapi mahakama zielekee katika mizani ya kufikisha huduma bora za utoaji haki kwa wananchi wengi zaidi. Benki ya Dunia inatumia maneno— Citizen-Centric Justice in Tanzania katika kusisitiza ukweli kuwa maboresho ya Mahakamahayatakuwa na maana yoyote endapo yatawatenga wananchi wa Tanzania wengi wao wakiwa masikini sana.
Mahakama inafurahi kuona kuwa Benki ya Dunia, kama mdau inafutilia kwa ukaribu namna Mahakama inavyokabiliana na changamoto za uboreshwaji wa huduma. Tarehe 23 Mei 23, 2017 nilisoma  jarida la Benki ya dunia lenye stori kuhusu WANANCHI WA TANZANIA WAWE LENGO LA MABOERSHO YA MAHAKAMA (FEATURE STORY-Citizen-Centric Justice in Tanzania: Expanding and Modernizing Court Services):

o   Jarida lilitukumbusha kuwa huduma za Mahakama bado haziwafikii zaidi ya wananchi milioni 25.

·        Maboresho ya Mahakama yalenge katika kuongeza idadi ya wananchi watakaopata huduma za mahakama.

·        Inasisitiza umuhimu kujengwa kwa Mahakama mpya na kupunguza makali yanayowakabili wananchi wengi ya kutokuwa na majengo ya mahakama. Benki ya Dunia imetoa wazo kuanzishwa kwa MAHAKAMA ZA KUTEMBEA (MOBILE COURTS) ili kupeleka huduma za utoaji haki kwenye maeneo yenye changamoto ya umbali kutoka mahakama za karibu.

·        Jarida lilitoa mfano wa Hakimu Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, Esther Kihiyo. Anawahudumia wananchi 33 kila siku. Anasikiliza na kuandika ushahidi kwa mkono wake na kuandika hukumu kwa mkono wake. Jengo la Mahakama ya Mwanzo analofanya kazi Esther Kihiyo halina huduma ya umeme, kwa hiyo anatumia Mwanga wa jua unaopenyeza kupitia madirishani. Pamoja na changamoto hizi, Esther anasema bado atafanya kazi licha ya ufinyu wa ofisi na kumbi za mahakama, licha ya kuwa na mfumo wa ki-elektroniki wa kusajili mashauri, bila kujali kuwa nafuu anayopata kila siku ni Mwanga wa jua.

·        “Majengo yetu sio mazuri,” anasema Esther Kihiyo…..  “wakati mwingine mvua zikinyesha majalada hulowa na mengine kupotea”

 Changamoto anazokabiliana nazo Esther Kihiyo ni za kawaida kabisa katika Mahakama nyingi za Tanzania. Hizi ni baadhi tu ya changamoto, ambazo Mahakama, kupitia mpango mkakati na maboresho, inakabiliana nazo. Ukarabati na maboresho katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ni mfano tu wa hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa Mpanga Mkakati na Programu za Maboresho.

Baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa, jengo la Mahakama Kuu Mbeya ni mfano wa kufuatwa wa kutatatua kabisa kawaida ya kuhama hama ofisi pindi Mahakama ya Rufani inapokuwa na vikao katika Kanda za Mahakama Kuu.

Katika Taarifa aliyoisoma kwa Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi tarehe 14/07/2017, Mtendaji Mkuu wa Mahakama alielezea changamoto la majengo:

      Mahakama kama mhimili wa Dola  haina jengo lake la Mahakama ya Rufani, wala Makao Makuu;

      Bado lengo la kila Mkoa katika Mikoa 26 kuwa na jengo la Mahakama Kuu bado haijafikiwa. Hata Mikoa yenye majengo ya Mahakama Kuu yapo katika hali mbaya na ni ya zamani na ya kurithi na yasiyoendana na hali ya sasa ya utoaji huduma wa Mahakama;

      Mahakama za Hakimu Mkazi 30, ni 10 tu zenye majengo;

      Kati ya Wilaya – 139 zinazopaswa kuwa na Mahakama ya Wilaya kwa mujibu wa Sheria ni 110 tu ndizo zinazofanya kazi kati ya hizo majengo ya Mahakama 28 ndizo zinazomilikiwa na Mahakama mengi yapo kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya, jmajengo ya maendeleo ya Jamii ya Halmashari n.k.

      Kuna Mahakama za Mwanzo 960. Changamoto kubwa ni uwepo wa Kata rasmi 3,963 za  Kiserikali  zinazohitaji huduma za Mahakama ya Mwanzo. Nyingi ya Mahakama za Mwanzo 960 zilizopo zina ubovu mkubwa usio na mazingira mazuri ya utoaji haki.

      Nyumba za Majaji nyingi ni za kupanga kwa watu binafsi na tunahitaji nyumba za kufikia Majaji kila Mkoa zenye huduma toshelezi.
Ingawa Mahakama za Mwanzo zinasikliliza asilimia 70% ya mashauri yote yanayowasilishwa katika ngazi mbali mbali za kimahakama, mahitaji ya majengo ya mahakama za Mwanzo bado ni kubwa sana. Chini ya Mpango wa Maboresho ya Mahakama, ramani ya mahitaji ya majengo mapya ya Mahakama za Mwanzo imetayarishwa ili kurahisha ujenzi pale fedha zitakapopatikana. Kwa mfano, ni dhamira ya Mahakama kuwa kila KATA hapa Tanzania iwe na Jengo la Mahakama ya Mwanzo, na lenye vifaa vya TEHAMA.
Ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo ni hatua muhimu ya kufikisha huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi walio wengi huko katika kata zaidi ya 3500 za Tanzania. Kwa kutambua kuwa gharama za ujenzi ni kubwa na inaweza kuchelewesha huduma za mahakama kuwafikia wananchi, Mahakama ya Tanzania, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi, imeanza kutumia Teknolojia ya Ujenzi wa Gharama Nafuu unaoitwa MOLADI. Teknolojia hii pia inaweza kupunguza gharama za ujenzi kwa asilimia 50%.

Kupitia utafiti wa kina uliofanywa na idara ya mipango ya Mahakama, Mikoa ya Mbeya na Songwe ina mahitaji ya majengo ya Mahakama za Mwanzo ili kufikia azma ya kuwa na Mahakama ya Mwanzo katika kila KATA:

 MKOA WA MBEYA

 
Wilaya
Mahakama za Mwanzo zilizopo Idadi ya Kata
IDADI ZA KATA
UPUNGUFU WA MAHAKAMA ZA MWANZO
Wilaya ya Mbeya
10
64
54
Wilaya ya Kyela
11
33
22
Wilaya ya Rungwe
15
29
14
Wilaya ya Mbarali
7
20
13
Wilaya ya Chunya
8
23
15
 
 
 
118

 MKOA WA SONGWE

Wilaya
Mahakama za Mwanzo zilizopo Idadi ya Kata
IDADI ZA KATA
UPUNGUFU WA MAHAKAMA ZA MWANZO
Wilaya ya Ileje
5
18
13
Wilaya ya Mbozi
11
29
18
Wilaya ya Momba
 
14
14
 
 
 
45

 5.0 MWISHO: MATARAJIO YA WANANCHI KUTOKA KITUO HIKI JUMUISHI CHA KUTOA HUDUMA ZA KIMAHAKAMA

1.   Kituo litakuwa rafiki kwa wananchi wote na kitahudumiwa na watumishi wa Mahakama wenye bidii, weledi na wanaochukia vitendo vinavyokiuka maadili. Pamoja na umuhimu wa kuwakaribisha wananchi kutumia huduma katika jengo, lazima kuwe na utaratibu kudhibiti usalama na uharibifu na matumizi maaya ya jengo. Namkabidhi Mheshimiwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya atashirikiana na wadau, aweke utaratibu wa namna gani wananchi watatumia jengo hili.

2.   Fedha nyingi zimetumika kulifanyia ukarabati mkubwa jengo na kuliwekea vifaa vipya vingi vya kisasa ikiwa ni pamoja na— Miundo mbinu ya TEHAMA, Huduma ya mawasiliano ya kimkutano kupitia video (Video Conference Facilities), huduma ambayo ikitumika inavyotegemewa, inaweza kupunguza gharama za mashahidi, kwamba, badala ya mashahidi kuletwa Mbeya wanaweza kusikilizwa huko walipo kwa njia ya video. Majengo ya kisasa yanaendana na umuhimu wa watumiaji kubadili TABIA na namna wanavyotumia Jengo.

3.   Pamoja na jukumu la kutunza jengo, maboresho na vifaa vilivyomo, kuwepo kwa mfumo wa matengenezo madogo madogo. Kwa kulitunza na kulienzi, hili jengo liendelee kuwa la mfano kwa mahakama zote Tanzania.

4.   Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya itakuwa ni mfano wa kuigwa katika kukusanya Takwimu ki-elektroniki na pia itakuwa ni mfano wa kuingiza, kuhifadhi na kutoa taarifa mbalimbali za mashauri kwa njia ya mitandao.

5.   Kwa kuwa Jengo litakuwa na ofisi za wadau wengine katika utoaji haki, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya itakuwa mfano wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya wadau hawa wenye jukumu la kutoa haki.

6.   Kuongezeka kwa kasi ya kumaliza mashauri yote, na hasa yale yenye maslahi kwa umma (kwa mfano: ya kibiashara, ardhi, na makosa makubwa ya kijinai kama—rushwa, madawa ya kulevya)

7.   Kumaliza mlundikano wa mashauri

8.   Kusimamia shughuli za utendaji wa mahakama na maadili ya maofisa wa mahakama na watumishi wengine.

MWISHO

Nawaomba wakuu wa mikoa na wilaya tuwe sehemu ya Mpango Mkakati na program ya maboresho. Kwa nchi kama TANZANIA yenye mahitaji makubwa lakini rasilmali fedha ni kidogo, ushirikiano unaoongozwa na Mpango Mkakati ni muhimu.

Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.

Ibrahim H. Juma

Kaimu Jaji Mkuu

27-07-2017

<><><><><><<><< 





HOTUBA FUPI YA KAIMU JAJI MKUU KATIKA UFUNGUZI RASMI WA JENGO LA MAHAKAMA YA WATOTO, MBEYA
26 JULAI 2017

1.0 UTANGULIZI—
Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya kiasi cha kufika na kushuhudia UFUNGUZI RASMI WA JENGO LA MAHAKAMA YA WATOTO hapa Mbeya. Mahudhurio ya Wadau wengi katika sherehe hizi za ufunguzi ni ishara tosha kuwa utekelezwaji wa Haki za Watoto zilizoainishwa katika Mikataba ya mbali mbali ya kikanda na Kimataifa na kupewa nguvu ya kisheria kupitia Sheria ya watoto ya mwaka 2009, linahitaji  ushirikiano baina ya taasisi na wadau wa haki za watoto.

 2.0 Maendeleo Endelevu yajengwa kwa misingi ya Haki za Watoto
Wakati natafakari ni jambo gani nisisitize wakati wa ufunguzi wa jengo hili, nilipata bahati ya kusoma andiko la Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, kuwa Maendeleo Endelevu yanaanza na kukamilika kwa misingi ya watoto kuwa salama,wawe ni wenye afya bora na waliopata elimu bora [SUSTAINABLE DEVELOPMENT STARTS AND ENDS WITH SAFE, HEALTHY AND WELL-EDUCATED CHILDREN, UNICEF, May 2013]. Katika neno lake la utangulizi katika andiko hilo, Anthony Lake, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF aliandika kuwa:

“Haki za watoto na siha yao njema, lazima ipewe kipaumbele katika maandalizi ya ajenda ya maendeleo endelevu ya baada ya mwaka 2015. Uwekezaji kwa manufaa ya watoto ni njia bora ya kufuta umaskini, kuongeza kasi ya kuchanua kwa manufaa kwa wote ….” 

       Children’s rights and well-being should remain at the centre of the post-2015 agenda. Investment in children is a fundamental means to eradicate poverty, boost shared prosperity, and enhance inter-generational equity. It is also essential for strengthening their ability to reach their potential as productive, engaged, and capable citizens, contributing fully to their families and societies. Sustainable development starts and ends with safe, healthy and well-educated children
       Jarida kwa ufupi linatuonya kuwa, tukiamua kudharau HAKI ZA WATOTO kwa upana wake sasa, azma ya maendeleo endelevu ya NCHI hapo baadae, itakuwa hatarini.

 3.0 Ustawi wa Watu wa Tanzania unaanza na Ustawi wa watoto
Maana ya Ustawi wa Watu wa Tanzania unaanza na Ustawi wa watoto ni kwamba tayari Katiba imetamka kuwa LENGO KUU NA JUKUMU LA SERIKALI ni USTAWI WA WANANCHI. Sasa, huo ustawi wa wananchi ni lazima ujengwe MISINGI IMARA YA USTWI WA WATOTO wa LEO HII:

·        Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka 2012, Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ina idadi ya watu Milioni:              44,928,923.

·        Watoto wenye umri: 0 ––– 4yrs. = 7,273,832 = 16.2%

·        Vijana [Young population] 0 ––– 14yrs. = 19,725,456 =43.9%

·        Vijana [Young population] 0 ––– 17yrs. = 22,504,526 =50.1%

 Kwa hiyo, kitendo cha leo cha ufunguzi wa jengo maalum la Mahakama ya Watoto ili isikilize mashauri ya watoto, ni tone tu ya mambo mengi ambayo jamii inatakiwa kufanya ili kuendeleza asilimia ya 50% ya wananchi wake ambao wana umri wa miaka 18 na kurudi chini. Ni tone dogo kwa sababu, kufikishwa katika mazingira bora ya kusikilizwa kwa mashauri yake hakumpunguzii mtoto— kukosa elimu, afya bora au hakufanyi mahabusu atakayorudishwa mtoto huyu kuwa na hali inayozingatia maslahi ya watoto.

Basi, ni wajibu wa Mahakimu wa Mahakama ya Watoto waulize maswali magumu kwa wale wanaowaleta watoto mahakamani kama huko wanapotoka au huko watakapo wahifadhi watoto wakati wa kusikilizwa kwa mashauri na baada kusikilizwa kwa mashauri pana endeleza maslahi mapana ya mtoto.

4.0 Mikataba ya Haki za Watoto Iliyoridhiwa na Tanzania

·        Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto [UN Convention on the Rights of the Child (UNCRC)]

·        Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto [African Charter on the Rights and Welfare of the Child (ACRWWC)]

·        United Nations Standard Minimum Rules for the Administration of Juvenile Justice (Beijing Rules)

·        United Nations Guidelines for the Prevention of Juvenile Delinquency (The Riyadh Guidelines).

5.0 Ni Matokeo Ya Kutungwa Kwa Sheria Ya Mtoto

Kutungwa kwa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya 2009 ni kwa ajili ya haki, ulinzi na ustawi wa mtoto:

·        Sheria hii imekusanya mapendekezo yote (ya ndani ya Tanzania, Kikanda, kimataifa) kuhusu maboresho ya haki na maslahi mapana ya mtoto na kutoa nguvu ya kisheria;

·        Baada ya kutungwa kwa Sheria mihimili ya dola imepewa majukumu ya kutekeleza na kuwajibika. Kwa Mhimili wa Mahakama, tunategemea Mahakama ya Watoto itusaidie kuwajibika na kutekeleza Sheria ya Mtoto.

 Kuna maeneo kadhaa katika Sheria ya Watoto ambayo yanasimamiwa na mamlaka nyingine. Pamoja na ukweli huo, bado Mahakama ya Watoto inaweza kutoa ushirikiano kwa mamlaka hizo au amri za mahakama zikasaidia utendaji wa mamkaka hizo, kwa mfano:

o   Mazingira mbalimbali ambayo yameainishwa na Sheria Namba 21 ya 2009 kuwa ni HATARISHI kwa mtoto— kama vile uyatima, kutelekezwa, kuteswa, kuzurura, kukinzana na sheria—Mahakama ya Watoto inaweza kutoa tafsiri na kupanua wigo wa “mazingira hatarishi” ;

o   Mahakama ya Watoto inaweza kutoa tafsiri na kupanua wigo wa– Ulinzi na wajibu wa wazazi kwa matunzo ya mtoto,matibabu na elimu;

o   Sifa za mtu kuwa mlezi na uasili wa mtoto;

o   Namna gani Mahakama itawasilisha taarifa mbali mbali au kutumia rejista ya watoto walioasiliwa kwa Msajili wa Vizazi na Vifo;

·        Uzuiaji wa kazi za udhalilishaji kwa watoto chini ya miaka 18.

·        Mahakama ya Watoto inaweza kutakiwa kutoa miongozo kuhusu mafunzo ya kazi (apprenticeship) kwa watoto chini ya miaka 18 na kuchunguza mikataba ya mafunzo ya kazi ambayo ni kandamizi au yasiyozingatia maslahi ya mtoto.

o   Mahakama ya Watoto inaweza kutoa maamuzi ambayo yatazikumbusha Serikali za Mitaa wajibu wao wa kuboresha ustawi wa mtoto walio ndani ya mamlaka za Serikali ya Mtaa husika.

o   Mahakama inaweza kuitahadharisha Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na Halmashauri wajenge shule maalum za watoto za kutosha. Hii itasaidia Mahakama ya Watoto kuwa, badala ya adhabu ya vifungo gerezani, watoto waliopatikana na hatia wapelekwe. Kwa kuanzisha na kuendesha Shule, Mihimili mingine nayo itakuwa inaisaidia Mahakama na Magereza kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria Namba 21 ya 2009.

o   Serikali za Mitaa na Serikali Kuu zitasadia sana Mahakama pale zitakapoanzisha vituo vya kutunzia na kulelea watoto wenye shida ya malezi na Bunge kutoa fedha za kutosha kuendesha vituo hivyo.

o   Mahakama za Watoto zinaweza kugundua mapungufu katika Sheria na kupendekeza kuwa Waziri mwenye dhamana ya watoto atunge  kanuni stahiki.

 6.0 Sheria Ya Mtoto: Shirikishi Na Inataka Ushirikiano
Tukumbuke kuwa Sheria Namba 21 ya 2009 imesimama katika misingi ya ushirikiano baina ya mihimili yote, ushirikiano na wadau mbali mbali kama UNICEF na NGOs zinashughulikia haki za watoto. Tukumbuke kuwa kuna mambo ambayo Sheria ya Mtoto inaitaka Mahakama ichukue uongozi, na kuna maswala ambayo mihimili mingine imepewa nafasi ya uongozi.
Ni nafasi nzuri sana kwa Mahakama kuipa uhai sheria (give life and meaning to the Law of the Child):

·        kwanza haki zote stahili zilizoainishwa ndani ya Sheria Namba 21 ya 2009 yanamfaidisha mtoto.

·        Pili, wanapotafsiri Sheria Namba 21 ya 2009, pale ambapo wanaona kuna “kutofahamika, “utata” n.k. wawe na ujasiri wa kuielekeza sheria kufikia malengo mazuri yaliyowekwa na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu haki ya watoto.

·        Tatu, kwa sababu Mahakimu katika Mahakama ya Watoto watakuwa na nafasi ya karibu kabisa kuona namna vifungu mbali mbali vya Sheria Namba 21 ya 2009 vinavyofanya kazi, wawe na wepesi kuorodhesha mapungufu katika Sheria hii na kuziwasilisha mbele ya Kamati ya Kanuni ya Jaji Mkuu kwa ajili ya kupendekeza kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu mabadiliko ya Sheria.

·        Nne, Mahakimu wawe tayari kukabiliana na matukio ambayo wakati Bunge linatunga Sheria haikuzitarajia. Nitawapa mfano wa changamoto niliyoletewa siku chache zilizopita kutoka kwa ….

o   Rahim O. Mpogo, Katibu Mtendaji, Umoja wa Miradi kwa Viziwi Tanzania [UMIVITA]:

o   “Kutokana na viziwi kuwa sehemu ya jamii ya watanzania ambapo kwa mujibu wa sera ya taifa ya watu wenye ulemavu ambayo ilipitishwa mwaka 2004 idadi ya viziwi iliopatikana kupitia sense maalum ya kufanya utambuzi wa watu wenye ulemavu ni milioni mbili (2,000,000).

o   Viziwi pia hupata misukosuko ya kimaisha ikiwemo kufikishwa/kushtakiwa/kushtaki kwa makosa mbali mbali wanayotuhumiwa/Kutuhumu.

o   Wamekuwa wakikosa huduma ya ukalimani wa lugha ya alama wakati wa usikilizaji wa kesi zao kitu ambacho kwa kiasi fulani huwanyima haki ya kupata kile kinachoendelea..

o   Kwa sasa kuna kesi mbili za viziwi ambazo ziko katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo na Baraza la Usuluhishi la migogoro ya ardhi Wilaya ya Ilala ambapo malipo kwa ajili ya huduma ya ukalimani bado hayajakubaliwa.

o   Hivyo, UMIVITA ingependa ofisi yako izitaarifu Mahakama zote nchini kuhusu huduma hii ya ukalimani kwa viziwi na iwajibike katika malipo ya huduma.

 7.0 MWISHO:
Pengine nimalizie kusisitiza mambo kadhaa:

7.1 Wajibu wa kujisomea na kujua maendeleo katika Haki za Mtoto Duniani

Mahakimu katika Mahakama ya Watoto wasiridhike kwa kusoma Sheria ya Mtoto tu na Kanuni ambazo anazitumia kila siku wakati dunia inabadilika na kutafakari haki za mtoto.
Tanzania, kama nchi nyingine zilizoridhia mikataba mbali mbali kuhusu haki za watoto, inawajibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa mikataba hiyo. Mahakimu ni lazima tusome Ripoti za Utekelezaji zinazowasilishwa na Tanzania na pia zile zinazowasilishwa kuhusu Tanzania. Ripoti hizi zinatuwezesha kugundua mapungufu yetu ya kiutekekezaji na sisi kupanga namna ya kuboresha utekekezaji.

 kama za Watoto: Ziwe Chanzo cha Mafunzo Kwa Mahakama zingine

o   Ni kesi chache sana hukatiwa rufaa na kufika Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani. Kwa hiyo, mafunzo kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Mtoto yatapatikana kutoka Mahakama za Watoto. Wekeni kumbukumbu zenu vizuri, andikeni hukumu zinazoelimisha. [Very few cases go very far up to the HC and CAT, we shall be reading the principles you will be making, to expand the jurisprudence of the welfare of the child.. [Obtaining coherent information on case law in Tanzania is hampered by the lack of comprehensive searchable case law data base].

 7.3 Ukaguzi wa Magereza, Sehemu wanapozuiliwa watoto, na kufuatilia taarifa
        Wajibu wa Hakimu [Proactive Role]

·        Magazeti na TV ni njia rahisi sana ya kujua mapungufu katika mfumo wa utoaji haki kwa watoto waliokinzana na sheria.

·        Tanzania yakiuka Mkataba wa Kimataifa wa haki ya mtoto Gerezani: by-- Mkombe Zanda (Mbeya):

o   Licha ya Tanzania kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, CRC, unaozuia kuwachanganya watoto na watu wazima gerezani lakini bado kuna watoto wengi wanaokaa magerezani kote nchini kinyume na mkataba huo.

o   Mbali na kuridhia Mkataba huo wa Kimataifa, Tanzania pia imeunda Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ili kulinda haki za mtoto lakini bado juhudi hizo hazijafanikiwa kuondoa uwezekano wa watoto kuishi magerezani kinyume na matakwa ya kisheria.

o   Kushindwa kwa Tanzania kutekeleza ipasavyo mkataba huo wa Kimataifa na sheria hiyo iliyoundwa nchini, kumebainishwa jijini Mbeya na Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Haki za Mtoto na Marekebisho ya Tabia kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Rabikira Mushi katika mahojiano na Star Tv wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Marekebisho ya Tabia na Mpango wa Utoaji Msaada wa Sheria kwa Watoto Wanaokinzana na Sheria.

 Napenda kuchukua nafsi hii tena kuwashukuru sana kwa kunisikiliza.

ASANTENI

Ibrahim H. Juma

KAMU JAJI MKUU

27-07-2017
 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni